read

Aya 47 – 48: Wana Wa Israil Tena!

Enyi wana wa Israil ikumbukeni neema Yangu.

Aya hii inatilia mkazo Aya iliyotangulia, na ni maandalizi kwa yatakayokuja baada yake. Tutaonyesha katika sehemu itakayofuatia hekima ya kukaririka. Makusudio ya kukumbuka hapa ni kushukuru; yaanizihukurunineemazangu kwa usikizina twaa.

Na nikawatukuza kuliko viumbe wengine.

Mwenyezi Mungu aliwafadhilisha kuliko mataifa mengine ya wakati huo. Herufi lam katika neno Alamin ni ya kuenea kwa kawaida, sio kuenea kwa kiuhakika. Inatosha kuwa ubora ni katika upande mmoja na sio pande zote. Upande ambao Waisrail wamepambanuka na watu wengine ni kwamba Mwenyezi Mungu aliwapelekea idadi ya Mitume; kwa mfano Musa, Harun, Yoshua, Zakaria na Yahya na wengineo. Wote hao ni Waisrail.

Vyovyote ilivyo, kuwa bora kwao kwa watu wa zama zao kwa upande fulani, hakufahamishi kuwa bora katika kila upande kwa watu wa wakati huo; wala sio kwamba mtu wao ni bora kuliko mtu mwingine.

Bali kule kuwa Mitume wengi wamekuja kutokana na kabila lao ni hoja juu yao na wala sio hoja yao, kwa sababu hilo linafahamisha kwamba wao walikuwa katika upotevu sana, ikawa kuna haja sana wapate waonyaji na wahadharishaji.

Na ogopeni siku mbayo nafsi haitaifaa nafsi nyingine kwa lolote.

Yaani kila mtu na lake hakuna dhahiri wala batini, hakuna kusaidiana wala kuoneana huruma.

يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِيهِ {34}

“Siku ambayo mtu atamkimbia ndugu yake.” (80:34)

Wala hayatakubaliwa kwake (hiyo nafsi) maombezi (shufaa), wala hakitapokelewa kikomboleo; wala hawatanusuriwa. Yaani Kiyama ni sawa na mauti, haufai usaidizi wowote, haitafaa fidiya yoyote, hata ikiwa ghali, wala haitazuia nguvu yoyote hata iwe kubwa kiasi gani. Hakuna chochote isipokuwa Rehema ya Mwenyezi Mungu:

لَئِنْ لَمْ يَرْحَمْنَا رَبُّنَا وَيَغْفِرْ لَنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ {149}

“Kama hataturehemu Mola wetu na kutusamehe, bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliopata hasara. (7:149)

Kukaririka Katika Qur’an

Mara ya pili Mwenyezi Mungu anawaku-mbusha wana Israil neema Zake na amerudia baada ya Aya tano. Hiyo siyo Aya peke yake iliyorudiwa katika Qur’an, zimeka-ririka Aya nyingi hasa zile zinazofungamana na wana wa Israil pamoja na Musa (a.s.). Wengi hujiuliza sababu ya kukaririka Aya.Wameafikiana wafasiri kwamba hekima ya kukaririka ni kutilia mkazo.

Baada ya kupita siku, wakuu wa vyama, wanasiasa, wafanyibiashara na wenye mashirika wamegundua kwamba, kukaririka jambo ndio njia nzuri ya kulipendekeza, kulikinaisha na kulifanyia propaganda.

Kwa ajili hiyo ndio wakaweka mitindo mbali mbali ya matangazo, kukawa na watu maalum wa kuhusika nayo na yakawa ghali sana. Gustave Lebon anasema katika kitabu chake kiitwacho The man and his work: “Mwenye kulikariri tamko mara kwa mara hulibadilisha kuwa itikadi.

Dr Gibson katika kitabu kilichotarjumiwa kwa kiarabu kayfa tufakkir”(Vipi utafikiri)” anasema “Ibara zina sumaku zinapokaririka mara kwa mara mbele ya macho yetu na masikio yetu, zinapumbaza akili zetu kabisa.”

Kwa hivyo basi Qur’an inakariri kwa mfumo mwingine pamoja na kuzidisha makemeo na mengineyo kwa kiasi cha hekima inavyotaka.

Shufaa

Hapana budi shufaa iwe na pande tatu: Mwenye kuombwa, mwenye kuombewa na muombezi ambaye anakuwa kati ya hao wawili, anaomba kwa yule wa kwanza ili amsaidie wa pili ni sawa apate idhini ya yule mwenye kuombwa au la. Hiyo ndiyo Shufaa kwa viumbe. Ama shufaa mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) maana yake ni msamaha na maghufira kwa mwenye dhambi; haitakuwa shufaa mbele ya Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa idhini yake.

