read

Aya 43 – 50: Ninawapa Mawaidha Kwa Jambo Moja Tu

Maana

Na wanaposomewa Aya zetu zilizo wazi wanasema: Huyu si chochote ila ni mtu anayetaka kuwazuia na waliyokuwa wakiyaabudu baba zenu. Na wakasema: Haya si chochote ila ni uwongo uliozuliwa. Na wale waliokufuru waliiambia haki pale ilipowajia: Haya si chochote ila ni uchawi ulio dhahiri.

Waliosema ni washirikina wa kiarabu, mtu wanayemkusudia ni Muhammad (s.a.w.). Wamempa wasifa wa uzushi na uchawi kwa sababu aliwataka waachane na mizimu na maagizo ya kijahilia. Pia aliwaambia wajizuie na mambo ya haramu, uovu, kumwaga damu na kuwakandamiza wanyonge. Vile vile aliwataka wafanye mambo kielimu na kiuadilifu.

Hilo ndilo kosa la Mtume mtukufu kwao. Kama unavyoona, ni kosa la mjuzi mwenye ikhlasi mbele ya mjinga mhaini, na la tabibu mwenye kutoa nasaha mbele ya mgonjwa anayejiona ni mzima. Amesema kweli yule aliyesema: “Mjinga anajifanyia mwenyewe ambayo hata adui hawezi kumfanyia adui yake.”

Wala hatukuwapa vitabu wavisome, wala hatukuwatumia muonyaji kabla yako.

Walishirikisha ambapo kila kitu kinafahamisha kuwa Yeye ni mmoja, wakawaiga mababa na mababu bila ya kuwa na hoja ya wahyi ulioteremshwa au Nabii aliyetumwa wala athaari yoyote ya ilimu. Tazama Juz. 17 (22: 1-7) kifungu cha: ‘Mjadala wakijinga na upotevu‘.

Na walikadhibisha wale waliokuwa kabla yao. Na hawakufikilia hata sehemu ya kumi ya tulivyowapa hao. Wakawakadhibisha mitume wangu. basi je, kulikuwaje kukanya kwangu?

Kabla yenu walishirikisha watu wa uma nyingi, waliwakadhibisha mitume; kama manvyokadhibisha nyinyi, nao walikuwa na maendeleo na nguvu zaidi kuliko nyinyi, lakini pamoja na hivyo Mwenyezi Mungu aliwaadhibu kwa dhulma yao na ujeuri wao. Je, hampati funzo na kuhofia kuwafika yaliyowafika wao?

Umetangulia mfano wake katika Juz. 10 (9:70).

Sema: Hakika ninawapa mawaidha kwa jambo moja tu, kwamba msimame kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wawili wawli na mmoja mmoja; kisha mfikiri. Mwenzenu hana wazimu. Hakuwa yeye ila ni muonyaji kwenu kabla ya kuwafikia adhabu kali.

Kusimama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni kushikamana na haki na kuwa mbali na kuiga na kufuata matamanio. Wawili wawili ni mmoja kumrudia mwingine na kuuchunguza mwito na ujumbe. Mmoja mmoja ni kila mmoja kurudia akili yake na dhamiri na kufikiria yale aliyokuja nayo.

Maana ni kuwa ewe Muhammad! Waambie wale wanaokukadhibisha kwamba mimi ninawataka jambo moja tu, uadilifu wa kuchunga haki, mfikirie mkiwa pamoja na mkiwa mbalimbali kuhusu mwito wangu; kisha muangalie, je kweli mimi ni mzushi, mchawi au mwenda wazimu; kama mnavyodai? Au ni mbashiri, muonyaji na mshauri nasaha mwenye busara? Nabii mtukufu aliwapa Watu wa Kitabu mwito kama huu, pale alipowaambia:

قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَىٰ كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلَّا نَعْبُدَ إِلَّا اللَّهَ وَلَا نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا{64}

“Sema: Enyi watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno la usawa baina yetu na baina yenu. Kwamba tusimwabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote.” Juz. 3 (3:64).

