Aya 27 -29: Soma Uliyopewa Wahyi
Maana
Na soma uliyopewa wahyi katika kitabu cha Mola wako. Hapana wa kubadilisha maneno yake.
Anasema Mwenyezi Mungu kumwambia Mtume wake mtukufu: Fikisha tuliyokuteremshia yanayohusiana na watu wa pango na wengineo katika yaliyokuja kwenye Qur’an Tukufu. Kuwa na yakini na yale tunayokupa habari. Amesema kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume wake.
Siku na matukio yamethibitisha kuwa Muhammad (s.a.w.) ni rehema iliyoongozwa kutoka mbinguni kwa ajili ya watu. Kila zama zinavyozidi kuendelea ndio unapatikana ushahidi wa hakika hii.
Wala hutapata makimbilio isipokuwa kwake.
Yaani huna pa kumkimbia Mungu. Maneno anaambiwa Muhammad (s.a.w.). Maana yake ya dhahiri ni kuwa wewe Muhammad una majukumu mbele ya Mwenyezi Mungu wala hutapona ukiwa utatia shaka katika haki- ka ya Qur’an au kufanya uzembe katika kuifikisha.
Hasha!HaiwezekanikwaMtumewarehemakutiashakaaukufanyauzembe. Vipi iwe hivyo na hali Mwenyezi Mungu anajua zaidi pa kuuweka ujumbe wake! Isipokuwa makusudio ni kumweleza yule anayetia shaka katika utume wa Muhammad (s.a.w.) au kuhalifu aliyokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanaomuomba Mola wao asubuhi na jioni, wakitaka radhi yake; wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka mapambo ya maisha ya dunia; wala usimtii tuliyemghafishilisha moyo wake asitukumbuke na akafuata matamanio yake na mambo yake yakawa yamepita kiasi.
Ikisemwa isuburishe nafsi yako pamoja na fulani; yaani kuwa naye. Makusudio ya wanaomuomba Mola wao ni wale waumini wenye ikhlasi. Asubuhi na jioni ni fumbo la kudumu kwenye twaa ya Mungu. macho yako yasiwaruke kwa kutaka mapambo ya dunia; yaani usigeuze umuhimu wako kutoka kwa watu wa dini ukaenda kwa watu wa dunia. Walioghafishilishwa ni makafiri na wenye makosa. Kupita kiasi mambo ni kauli na vitendo kupituka haki na uadilifu.
Imepokewa kuwa Uyayna - mmoja wa viongozi wa washirikina - alikwenda kwa Mtume (s.a.w.) akaona mafukara wamekaa naye, akiwemo Salmani Farisi akiwa na kilemba kilichojaa jasho na mkononi akiwa na jani la mtende.
Uyayna akasema: “Huu uvundo wa hawa haukusumbui wewe. Sisi vigogo wa Mudhar tukisilimu watasilimu watu wengi. Hakuna kinachotuzuia isipokuwa wafuasi wako hawa tu. Hebu achana nao tukufuate sisi au uwafanyie kikao chao na sisi tuwe na kikao chetu.” Ndipo ikashuka Aya hiyo.
Sisi hatujui usahihi wa mategemezi ya riwaya hii, lakini tunaitilia nguvu kwa sababu inaenda na muktadha wa hali; yaani hali ya wapenda makuu na kujifanya wakubwa wakiwadharau wanyonge. Hilo limenukuliwa na Qur’an:
وَمَا نَرَاكَ اتَّبَعَكَ إِلَّا الَّذِينَ هُمْ أَرَاذِلُنَا بَادِيَ الرَّأْيِ {27}
Kabla ya Mtume (s.a.w.) kumjibu Uyayna na mfano wake kuwa ndio au hapana, aliye Mtukufu na kutuka akamwambia: kuwa pamoja na waumini, kwa vile wao wako pamoja nami, nami niko pamoja nao na uvumilie na wanayoyasema wapenda makuu. Kwa sababu subira yako kwao ni subira ya Mwenyezi Mungu na utiifu wake. Kwani huoni imani yao na ikhlasi yao kwangu na kwako katika kila kitu, wakitaka radhi yangu na thawabu zangu?
Ama waovu waliopofushwa na matamanio ya nyoyo zao, wanaofanya mambo kwa masilahi yao tu, wakikataa kuishi na wengine kwa haki na uadilifu, isipokuwa kiburi na kujikweza na kupituka mipaka yote ya Mwenyezi Mungu na ya binadamu. Hawa usiwasikilize. Kwani kauli yao hiyo ni ushenzi, uongo na upotevu; bali ni juu yako kupambana nao na kuwawekea ngumu kwa kauli na vitendo:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قَاتِلُوا الَّذِينَ يَلُونَكُمْ مِنَ الْكُفَّارِ وَلْيَجِدُوا فِيكُمْ غِلْظَةً ۚ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ {123}
Sema hii ni kweli itokayo kwa Mola wenu.
Anaambiwa Mtume awaambie wale walioghafilishwa nyoyo zao au watu wote. Hii ni usisitizo wa kauli iliyotangulia ya wasomee uliyopewa wahyi
Basi atakaye aamini na atakaye akufuru.
Hii ni sawa na kauli yake Mungu:
إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا {3}
Aya hii inafahamisha kuwa mtu ana hiyari sio mwenye kuendeshwa. Lakini Razi amemrudi mwenye kutoa dalili kwa Aya hii kwamba utashi wa mtu haufanyi yeye mwenyewe, bali unafanywa na Mungu kwa hiyo kwake yeye mtu ni mwenye kuendeshwa hana hiyari.
Nasi tunamjibu: Hakika utashi wa mtu unatokana na sababu na mazingira yanayomzunguka. Mfano mtu kumuona mwanamke mzuri nafsi yake ikampondokea, na hali dini imewajibisha mtu kuizuiwa nafsi yake, katika hali hii.
Hakuna mwenye shaka kwamba hili liko chini ya uwezo wake mtu (anaweza kulizuia). Mtume wa Mwenyezi Mungu ameliita hilo ‘Jihadi kubwa.’ Kuna riwaya isemayo kuwa Mtume alituma kikosi cha wapiganaji.
Kiliporudi, akasema: Karibuni watu waliomaliza jihadi ndogo na kubakiwa na jihadi kubwa.” Akaulizwa ni ipi jihadi kubwa ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: Jihadi ya nafsi. Hakika jihadi bora ni ya yule mwenye kufanya jihadi ya nafsi yake ambayo iko baina ya mbavu zake.
Hakika sisi tumewaaandalia wenye kudhulumu moto ambao hema lake litawazunguka. Na wakiomba msaada watapewa maji kama mafuta yaliyotibuka yanayobabua nyuso. Kinywaji kibaya kilioje na mahali pabaya palioje pa kupumzika!
Hili ni onyo na hadhari kwa kwa yule anayeathirika na ukafiri kuliko imani na batili kuliko haki, kwamba adhabu itazunguka pande zote; sawa na hema linavyomzunguka mtu, na watendela kupata kila aina ya dhabu.
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ إِنَّا لَا نُضِيعُ أَجْرَ مَنْ أَحْسَنَ عَمَلًا {30}
أُولَٰئِكَ لَهُمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِنْ ذَهَبٍ وَيَلْبَسُونَ ثِيَابًا خُضْرًا مِنْ سُنْدُسٍ وَإِسْتَبْرَقٍ مُتَّكِئِينَ فِيهَا عَلَى الْأَرَائِكِ ۚ نِعْمَ الثَّوَابُ وَحَسُنَتْ مُرْتَفَقًا {31}