Uamuzi Wa Historia
Wanahistoria waadilifu wa Kiislamu na Wakikristo wote kwa pamoja wanakubaliana kuwa ndoa alizozifunga Mtume wa Islamu (s) hazikusababishwa na tamaa ya kuitosheleza ashiki yake. Kama ingekuwa hivyo, basi asingemuoa mwanamke aliyekuwa mjane mara mbili, aitwae Khadija, mwenye umri ya miaka 40 na yeye Mtume wa Islamu (s) akiwa kijana wa umri wa miaka 25 tu, umri ambao mtu huwa katika kiwango kamili cha ashiki.
Mtume Muhammad (s) aliishi na mke wake wa kwanza (ambaye wakati ule alikuwa mkewe peke yake), Bibi Khadija (a) kwa furaha, kwa mapenzi na uelewano mkubwa, kwa muda wa miaka 26 ingawaje wasichana wazuri wa Uarabuni waliweza kupatikana kwa urahisi na walikuwa tayari kuolewa na Mtume (s). Muda wote huo (wa miaka 26) Mtume (s) hakuoa mke mwingine. Bila shaka Mtume (s) angelifikiria kuoa mke mwingine aliye na umri mdogo kuliko ule wa Bibi Khadija (a) wakati alipokuwa na Bibi Khadija (a), kama angelikuwa mwenye tamaa za kiashiki na mpenda wanawake; hasa wakati ule ambapo desturi za nchi yake zilikubaliana na ndoa za wanawake wengi.