Hakuna jambo linalosadikisha zaidi dalili ya ukweli wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), katika aliyokuja nayo, kuliko kuwapa mwito wa haki na uadilifu mahasimu.

Imepokewa Hadith kutoka kwa Ibn Abbas, kwamba Mtume (s.a.w.) siku moja alipanda Swafa na akasema: “Enyi wenzangu! – Neno analolitumia anayetaka kuokoka ikiwa kuna jambo kubwa - basi makuraishi wakakusanyika. Akawaambia: “Mnaonaje kama nikiwaambia adui atawajia asubuhi au jioni, mtanisadiki?” Wakasema: “Ndio!” Akasema: “Hakika ninawaonya na adhabu kali. Abu Lahab akamjibu kwa neno la kukana... lakini hazikupita siku ila walisalimu amri wakiwa wanyonge.

Sema: Ujira niliowaomba ni wenu nyinyi. Sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu. Naye ni shahidi juu ya kila kitu.

Makusudio ya ‘ni wenu nyinyi’ ni kukana swali la ujira. Ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:

فَمَا سَأَلْتُكُمْ مِنْ أَجْرٍ ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَى اللَّهِ ۖ {72}

“...basi mimi siwaombi ujira. Ujira wangu hauko ila kwa Mwenyezi Mungu.” Juz. 11 (10:72).

Sema: Hakika Mola wangu hutoa haki, Mjuzi mno wa ghaibu.

Yaani anatoa wahyi kwa haki kuupeleka kwa mitume yake naye anajua vizuri nani wa kumpelekea ujumbe wake mkuu.

Sema: Haki imefika na batili hajitokezi wala hairudi.

Makusudio ya haki hapa ni risala ya Muhammad (s.a.w.) na batili ni shir- ki. Kujitokeza na kurudi ni kinaya cha kwisha kabisa batili na kutodhihiri athari yake katika Bara Arabu kabisa baada ya risala ya Muhammad (s.a.w.).

Sema: Ikiwa nimepotea basi nimepotea kwa kuidhuru nafsi yangu tu, wala nyinyi madhara yangu hayawahusu.

Na ikiwa nimeongoka basi ni kwa sababu ya kuniletea wahyi Mola wangu.

Ni kwake Yeye peke yake fadhila za kuongoka kwangu; wala sijimilikii wala kummilikia mwingine isipokuwa yale aliyonimilikisha Mwenyezi Mungu.

Hakika Yeye ni Mwenye kusikia aliye karibu.

Mkisema anasikia, mkidhamiria au mkitenda atajua, kwa sababu yeye yuko karibu zaidi na nyinyi kuliko mshipa wa shingo.

وَلَوْ تَرَىٰ إِذْ فَزِعُوا فَلَا فَوْتَ وَأُخِذُوا مِنْ مَكَانٍ قَرِيبٍ {51}

Na lau ungeliwaona watakapofazaika, basi hapana pa kukimbilia, na watakamatwa mahala pa karibu.

وَقَالُوا آمَنَّا بِهِ وَأَنَّىٰ لَهُمُ التَّنَاوُشُ مِنْ مَكَانٍ بَعِيدٍ {52}

Na watasema: Tumemwamini! Lakini watapata wapi kutoka huko mahali mbali?

وَقَدْ كَفَرُوا بِهِ مِنْ قَبْلُ ۖ وَيَقْذِفُونَ بِالْغَيْبِ مِنْ مَكَانٍ بَعِيدٍ {53}

Na walikwishamkataa hapo zamani, wakiyatupilia mbali ya ghaibu kutoka mahali mbali.

وَحِيلَ بَيْنَهُمْ وَبَيْنَ مَا يَشْتَهُونَ كَمَا فُعِلَ بِأَشْيَاعِهِمْ مِنْ قَبْلُ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا فِي شَكٍّ مُرِيبٍ {54}

Na watawekewa kizuizi baina yao na hayo wanayoyatamani, kama walivyofanyiwa wenzao zamani. Hakika wao walikuwa katika shaka ya kutia wasiwasi.