Aya 130-134: Na Ni Nani Atajitenga Na Mila Ya Ibrahim
Maana
Na ni nani atajitenga na mila ya Ibrahim isipokuwa anayeitia nafsi yake katika upumbavu? Haya ni matahayarizo kwa Mayahudi na Manasara na washirikina wa Kiarabu ambao hawakumwamini Muhammad. Siri ya matahayarizo haya ni kwamba Mayahudi wanajifaharisha kwa kunasibika kwao na Israil: Na Israil ndiye Yaqub bin Is-hak bin Ibrahim; Manaswara nao wanajifaharisha kwa Isa na nasabu ya Isa kwa upande wa mama inaambatana na Israil vile vile.
Ama washirikina wa Kiarabu wengi wao wanatokana na Adnani nasabu yao inarudia kwa Ismail bin Ibrahim kuongezea kwamba wao walipata heri wakati wa kijahili kwa baraka za nyumba iliyojengwa na Ibrahim.
Kwa hiyo wote wanajifaharisha kwa Ibrahim na mila ya Ibrahim na inajulikana wazi kwamba Muhammad (s.a.w.) anatokana na kizazi cha Ibrahim na yuko katika mila ya Ibrahim. Kwa hivyo mwenye kumkanusha Muhammad na mila yake ndio amemkanusha Ibrahim na mila yake. Hapana shaka kwamba mwenye kukanusha matokeo ya utukufu na fahari yake, basi yeye ni safihi (mpumbavu) sawa na mwenye kufanya mambo ya kumwangamiza yeye mwenyewe.
Hakika sisi tulimtakasa (Ibrahim) katika dunia; Yaani tulimfanya safi mwenye kutakata na uchafu; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنْكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا {33}
Na hakika yeye katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema.
Kwa uwazi kabisa ni kwamba yeye katika dunia yuko hivyo; kwa sababu Uislamu unaiunganisha akhera na amali za duniani; ambaye katika dunia atakuwa mwema na mwenye busara, basi huko akhera pia atakuwa hivyo na ambayekatika dunia atakuwa mwovu na kipofu basi huko akhera pia atakuwa hivyo.
Mola wake alipomwam-bia silimu akasema: Nimesilimu kwa Mola wa walimwengu.
Unaweza kuuliza, Je, Mwenyezi Mungu alimtaka Ibrahim asilimu (anyenyekee) kabla ya kumpa Utume au baada yake? Kwa sababu haiwezekani Mwenyezi Mungu kumpa wahyi asiyekuwa Mtume. Na pia hawezi kuteremsha wahyi kwa mtu ila baada ya kusilimu (kunyenyekea).
Jibu: Hakika kauli yake Mwenyezi Mungu: “Silimu (Nyenyekea)” akasema nimesilim ni fumbo la kuwa Ibrahim ni msafi mwenye Ikhlas na kwamba yeye ndiye mwenye kuchukua utume na ujumbe kwa ukamilifu.
Kwa hivyo makusudio yake ni kumsifu Ibrahim kutokana na Ikhlasi yake, twaa yake na kufuata kwake amri. Wakati huo huo ni matahayarizo kwa Mayahudi, manaswara na washirikina wa Makka ambao wanajifaharisha kwa Ibrahim, kisha wanamuasi na kumpinga yule aliyekuja kuhuyisha mila ya Ibrahim na kueneza desturi na itikadi yake.
Na Ibrahim akawausia haya wanawe na Yaqub pia: Enyi wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu amewachagulia dini hii; basi msife ila nanyi mmekuwa Waislamu.
Yaani thibitini juu ya Uislamu mpaka kufa ili mfufuliwe juu ya Uislamu na mumkabili Mwenyezi Mungu kwa huo Uislamu.
Haki Ya Mtoto Kutoka Kwa Mzazi
Aya hiyo iliyotangulia inatambulisha kwamba mzazi ana jukumu kubwa na malezi ya mtoto wake na kumwongoza kwenye dini ya haki. Imam Zaynul-Abidin (a.s.). Amesema: “Ama haki ya mtoto wako ni kujua kuwa anatokana na wewe na kwamba wewe una jukumu la kuitengeneza vizuri adabu yake na kumfahamisha kuhusu Mola wake Mtukufu na kumsaidia kumtii. Basi mwamrishe amali ambayo anajua kuwa atapata thawabu kwa kufanya wema, na kupata dhambi kwa kufanya mabaya.
