read

Aya 18 – 22: Tukateremsha Maji Kutoka Mbinguni

Maana

Na tumewateremshia kutoka mbinguni maji kwa kiasi.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kusema kuwa hatukughafilika na viumbe, alipigia mfano wa hilo kwa kuteremsha maji kutoka mbinguni kwa kiasi kile kinachowafaa watu; si kingi cha kuwadhuru wala kichache cha kudhuru mimea.

Na tukayatuliza ardhini katika chemchemi, visima, mabawa na mito, ili yawafae watu wakati wa kiangazi.

Na hakika sisi ni wenye uwezo wa kuyaondoa.

Yule aliyeweza kuyaleta bila shaka anaweza kuyaondoa kwa kuyazuia au kuyakausha yasiweze kuwafaa, lakini hakufanya hivyo kwa kuwahurumia.

Basi kwa maji hayo tukawafanyia bustani za mitende na mizabibu, mnapata humo matunda mengi na katika hayo mnakula.

Imehusishwa kutajwa mitende na mizabibu kwa sababu waarabu wakati huo walikuwa hawajui kingine zaidi yake.

Na mti utokao katika Mlima Sinai unaotoa mafuta na kitoweo kwa walaji.

Makusudio ya mti utokao Mlima Sinai ni mzaituni. Mlima Sinai ni ule mlima aliozungumza Musa na Mola wake na kitoweo ni mafuta ambayo hutengenezwa siagi ya kutowelea mkate.

Wafasiri wengi wamesema kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amehusisha kutaja aina hizi tatu kwa sababu ni miti mitukufu zaidi na ina manufaa mengi, lakini ukweli ni kuwa ilikuwa ndio iliyoenea zaidi kwa waarabu.

Umetangulia mfano wake mara nyingi. Angalia kwenye Juz. 14 (16:10).

Na hakika katika wanyama howa; ngamia ng'ombe, mbuzi na kondoo, mna mazingatio mtakayoyazingatia.

Tunawanywesha katika vile viliomo matumboni, maziwa na mnapata katika hao manufaaa mengi, yakiwa ni pamoja sufu, manyoya na ngozi zake. Na katika hao mnawala nyama yake.

Na juu yao na juu ya majahazi mnabebwa kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Umetangulia mfano wake katika Aya nyingi. Angalia Juz. !4 (16:5)

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّهَ مَا لَكُمْ مِنْ إِلَٰهٍ غَيْرُهُ ۖ أَفَلَا تَتَّقُونَ {23}

Na hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake, akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu asiyekuwa Yeye. Basi je, hamna takua?

فَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ قَوْمِهِ مَا هَٰذَا إِلَّا بَشَرٌ مِثْلُكُمْ يُرِيدُ أَنْ يَتَفَضَّلَ عَلَيْكُمْ وَلَوْ شَاءَ اللَّهُ لَأَنْزَلَ مَلَائِكَةً مَا سَمِعْنَا بِهَٰذَا فِي آبَائِنَا الْأَوَّلِينَ {24}

Wakasema wale wakuu waliokufuru: Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi, anataka kujipatia ubora juu yenu. Na lau Mwenyezi Mungu angelipenda, hakika angeliteremsha Malaika. Hatukuyasikia haya kwa mababa zetu wa kwanza.

إِنْ هُوَ إِلَّا رَجُلٌ بِهِ جِنَّةٌ فَتَرَبَّصُوا بِهِ حَتَّىٰ حِينٍ {25}

Huyo si lolote ila ni mtu mwenye wazimu. Basi ngojeni kwa muda.

قَالَ رَبِّ انْصُرْنِي بِمَا كَذَّبُونِ {26}

Akasema: "Mola wangu! Nisaidie kwa kuwa wamenikadhibisha.

فَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِ أَنِ اصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا فَإِذَا جَاءَ أَمْرُنَا وَفَارَ التَّنُّورُ ۙ فَاسْلُكْ فِيهَا مِنْ كُلٍّ زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ وَأَهْلَكَ إِلَّا مَنْ سَبَقَ عَلَيْهِ الْقَوْلُ مِنْهُمْ ۖ وَلَا تُخَاطِبْنِي فِي الَّذِينَ ظَلَمُوا ۖ إِنَّهُمْ مُغْرَقُونَ {27}

Tukampa wahyi: Tengeneza jahazi mbele ya macho yetu. Basi itakapokuja amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize wa kila namna dume na jike, wawili na ahli zako, isipokuwa ambaye kauli imekwishatangulia juu yake katika wao. Wala usinitajie hao waliodhulumu, Hakika wao watagharikishwa.

فَإِذَا اسْتَوَيْتَ أَنْتَ وَمَنْ مَعَكَ عَلَى الْفُلْكِ فَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي نَجَّانَا مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ {28}

Na utakapotulia wewe na walio pamoja nawe jahazini, sema, sifa njema (Alhamdulillah) ni za aliyetuokoa na watu madhalimu.

وَقُلْ رَبِّ أَنْزِلْنِي مُنْزَلًا مُبَارَكًا وَأَنْتَ خَيْرُ الْمُنْزِلِينَ {29}

Na sema, Mola wangu! niteremshe mteremsho wenye baraka na wewe ndiwe mbora wa wateremshaji.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ وَإِنْ كُنَّا لَمُبْتَلِينَ {30}

Hakika katika hilo kuna ishara na kwa hakika sisi ni wenye kuwafanyia mtihani.