Umaarufu Wake Wa Kielimu
Ingawa aliishi miaka ishirini na nane tu, aliiua kiu ya kisomo ya wanachuoni wengi wa wakati ule na pia aliweza kupambana vya kutosha na mafalsafa wa wakati huo ambao walikuwa wakieneza mambo yaliyokuwa kinyume cha mafundisho ya dini.
Mtu mmoja aliyeitwa Ishaq Kindi alikuwa akiandika kitabu juu ya migongano ya aya za Qur'ani. Habari hizi zilipomfikia Imamu (a.s.) alianza kutafuta nafasi. Siku moja wanafunzi kadhaa wa Ishaq aliwauliza, "Hakuna hata mmoja miongoni mwenu mwenye akili za kutosha kumshauri mwalimu aache upuuzi aufanyao juu ya Qur'ani? Walisema, "Tutafanya nini na sisi ni wafunzi wake tu?" Imamu alisema, "Vizuri, je, mnaweza angalau kumwambia yale ninayowaambieni? " Wakasema, "ndiyo tunaweza kufanya".
Ndipo Imamu alipowaonyesha baadhi ya zile aya za Qur'ani zinazozungumziwa na akawaambia waende wamuulize mwalimu wao kama maneno ambayo alikuwa anayatumia katika hoja zake yana maana hizo tu alizoyachukulia tu au kama kwa kutazama matumizi ya maneno ya Waarabu, maana nyingine za maneno hayo zilipatikana, ambazo kama yakifikiriwa maneno hayo kwa maana hizo yanaondoa suala lolote lile la kupingana kwa aya hizi. Kama zipo maana nyingine, basi alikuwa na haki gani ya kung'ang'ania kuyachukua maneno hayo kwa maana hizo alizozichukulia yeye? Kisha Imamu (a.s.) aliwaeleza wale wanafunzi maana halisi ya aya hizo. Nao wakaenda na wakafanya kama walivyoagizwa. Ishaq alipozisikia zile hoja walizozitoa aliwauliza wamweleze walipojifunza yote hayo. Kwanza, walitaka kuficha lakini aliposisitiza kuwa hayo siyo mawazo yao, walikubali kuwa walijifunza kutoka kwa Abu Muhammad, yaani Imamu (a.s.). Ishaq alisema "Hakuna mwingine ambaye angelifanya hivyo, isipokuwa mtu wa ukoo wa Mtume". Kisha akachoma yale yote aliyokwisha kuandika.
Huu ni mfano mmoja tu wa yale aliyokuwa akiyafanya Imamu kila siku, akielewa kuwa hiyo ni kazi yake akiwa mrithi wa kweli wa Mtukufu Mtume. Na serikali ikidai kuwa ni ya Kiislamu, ilikuwa inafanya mambo ya zinaa na ulevi, na wakati watawala rahisi waliposhika madaraka ilikuwa ni kuongeza vizuizi tu kwa Imamu. Lakini alikuwa mfano halisi wa subira na uvumilivu na hivyo aliendelea katika njia yake ya kazi hii tukufu.
Katika kukusanya Hadithi za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) "wakusanya hadithi" wamechukua hadithi toka kwake. Moja ya hadithi muhimu sana ni ile isemayo, "Mlevi ni sawa na mwenye kuabudu sanamu". Hadithi hii imekaririwa na Bwana Ibn Al-Jauzi katika kitabu chake kiitwacho 'Tabrim-ul-Khamr' (Uharamu wa Kulewa Mvinyo). Na Bwana Abu Na'im Fazl bin Wakin alisema kuwa hadithi hii ni ya kuaminika sana na imechukuliwa kutoka kwenye ukoo wa Mtukufu Mtume na pia imepokewa na kundi la masahaba wa Mtukufu Mtume.
Bwana Sam'ani katika kitabu chake kiitwacho 'Kitab-Al-Ansab' ameandika, "Abu Muhammad Ahmad bin Ibrahim bin Hashim Tusi Baladhuri Hafiz Wa'iz alisikia hadithi ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) huko Maka kutoka kwa Imamu atokanaye na dhuria wa Mtume, Hasan bin Ali bin Muhammad bin Ali bin Musa Al-Ridha na akazikusanya".