Je mlikuwapo yalipomfikia Yaqub mauti.
Kumfikia mauti ni wakati wa kufa, alipopata alama za kufa. Mwenye Majmau anasema: “Mayahudi wanadai kuwa Yaqub alipokufa aliwausia wanawe kushikamana na Uyahudi. Ndio Mwenyezi Mungu akabatilisha madai yao juu ya Yaqub; sasa vipi mnadai mambo ya uongo?”
Kwa hakika ni kwamba Yaqub aliwaambia wanawe: “Je mtaabudu nini baada yangu?”
Unaweza kuuliza kwamba neno ‘nini’ hutumiwa kwa kisicho na akili, sasa imekuaje hapa kutumiwa kwa mwenye kuabudiwa kwa haki?
Jibu: Wakati huo watu walikuwa wakiabudu masanamu, ndipo likaletwa swali kutokana na vile wanavyoabudu sio kutokana na uhaki wa kuabudu. Kwa hiyo maana itakuwa ni kitu gani mtaabudu?
Wakasema: “Tutamwabudu Mola wako na Mola wa baba zako, Ibrahim na Ismail na Is-hak, Mungu mmoja tu, na sisi tunasilimu Kwake.”
Unaweza kuuliza Yaqub ni moto wa Is-hak, na Ismail ni ami yake (ndugu wa baba yake) sasa imekuwaje kumwingiza Ismail pamoka na mababa?
Jibu: Ami yuko katika daraja ya baba kwa sababu ni nduguye na anaadhimishwa kama anavyoadhimishwa baba. Iko Hadith ya Mtume (s.a.w) inayosema; kuwa Mtume alisema: ‘Nirudishieni baba yangu.” yaani ami yake Abbas.
Huo ni umma uliokwishapita. utapata ulioyachuma, nanyi mtapata mtakayoyachuma.
Aya hii inaashiria kawaida ya mambo, kwamba natija za amali zote na athari zake zitamrudia mwenye kutenda peke yake, hawezi kunufaika nazo mwenye nasaba naye na wala hazitamdhuru mwingine. Uislamu umethibitisha kawaida hii kwa mifumo mbali mbali ya maneno, kama vile anavyosema Mwenyezi Mungu:
“...Wala hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine” (6:164)
“Na kwamba mtu hatapata ila yale aliyoyafanya.” (53:39)
Pia Mtume (s.a.w.) amesema kumwambia mwanawe Fatima: “Ewe Fatima! Fanya amali wala usiseme mimi ni binti wa Muhammad, kwa sababu mimi sitakutoshea wewe na kitu chochote kwa Mwenyezi Mungu.” Na mengineyo. Kufafanua zaidi maudhui haya kutafahamisha kwamba mpaka leo sisi hatujui mambo yaliyo wazi kabisa.
وَقَالُوا كُونُوا هُودًا أَوْ نَصَارَىٰ تَهْتَدُوا ۗ قُلْ بَلْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۖ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ {135}
قُولُوا آمَنَّا بِاللَّهِ وَمَا أُنْزِلَ إِلَيْنَا وَمَا أُنْزِلَ إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ وَمَا أُوتِيَ مُوسَىٰ وَعِيسَىٰ وَمَا أُوتِيَ النَّبِيُّونَ مِنْ رَبِّهِمْ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِنْهُمْ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ {136}
فَإِنْ آمَنُوا بِمِثْلِ مَا آمَنْتُمْ بِهِ فَقَدِ اهْتَدَوْا ۖ وَإِنْ تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا هُمْ فِي شِقَاقٍ ۖ فَسَيَكْفِيكَهُمُ اللَّهُ ۚ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ {137}
صِبْغَةَ اللَّهِ ۖ وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللَّهِ صِبْغَةً ۖ وَنَحْنُ لَهُ عَابِدُونَ {138}