read

Husaini Mwana wa Ali

Naanziliza kwa jina
Lake yeye Subhana
Mola asiye kijana
Wala mke asiliye

Ndie watangu natangu
Kabula ya ulimwengu
Muumba nchi na mbingu
Milele Atabakiya

Asie na mshirika
Na wala hakuzalika
Ameketi pasi shaka
Enzie imetimiya

Sasa penda kuweleza
Kisa chenye kuchukiza
Na moyo nitaukaza
Hadi mwisho kufikiya

Ni rafiki wa Rasuli
Muhammadi mur sali
Husaini mwana wa Ali
Na Fatima Hashimiya

Kipenzi chake Nabiya
Kuliko viumbe piya
Uhai wake sikia
Husaini akimwambiya

Wewe mtu wa peponi
Huna shaka asilani
Apendae kubaini
Namtizame Husaini

Baada kufa Rasuli
Muda ulipotawili
Na Alii mjamali
Alipoaga duniya

Kukazidi wasiwasi
Ulimwengu ukahisi
Pasiwe mwenye nafasi
Matumbo kupiganiya

Baada yote kufika
Na damu zikimwaika
Waso haya wakatoka
Vita wakaandaliya

Vikaandaliwa vita
Na mengi mno matata
Umbea nausalata
Vigaro vikatimiya

Vigaro vya mahasidi
Nyoyo zenye ufisadi
Chini ya yeye Yazidi
Vitani wakaingia

Husaini yuko ndiani
Kutaka ihami dini
Kuwapinga mashetani
Nakuituza duniya

Kwa moyo uso imani
Majeshi yakawa kani
Na damu waitamani
Ya Husaini na dhuriya

Wakawa wajikatakata
Watakayo washapata
Na Imamu washamwita
Mjini kwao kwingiya

Habari hiyo hanayo
Amekaza wake moyo
Kumbe mambo sasa siyo
Mauti yamngojea

Yunjiani enda zake
Akaweta watu wake
Waume na wanawake
Na radhi akawiliya

Kuwajuza kwa yakini
Hila zote kwa makini
Pasipo matumaini
Iraqi kufikiliya

Kawambiya kimbieni
Atakae samahani
Ila mimi niwacheni
Nimuhali kukimbiya

Baada yeye kukuli
Wengi hawakuhimili
Kama vile mafahali
Nyumbani wakarudia

Akabakiya Husaini
Na dhuriya wa nyumbani
Na baadhi ikhiwani
Akali wakasaliya

Alipofika Iraqi
Jamii ya halaiki
Furaha na kujinaki
Jeshi likamwingilia

Akawa hana namna
Pande zote amebanwa
Pamwe na wake vijana
Wapi watakimbiliya

Akasema kwa lafudhi
Kwa fasaha na mahadhi
Adui kuwapa radhi
Kuwatajia Jalia

Akawaonya mifano
Hati zao za mkono
Barua zilizo nono
Walizo kumwandikia

Kayesha yote maneno
Wala pasipo usono
Yote yasiwe ni neno
Yao wakashikilia

Wakamuonya adhabu
Na nyingi mno sulubu
Zimewaingia ghadhabu
Bila sababu ya njia

Adui pasi kuchoka
Wakamwandama M-maka
Karbala wakafika
Kusudi wa mwandamiya

Furati wakaushika
Pasi nafasi kutoka
Mto wakauzunguka
Na maji wakijinyweya

Kiu ikazidi sana
Na joto likawabana
Imamu na wake wana
Dhiki ikawadhidiya

Ikawa hakuna budi
Dhiki imeshawazidi
Wazee kwa auladi
Roho zikiteketea

Kiu ilo kubwa mno
Joto lisilo kifani
Vijana wazi midomo
Maji wanahitajiya

Maji wanywayo wanyama
Punda farasi na kima
Mjukuu wa Hashima
Adui akazuwiya

Akenda kwao salama
Karibu roho kutema
Abdallah anawana
Kwa kiu kumzidiya

Kile kijana swaghiri
Imamu wetu Amiri
Tamaa hakukasiri
Ya mali kumpatiya

Adui wasikubali
Japo lau tone mbili
Mahali wakaratili
Pasi imani kuingiya

Ndipo akikariri
Imamu akihubiri
Alipata takisiri
Chembe wakamrushiya

Wakamba ha ndiyo maji
Katu huyaonji maji
Mnyweshe yamfereji
Ni leo mtatubiya

Kijana kikalalama
Chembe limeshika nyama
Na damu mwili nzima
Mikononi kikafiya

Mikononi mwa Imamu
Yote ikajaa damu
Na roho yake ghulamu
Ikaiaga duniya

Katu wakamba adui
Maji yetu situmai
Mtayaona jamii
Kinywani hamtotiya

Ukazidi ukaidi
Kwa jeshi la mafisadi
Ikawa hapana budi
Roho zikiteketeya

Basi huu ndiyo mwanzo
Wakazidisha mikazo
Pasiwe hata pumbazo
Vitoto vikiumiya

Kajaribu kwa upole
Kuwaeleza walo pale
Maji yote yako tele
Japo tone kutumiya

Akenda huko karibu
Kiu ilimughilibu
Alipotaka jaribu
Chembe kikamuingiya

Kikamwingia Imamu
Chembe chao mahasimu
Mdomoni kikadumu
Na damu ikamweneya

Huku kiu imemshika
Damu ikichirizika
Msiba umemfika
Hana pakukimbiliya

Kakishika kakizuwa
Kwa nguvu akakitowa
Kamshukuru Molawa
Muumba wa waja piya

