read

5. Shirki Ni Nini Na Si Nini

Kwa taarifa tuliyoitoa (na tunaomba tuelezwe kama tumeacha kitu katika taarifa hiyo), kati ya madondoo sita yaliyonukuliwa na ndugu zetu hao, matano yametushinda kuelewa vipi yaweza yakawa ni shirki. Kwa hivyo hatutashughulika nayo kwa leo mpaka hapo tutakapofafanuliwa inshallah. Tutakaloshughulika nalo leo ni moja tu lililobaki ambalo, kwa hujja walizozitoa kulipingia, tumeweza kulifahamu lililowafikirisha wao kuwa ni shirki. Nalo ni lile la Buswiri kusema katika Burdah: "Haukupata kunipiga vita Ulimwengu nikataka nusra kwa Mtume ila huipata tu."

Kulikosoa hilo, Ahlu-Tawheed wameitaja Sura 3:126 ambayo wameifasiri hivi: "Na msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu na Mwenye hikima". Kwa kuitaja aya hii, kwa hivyo, tumeelewa kwamba ndugu zetu hao wameyaelewa maneno ya Buswiri hivi: "Kwa kuwa msaada (nasr) hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, kuuomba kwa mtu mwengine yoyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu, hata awe ni Mtume (s.a.w.w.), ni sawa na kumfanya mtu huyo ni Mwenyezi Mungu! Na kufanya hivyo ni shirki; kwa hivyo katika Burdah muna shirki!"

Majibu Yetu

Kwanza; katika tafsiri yao ya hiyo Sura 3:126 wameongeza maneno katika pinde, tuliyoyachapa kwa italiki, ambayo hayamo katika aya hiyo, wala hayaipunguzii maana lau yasingeongezwa.

Pili; kama maana ya "msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu" ni kwamba haturuhusiwi kutafuta msaada kwa asiyekuwa Yeye, au asiyekuwa Yeye hana msaada wa kuutoa, basi ilikuwaje watu wa Madina wakaitwa answaar (wasaidizi)? Walimsaidia nani? Huyo aliyesaidiwa, aliukosa msaada wa Mwenyezi Mungu hata wakaingia kati wao? Na sisi Waislamu, pamoja na Mtume wetu (s.a.w.w.), tunamshirikisha Mwenyezi Mungu kwa kuwaita answaar watu wa Madina?

Tunaposoma Sura 3:81 tunaona jinsi Mwenyezi Mungu alivyochukua ahadi kwa Mitume Yake kwamba itamsaidia / itamnusuru (latansurunnahuu) Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Jee, kama "msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu," ilikuwaje hapo, Yeye Mwenyewe, akautaka kwa asiyekuwa Yeye? Jee, kwa kitendo hicho, Mwenyezi Mungu -- Mwenyezi Mungu apishe mbali! -- alikusudia kuifanya Mitume Yake ni miungu?

Katika Sura 7:157, kati ya sifa za waumini ambao "ndio wenye kufaulu", ni wale ambao wamemsaidia / wamemnusuru (wanaswaruuhu) Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Jee, kama "msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu", kwa nini akawaagiza waumini wamsaidie Mtume Wake? Kwa sifa hiyo hapo, ndio Mwenyezi Mungu amewafanya waumini kuwa ni miungu? Mwenyezi Mungu -- Mwenyezi Mungu apishe mbali -- hapo amefanya shirki?

Hali kadhaalika; tunaposoma Sura 28:15 tunaona jinsi jamaa yake Nabii Musa (a.s) "alivyomuomba msaada" (fastaghaathahuu) juu ya adui yake. Jee, Nabii Musa (a.s) alimrukia jamaa yake huyo, na kumwambia asilete shirki kwa kumuomba yeye msaada badali ya Mwenyezi Mungu? La! Alimsaidia; na siku ya pili (Sura 28:18) yule aliyeomba msaada jana (istanswarahuu) akamuomba tena! Jee, kama "msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu", kwa kutoa msaada wake huo, Nabii Musa (a.s) alikuwa Mwenyezi Mungu, au hakujua kuwa "msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu"?

Kwa kutaja mifano hiyo hapo juu, sisi tusomao maulidi hatukusudii kukanusha yaliyomo katika aya iliyotajwa na wapinga maulidi, kuwa "msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu"; hasha! Tunalokusudia ni kufahamisha kwamba: maneno yanapofanana, si lazima na maana yafanane (yawe mamoja). Kwa hivyo, msaada ambao Buswiri aliuomba kwa Bwana Mtume (s.a.w.w.), na sisi huukariri tunapoisoma hiyo Burdah, sio msaada ambao huombwa kwa Mwenyezi Mungu. Ni majina tu kufanana -- kama ulivyokuwa ule ambao Mwenyezi Mungu alimtakia Mtume Wake kwa Mitume mengine, na aliotutaka sisi waumini tumpatie Mtume Muhammad (s.a.w.w.), na ambao watu wa Madina walimpatia Bwana Mtume (s.a.w.w.) hata wakaitwa answaar (wasaidizi wake), na ule ambao Nabii Musa (a.s) alimpatia jamaa yake.