Amesema mwenye Majmaul-Bayan “Shufaa kwetu ni yenye kuhusika na kuondoa madhara na kuondoa mateso kwa mumin mwenye dhambi.”

Muutazila na Khawarij wamekanusha Shufa ya Muhammad (s.a.w.) kwa wenye madhambi makubwa katika umati wake, kwa maana hii tuliyoinakili kutoka kwa mwenye Majmaul-Bayan, lakini Imamiya na Ash’aira wameithibitisha kwamba iko.

Akili haihukumu kutokea Shufaa au kutotokea, lakini haioni pingamizi yoyote ya kupatikana. Kwa hiyo, kusihi kwake na kuthibiti kwake kutategemea kunakili kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ambaye kumemthibitikia kunakili huko, basi ni wajibu kwake kuamini Shufaa, na kama hakuthibitikiwa basi atasamehewa. Kwa hali hiyo inatubainika kuwa shufaa si msingi wa dini na kwamba mwenye kuikanusha na huku anamwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi huyo ni Mwislamu bila shaka.

Tukirudi kwenye Aya za Qur’an tunakuta nyingine zinakanusha; kama ile inayosema:

يَوْمٌ لَا بَيْعٌ فِيهِ وَلَا خُلَّةٌ وَلَا شَفَاعَةٌ ۗ{254}

...Siku ambayo hapatakuwa na bishara wala urafiki wala Shufaa (uombezi).... (2:254)

Hapo inaonyesha kukanusha Shufaa kabisa. Na Aya nyingine zinathibitisha kwa sharti; kama ile inayosema:

وَكَمْ مِنْ مَلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِنْ بَعْدِ أَنْ يَأْذَنَ اللَّهُ لِمَنْ يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ {26}

....Hautafaa chochote uombezi (shufaa) wao isipokuwa baada ya Mwenyezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia. (53:26)

Tukiziunganisha Aya mbili hizi na tukazikusanya pamoja, natija itakuwa, Mwenyezi Mungu atakubali Shufaa kutoka kwa mwombezi baada ya kumpa idhini. Sio lazima kupatikana idhini ya Mwenyezi Mungu kwa jina la mmoja mmoja, bali inatosha tu kwa Mtume kujua kwamba Shufaa ni halali ikiwa yule mwenye kuombewa si katika wenye kuwakandamiza watu na kunyang’anya riziki zao; bali ni katika watu wa kawaida tu, ambao wanafanya madhambi ya kawaida.

Kwa maneno mengine ni kwamba makusudio ya idhini ya Mwenyezi Mungu kwa Shufaa ni kumpa wahyi Mtume wake kwamba Mimi nimekuruhusu kuwaombea uwatakao katika Umma wako ambao wamefanya madhambi maalum.

Hapo basi mambo ya hao wenye madhambi yatakuwa mikononi mwa Mtume (s.a.w.); naye atamwombea yule mwenye kustahiki kuombewa. Imethibiti kwamba yeye amesema: “Nimeuweka akiba uombezi wangu kuwaombea wenye madhambi makubwa katika Umma wangu.”

Sisi tuna yakini kuthibiti Shufaa katika Uislamu. Lakini hatujui kwa ufafanuzi; wakati huo huo tunaamini kwa imani ya mkato, kwamba mwombezi bora wa mtu ni matendo yake, na kwamba kitakachowaombea wenye dhambi ni toba. Hakika Mwenyezi Mungu haweki kizuizi kwa mwenye kutaka kuokoka akiwa na ikhlasi na akakimbilia kwenye ukarimu wa Mwenyezi Mungu hali ya kunyenyekea.

وَإِذْ نَجَّيْنَاكُمْ مِنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَسُومُونَكُمْ سُوءَ الْعَذَابِ يُذَبِّحُونَ أَبْنَاءَكُمْ وَيَسْتَحْيُونَ نِسَاءَكُمْ ۚ وَفِي ذَٰلِكُمْ بَلَاءٌ مِنْ رَبِّكُمْ عَظِيمٌ {49}

Na tulipowaokoa kwa watu wa Firaun waliowapa adhabu mbaya; wakiwachinja watoto wenu wakiume na kuwaacha hai wakike; na katika hayo ulipatikana mthihani mkubwa uliotoka kwa Mola wenu.

وَإِذْ فَرَقْنَا بِكُمُ الْبَحْرَ فَأَنْجَيْنَاكُمْ وَأَغْرَقْنَا آلَ فِرْعَوْنَ وَأَنْتُمْ تَنْظُرُونَ {50}

Na tulipoitenga bahari kwa ajili yenu na tukawaokoa, na tukawazamisha watu wa Firaun na hali mwatizama.