Zikazidishwa sulubu
Mno na nyingi taabu
Rafikize wakaghibu
Mauti kuyandamiya

Rafiki wakaanguka
Imamu kumzunguka
Na damu zikimwaika
Akawa aogeleya

Katikati kwenye damu
Adui wakakalimu
Katu yako hayatimu
Mauti yakungojeya

Mauti yenye taabu
Usumbufu na adhabu
Yatakufika karibu
Kaa ukiliadhaniya

Ni leo, leo ni leo
Utaiona kwa leo
Na wote hao watu
Wote tutawalemeya

Kakalimu muungwana
Kamshukuru Rabana
Na Molawe kalingana
Na dua kujiombeya

Akatamka Husaini
Kamwambia Mola manani
Kwako wewe shukrani
Nyoyo zimefurahiya

Hatuna katu huzuni
Kwa ulio yasaini
Mauti twayatamani
Kuliko kuangukiya

Vita vikauma sana
Pasipo kusemeyana
Na Imamu akawana
Pasi nyuma kurejeya

Lakini ifae nini
Kwa adui elfeni
Na ziyada ilondani
Husaini akalegeya

Akalegeya kwa dhiki
Aloikuta hilaki
Asimpate rafiki
Huruma kumuoneya

Ukweli ulodhihiri
Ikakabili ni shari
Haikuweko ni siri
Shida zikawachachiya

Kutamka kwa upole
Pasipo nyingi kelele
Sahibuze kuwambile
Atakaye kukiribiya

Usiku huo gizani
Kawambia kimbiyeni
Na mimi radhi moyoni
Na dua nawaombeya

Jamii wakakataa
Heri kwao kujifia
Kuliko kuyakimbia
Mauti wakaridhiya

Adui likadhihiri
Moyo umetahayari
Na upesi ikaswiri
Imamu kumjiliya

Mtoto wake Husaini
Naye alipobaini
Karuka pasi makini
Amie kumteteya

Pasi khofu wala shaka
Adui akamshika
Na maneno katamka
Msihaya kamwambiya

Kamwambiya huna haya
Bure wayatenda haya
Utaikuta hizaya
Mbele ya Mola jaliya

Adui likazunguka
Mtoto akamshika
Husaini akimtaka
Kijana kumuusiya

Huku mepiga pambaja
Na adui huko waja
Na huku akiwapiga
Mpaka mwisho kufikiya

Yakamzidi machungu
Akamsabihi Mungu
Akaaga Ulimwengu
Mjukuu wa Nabiya

Ghafula akijiliwa
Roho yake ikatwawa
Adui lake Moliwa
Imamu akamwendeya

Akamwendeya kwa dhati
Akamendesha mauti
Jiadui afiriti
Dharuba kumwemezeya

Alipokufa Husaini
Yalitimu thelathini
Na tatu yaliyo ndani
Mafumu yalowingiya

Kuna tena thelathini
Na nne mwake mwilini
Panga za hao wahuni
Mwilini zimesaliya

Mbali mengi majaraha
Kuyataja ni karaha
Moyo hauna furaha
Kwa Imamu kujifiya

Ndio huo mwisho wake
Hiki ndicho kisa chake
Cha Imamu tusichoke
Milele kujisomeya

Walipokwisha saini
Adui wakabaini
Sasa hii ni yakini
Ushindi umewajiya

Wakendewa majohari
Mabanati wa Amiri
Matekani wakaswiri
Huku wakiwachezeya

Pasi haya za uso
Wakaona ni kifani
Kuwatia taabani
Jamaa zake Nabiya

Wakazidisha jeuri
Wala pasipo na siri
Na kichwa chake Amiri
Fumoni wakakitiya

Huku wakikichezeya
Na huku wakiimbiya
Pasi imani kuwaingia
Wote wamefurahiya

Njiani walikipita
Nyoyo zao mezipata
Zimekwisha jaa vita
Shetwani amewaingiya

Alipopata habari
Kwa ambayo yamejiri
Yazidi akaamuri
Ili kwehwa kumwiliya

Furahani vibaraka
Haraka kukipeleka
Kwa Yazidi kikafika
Meyowe kufurahiya

Akawa akichezeya
Na vijiti kukitiya
Huku akimbiliya
Chini kukiumbiriya

Aso haya wala dini
Yazidi akatamani
Uchunguwe wa moyoni
Utatowa kwa duniya

Na huku akikigota
Meno akiyaambata
Uovu na usalata
Hakuna alodhaniya

Ajabu hii ajabu
Kwa kijanache swahibu
Kumfikiya ikabu
Wala pasipo hatiya

Muili ukiwa mbali
Kijana cha Murisali
Wakawachiwa mahuli
Na nyama kukitezeya

Basi haya ni mauti
Walotenda asherati
Lakini kwao laiti
Milele wamejutiya

Walitenda pasi haya
Dini kutotegemeya
Ya Mola kuyachezeya
Pasi nyuma kurejeya

Yapasa tuyalilie
Mauti yake Husaini
Islamu natulie
Kwa kifo chake Husaini

Hapa napenda kukoma
Hadithie kuisoma
Bali mengi sikusema
Dhiki nikiisikiya

Kisomoni waungwana
Majumbani na vijana
Mpate jua maana
Mambo yaliyotukiya

Yatupasa Isilamu
Machozi hadi ya damu
Kumliliya Imamu
Kwetu imetupasiya

Rabi atamtukuza
Peponi kum-bakiza
Kuzidi akimjaza
Neema kumshushiya

Hapa naweka kalamu
Nimefikiya makamu
Wala mbele siyo tamu
Hapa nitakomeleya