Msaada wa Mwenyezi Mungu unatokana na Yeye Mwenyewe; hakupawa na yoyote uweza huo wa kusaidia. Lakini wa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, akiwamo Mtume Muhammad (s.a.w.w.), si wake mwenyewe; ni wa kupawa (kuwezeshwa na Mwenyezi Mungu). Na hapo ndipo palipo na tafauti baina ya shirki ni nini, na si nini.

Ukiamini kwamba Mtume (s.a.w.w.) -- yeye mwenyewe, bila ya kupawa uweza huo na Mwenyezi Mungu -- aweza kusaidia; hiyo ni shirki. Na hilo silo alilokuwa akiliamini Buswiri, wala silo tunaloliamini sisi tusomao maulidi. Lakini ukiamini kuwa msaada uwezao kupawa na Mtume (s.a.w.w.) ni ule aliowezeshwa yeye na Mwenyezi Mungu; hiyo si shirki. Na hilo ndilo alilokusudia Buswiri katika Burdah, na ndilo tunaloliamini sisi tunaosoma maulidi. Kwa hivyo kubwa ambalo wapinga maulidi waweza kutwambia sisi ni kuwa Mtume (s.a.w.w.) hakuwa / hana uweza huo; kwa hivyo ni kazi bure kumuomba hivyo -- jambo ambalo hatulikubali kwa sababu ya hujja tulizonazo. Lakini hawawezi kutwambia ni shirki, kwa mifano mingi tuwezayo kuwatolea katika Qur'ani Tukufu.

Wapinga Maulidi Hupotea Wapi

Wapinga maulidi, wanaposoma vitabu vya maulidi, wakaona kuwa Mtume (s.a.w.w.) amesifiwa kwa neno alilosifiwa Mwenyezi Mungu, au kitendo chake kimetajwa kwa neno ambalo, kwa kawaida, hunasibishwa nalo Mwenyezi Mungu -- wanapoona hayo, moja kwa moja husema ni shirki, kwa sababu hivyo ndivyo wanavyoielewa wao shirki, na hali hivyo sivyo.

Neno lililotumiwa kumsifia Mwenyezi Mungu, linapotumiwa kumsifia Mtume (s.a.w.w.), halimfanyi Mtume kuwa ni Mungu (kwa hivyo si shirki) kama ambavyo, vile vile, neno lililotumiwa kuelezea kitendo cha Mtume (s.a.w.w.), halimfanyi Mtume kuwa ni Mungu. Kwa kutolielewa hili ndipo wapinga maulidi -- wao na viongozi wao -- walipokosea na kudai kuwa vitabu vya maulidi vina shirki!

Kuthubutisha kosa lao hilo, hapa chini tunayataja mifano michache tu (sio yote) kutoka katika Qur'ani Tukufu:

1. Tunaposoma Sura 2:143, tunamuona Mwenyezi Mungu anavyojisifu kuwa Yeye ni rauufun (Mpole) na rahiimun (Mwenye kurehemu). Na tunaposoma Sura 9:128, tunamuona Mwenyezi Mungu, Yeye Mwenyewe, anamsifu Mtume Wake (s.a.w.w.) kwa sifa zizo hizo za rauufun rahiimun! Jee, kwa kufanana matamko ya sifa hizo, Mwenyezi Mungu alikusudia kumfanya Mtume Wake ni Mungu kama Yeye? Jee, sisi tunapomsifu Mtume kwa sifa hizo, huwa tumefanya shirki kwa sababu tu matamko yaliyotumiwa yanafanana?

Jawabu ni: La! Isipokuwa kama tutaamini kuwa uraufu na urahimu wa Mtume (s.a.w.w.) ni sawa na ule wa Mwenyezi Mungu! Na hilo, sisi watu wa maulidi, hatulisemi wala hatuliamini. Tunaloliamini sisi ni kwamba uraufu na urahimu wa Mwenyezi Mungu ni Wake Mwenyewe kwa asili (bil aswaala / independently); wa Mtume (s.a.w.w.) ni wa kupawa na Yeye, Mola wake. Kama kumsifu Mtume kwa sifa hizo ni shirki kwa sababu tu zimefanana na za Mwenyezi Mungu, basi na wapinga maulidi nao pia ni mushrikina kwa sababu hatuamini kwamba wanapoifikia aya hiyo (Sura 9:128), kama Waislamu, huiruka wakaacha kuisoma, au huibadilisha maneno yake.

