Aya 55 – 57: Ukhalifa Wa Waumini Ardhini
Maana
Mwenyezi Mungu amewaahidi wale ambao wameamini na wakatenda mema kuwa hakika atawafanya makhalifa katika ardhi, kama alivyowafanya waliokuwa kabla yao.
Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa umma wowote utakaomwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ukashikana na sharia yake, basi Mwenyezi Mungu atawafanya makhalifa na kuwaimarisha ardhini. Hilo ni hakika.
Baadhi ya wafasiri wamechukua hakika hii, kisha wakafafanua na kufasiri maana ya imani na matendo mema. Wakayawekea mipaka yake na maelezo yake. Ama sisi tuko pamoja na wale waliosema kuwa makusudio ya Aya ni Mtume na maswahaba. Kwani wao walipata tabu na udhia mwingi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kabla na baada ya Hijra. Washirikina na mayahudi kwa pamoja waliwalenga kwa mishale yao.
Hadi kufikia mwaka wa ushindi, walikuwa huko Madina hawawezi kupambazukiwa au kuchwelewa na jua bila ya kushika silaha. Mpaka mmoja wao akasema, kama ilivyo katika tafsir At-Tabari: Hakuna siku tutakayokuwa na amani na kuweka chini silaha yetu. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) akamwambia: 'Hamtakuwa na wepesi (mpaka ikifika ile siku) atakapokuwa mtu anakaa bila ya silaha. Ahadi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikathibitika.
Hazikupita siku, ikawa wanaishi katika amani ya nafsi zao na mali zao, wakatawala nchi zote za urabuni na kuchukua miji mingi ya Ulaya ya mashariki na magaharibi.
Na kwa yakini atawaimarishia dini yao aliyowapendelea.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaishiria kuenea Uislamu na utawala wake mashariki mwa ardhi na magharibi yake.
Na hakika atawabadilishia amani baada ya hofu yao.
Hii ndio natija ya kuvumila, kuwa na subira na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Yamepita maelezo yake kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 9 (8:26)
Wawe wananiabudu, hawanishirikishi.
Shirki haihusiki na kuabudu masanamu peke yake. Atakayemtii kiumbe katika kumuasi Mungu basi huyo yuko katika hukumu ya shirki.
Na mwenye kukufuru baada ya hayo ya kuwa khalifa, kuimarishwa kati- ka ardhi na kuwa na amani baada hofu, basi hao ndio mafasiki na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu mafasiki.
Na simamisheni Swala na toeni Zaka na mtiini Mtume ili mpate kurehemiwa.
Huu ni ubainifu na tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya iliyopita. 'Wale ambao wameamini na wakatenda mema.
Usiwadhanie waliokufuru kwamba watashinda na makazi yao ni motoni na hakika ni marejeo maovu.
Anaambiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kwa lengo la kumhadharisha anayeuhalifu ujumbe wake na akaupinga. Vile vile yeye ni tishio kwa kila mwenye kubadili neema ya Mwenyezi Mungu kuwa kufuru. Katika Nahjul-balagha imeelezwa: "Uchache wa kulazimiana kwenu na Mwenyezi Mungu ni kutotumia neema zake kwa kumuasi."
Njia Nyingine Ya Muujiza Wa Qur'an
Katika Juz.1 (2:23 - 25) kifungu cha 'Siri ya muujiza wa Qur'an,' tulieleza kauli za maulama kuhusu muujiza wa Qur'an. Katika Juz. 3 (3:61) tulisema kwamba kuwa tayari Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) na maapizano kwa kutegemea ushindi ambao umeelezewa na Qur'an na ukawa, ni dalili kubwa ya ukweli wa Qur'an na yule aliyeletewa.
Katika Juz. 6 (5:53) tulieleza kwamba Qur'an ilivyofichua tabia ya mayahudi kwamba wao lau watakuwa na utawala wangefanya kama wafanyavyo leo huko Palestin, ni dalili mkataa ya muujiza wa Qur'an; ambapo yamethibitika hayo baada ya kuyatolea habari kwa zaidi ya miaka elfu moja na mia tatu iliyopita.
Hivi sasa sisi tunapofasiri Aya hii tuliyo nayo 'Mwenyezi Mungu amewaahidi…' tumegundua njia nyingine ya muujiza wa Qur'an. Nayo ni kuwa matamshi ya Qur'an ni ya kiarabu ambayo wameyatumia waarabu katika mazungumzo na maandishi, kabla ya Qur'an na baada yake, bila ya tofau- ti ya herufi au mfumo wa jumla, lakini pamoja na hayo, jumla kwenye Qur'an inabeba maana nyingi, jambo ambalo halipatikani pengine pasipokuwa kwenye Qur'an; hata Hadith pia.
Ndio maana Imam Ali (a.s.) akamwambia Ibn Abbas: "Usigombane na makhawarij kwa Qur'an, kwa sababu Qur'an inachukua sana njia mbalimbali, utasema na wao watasema, lakini wahoji kwa Hadith, hawatakuwa na njia ya kutokea"
Siri katika hilo inakuwa katika upeo wa mwenye kunena sio wa maneno yenyewe. Vinginevyo mfumo wa Qur'an na isiyokuwa Qur'an ungekuwa mmoja tu. Hakika maneno yameganda hayana uhai. Msemaji ndiye anayeyapa uhai. Ndio maana kukawa na tofauti ya uhai wa maneno kulingana na msemaji mwenyewe.
Atakavyozungumza mataalamu ni tofauti na atakavyozungumza mtu wa kawaida, hata kama maneno na jumla zitakuwa sawa. Hata Qur'an pia ufahamu wake unatofautiana kulingana na anayeisoma. Vile vile maneno yoyote yanatofautiana kulingana na anayesema akiwa mnafiki au mwenye ikhlasi.
Kwa hiyo upeo mkubwa wa Qur'an kwa njia mbalimbali ni dalili mkataa kuwa inatokana na ambaye elimu yake imeenea kwenye kila kitu.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِيَسْتَأْذِنْكُمُ الَّذِينَ مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ وَالَّذِينَ لَمْ يَبْلُغُوا الْحُلُمَ مِنْكُمْ ثَلَاثَ مَرَّاتٍ ۚ مِنْ قَبْلِ صَلَاةِ الْفَجْرِ وَحِينَ تَضَعُونَ ثِيَابَكُمْ مِنَ الظَّهِيرَةِ وَمِنْ بَعْدِ صَلَاةِ الْعِشَاءِ ۚ ثَلَاثُ عَوْرَاتٍ لَكُمْ ۚ لَيْسَ عَلَيْكُمْ وَلَا عَلَيْهِمْ جُنَاحٌ بَعْدَهُنَّ ۚ طَوَّافُونَ عَلَيْكُمْ بَعْضُكُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمُ الْآيَاتِ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ {58}
وَإِذَا بَلَغَ الْأَطْفَالُ مِنْكُمُ الْحُلُمَ فَلْيَسْتَأْذِنُوا كَمَا اسْتَأْذَنَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمْ آيَاتِهِ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ {59}
وَالْقَوَاعِدُ مِنَ النِّسَاءِ اللَّاتِي لَا يَرْجُونَ نِكَاحًا فَلَيْسَ عَلَيْهِنَّ جُنَاحٌ أَنْ يَضَعْنَ ثِيَابَهُنَّ غَيْرَ مُتَبَرِّجَاتٍ بِزِينَةٍ ۖ وَأَنْ يَسْتَعْفِفْنَ خَيْرٌ لَهُنَّ ۗ وَاللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ {60}