Zaidi ya bwana huyu, majina ya wanafunzi wengine mashuhuri wa Imamu yanaorodheshwa hapa chini:
1. Bwana Abu Hashim Dawud bin Qasim Ja'fari aliyekuwa Mwanachuoni mzee ambaye aliwaona Maimamu wanne kutoka lmamu Ali Ridha (a.s.) hadi Imamu Hasan Askari (a.s.) na alisoma kwao wote. Vile vile alikuwa mjumbe wa Imamu Hasan Askari (a.s.).
2. Bwana Dawud bin Abi-Zaid Nishapuri aliwaona Imamu Hasan Askari (a.s.) na baba yake lmamu Ali Naqi (a.s.).
3. Bwana Abu Tahir Muhammad bin Ali bin Hilal.
4. Bwana Abul Abbas Abdullah bin Ja'far Himyari Qummi alikuwa mwanachuoni mashuhuri sana na mwandishi wa vitabu vingi ambavyo miongoni mwao Qurb-al-Asnad bado kipo mpaka leo na ndiyo chanzo cha kitabu kiitwacho Kafi na vitabu vingine.
5. Bwana Muhammad bin Ahmad bin Ja'far Qummi alikuwa mmoja wa wajumbe mashuhuri wa Imamu.
6. Bwana Ja'far bin Suhail Saiqal pia alikuwa mjumbe mashuhuri wa Imamu.
7. Bwana Muhammad bin Hasan Jaffar Qummi alikuwa mwanachuoni mashuhuri na mwandishi wa vitabu kadhaa kati ya hivyo, Basa'irul Darajat kinajulikana. Pia alihifadhi barua walizokuwa wakiandikiana na Imamu Hasan Askari (a.s.) kuhusu sheria za kidini.
8. Bwana Abu Ja'far Humani Barmaki aliandika kitabu cha majibu ya Imamu kuhusu maswali ya sheria za kidini ambayo mwandishi aliandika kumwuliza Imamu (a.s.).
9. Bwana lbrahimu bin Abi Hafs Abu Ashaq Katib, Bwana huyu alikuwa miongoni mwa wafuasi wa Imamu na aliandika kitabu.
10. Bwana Ibrahim bin Mehryar, alikuwa mwandishi wa kitabu kiitwacho 'Kitabul Basharat'.
11. Bwana Ahmad bin Ibrahim bin Isma'il bin Dawud Hamdan Al-Katib Al-Nadim, alikuwa na elimu kubwa ya uandishi wa vitabu na lugha. Aliandika vitabu vingi na alijiambatanisha sana na Imamu.
12. Bwana Ahmad bin Ashaq Al-Ashari Abu Ali Al-Qummi, alikuwa mwanachuoni mwenye elimu ya kutosha. Aliandika vitabu vichache miongoni mwao kikiwemo kitabu kiitwacho "Ilal-Al-Saum", (Falsafa ya Funga).
Haya ni majina machache tu. Pata hitajika kitabu kizima kuweza kuyataja majina yote.
Bwana Abu Ali Hasan Khalidi bin Muhammad bin Ali Barqi aliandika Tafsir (kitabu juu ya ufafanuzi wa Qur'ani Tukufu) kwa njia ya imla aliyosomewa na Imamu. Wanachuoni wa kidini wanasema kuwa kitabu hiki kiligawanywa katika juzuu 120.
Kwa bahati mbaya maandishi haya muhimu sana hayapatikani siku hizi. Hata hivyo katika Tafsiri kadhaa kuna kumbukumbu za Imamu ambazo zinaweza zikawa zinatokana na kitabu hiki. Kitabu kingine juu ya somo hilo kilichopo na kinacho semekana kuwa kimetokana na Imamu hakiaminiki. Waraka mrefu wa Imamu, aliomwandikia Bwana Ishaq bin Isma'il Ash'ari na mkusanyo mkubwa wa hadithi za kuaminika, mafundisho na hotuba vimehifadhiwa katika kitabu Kiitwacho 'Tuhaful-Uqul'.
Yote hii ni kazi ya maisha ya muda wa miaka 28, muda ambao miaka sita tu ndiyo aliyokuwa Imamu baada ya kifo cha baba yake Imamu Ali Naqi (a.s.) na hiyo pia aliitumia katika hali ya majaribio magumu kama ilivyokwisha elezwa awali.