2. Tunaposoma Sura 16:70, tunaona kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyetuumba na ndiye anayetufisha / anayetuuwa (yatawaffaakum); na tunapoisoma Sura 32:11, tunaona kwamba atakayetufisha (yatawaffaakum) sisi ni "malaika wa mauti". Sasa tushike lipi hapo, maana neno lililotumiwa kuelezea kitendo hicho cha kutoa roho ni lilo hilo moja: yatawaffaakum? Afishaye ni Mwenyezi Mungu, au ni huyo malaika?

Tukisema ni Mwenyezi Mungu peke Yake, tutakuwa tunaikanusha Qur'ani kwa sababu Qur'ani yiyo hiyo imetwambia kuwa na malaika huyo naye huifanya kazi hiyo. Na tukisema ni malaika peke yake, tutakuwa vile vile tunaikanusha Qur'ani kwa sababu Qur'ani yiyo hiyo imetwambia kuwa Mwenyezi Mungu naye huifanya kazi hiyo. Sasa ni nani basi? Ni wote wawili?

Jawabu ni: Ndiyo! Ni wote wawili; lakini pana tafauti. Japokuwa maneno (yatawaffaakum) yaliyotumiwa yanafanana, tawaffaa ya Mwenyezi Mungu si sawa na ya malaika. Ya Mwenyezi Mungu ni ya uweza Wake alionao Yeye Mwenyewe kwa asili. Ile ya malaika si hivyo. Yake ni ya "kuwakilishwa" (alladhii wukkila bikum) na Mwenyezi Mungu, kama aya yake (Sura 32:11) inavyofafanua. Kwa hivyo, ukiamini hivyo; hiyo si shirki. Lakini ukiamini kuwa uweza wa kufisha alionao malaika ni sawa na ule alionao Mwenyezi Mungu; hiyo, bila shaka yoyote, itakuwa ni shirki. Na ni Mwislamu gani anayeamini hivyo?

3. Tunaposoma Sura 22:6, tunaona kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anayefufua (yuhyii) wafu; na tunaposoma Sura 3:49, tunamuona Nabii Isa (a.s), mtume wa Mwenyezi Mungu, anasema kuwa yeye naye anafufua (uhyii) wafu! Sasa basi, kwa kusema hivyo, Nabii Isa hapo alijifanya ni Mungu? Au sisi, tunapoisoma aya hiyo katika Qur'ani, huwa tunamshirikisha Nabii Isa na Mwenyezi Mungu?

Jawabu ni: Ndiyo, kama tutaamini kuwa Nabii Isa (a.s) alikuwa nao uweza huo yeye mwenyewe. Lakini kama tutaamini, kama alivyoeleza yeye mwenyewe Nabii Isa katika aya yiyo hiyo, kuwa aliweza kufanya hilo "kwa idhini ya Mwenyezi Mungu" (bi idhnillaahi), hapo hatutakuwa tumemshirkisha na Mwenyezi Mungu japokuwa neno lililotumiwa kwa wote wawili -- yuhyii na uhyii -- ni lilo hilo moja.

4. Tunaposoma Sura 25:2, tunaona kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba kila kitu. Sisi binadamu (Sura 32:7) alituumba (khalaqa) kwa udongo, kisha (Sura 32:9) akatuvivia / akatupulizia (nafakha fiihi) roho Yake, tukawa. Hali kadhaalika Nabii Isa (a.s); kwa mujibu wa Sura 3:49 anasema, "…Ninawaumbia nyinyi (akhluqu lakum) kwa udongo, kama sura ya ndege, kisha nampuliza (anfukhu fiihi), mara anakuwa ndege …"

Jee, Nabii Isa hapo alikuwa Mungu? Au sisi Waislamu -- tunaosoma maulidi na tunaoyapinga -- tunapoisoma aya hiyo, pamoja na kuwa ametumia maneno yale yale (akhluqu lakum na anfukhu fiihi) yaliyotumiwa na Mwenyezi Mungu, humfikiria Nabii Isa (a.s) kuwa ni Mungu? Hasha! Kwa nini? Kwa sababu, katika aya hiyo hiyo, amesema kuwa ameweza kulifanya hilo "kwa idhini ya Mwenyezi Mungu" (bi idhnillaahi); si kwa uweza wake yeye mwenyewe.

Kwa mifano mine hiyo tuliyoitaja hapo juu, tumeona kwamba linalozingatiwa katika kuhukumu jambo kuwa ni shirki au la, si maneno yanayotumiliwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kufanana; hasha! Linalozingatiwa ni hilo tunalomnasibisha nalo Mtume, au kiumbe yoyote, linatokana na uweza alionao yeye mwenyewe kwa asili au aliopawa na Mwenyezi Mungu? Tukiamini hilo la kwanza,, itakuwa ni shirki. Tukiamini hilo la pili, itakuwa si shirki. Na hili ndilo aliloliamini Buswiri na wanaoyakubali ya Burdah: kwamba uweza alionao Mtume (s.a.w.w.) wa kutoa msaada ni wa kupawa na Mwenyezi Mungu; si wake mwenyewe kwa asili.