Mwanamke Mshirika Katika Maisha
Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:
“Enyi watu! Hakika tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekufanyeni mataifa na makabila (mbali mbali) ili mjuane. Hakika ahishimiwaye zaidi miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi..” (49:13)
Je, dini zimemdhulumu mwanamke? Wako wasemao hivyo lakini kabla ya kujibu swali hili, kwanza ni lazima tufafanue mambo mawili:
Lazima tutofautishe kati ya dini zingine na dini ya Kiislam, kwa sababu katika dini zingine mwanamke huenda akawa na picha mbaya. Nami sina shaka kwamba dini iliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu haiwezi kumdhulumu mwanamke au kumvunjia heshima.
Ama katika dini ya Kiislam, mwanamke ana heshima, na anatukuzwa zaidi ya mwanamume.
Ni lazima tutofautishe kati ya mafunzo ya dini kwa mwanadamu na wanaadamu wenyewe wanaoifuata hiyo dini, kwani huenda ikawa hao wanaofuata dini wanamdhulumu mwanamke katika nyanja fulani, lakini hatuwezi kusema hivyo ndivyo dini inavyotaka, kwa sababu dini yenyewe haitaki uonevu, uwe umefanyiwa mwanamume au mwanamke au hata wanyama na mimea. Kwa hivyo, mimi ninapozungumzia haki za mwanamke, sizungumzii msimamo wa wafuasi wa dini, bali nazungumzia msimamo wa dini, basi nasema hivi; dini haiwezekani imdhulumu mwanamke, kwa sababu ndogo tu, nayo ni kwamba dini ni orodha ya maisha iliyoletwa na mwenyewe aliyeumba hayo maisha. Na ikiwa Mwenyezi Mungu alimuumba mwanamke ili amtukuze, basi amemuumba ili amrehemu, ili amuingize peponi, kama alivyomuumba mwanamume kwa hayo; kwa hivyo haiwezekani amdhulumu, kwa sababu huyo mwanamke hakuchagua awe mwanamke au mwanamume.
Mwanamke huzaliwa mke, hana hiyari, na mwanamume pia huzaliwa mume pasi na hiyari. Vipi tena dini imhukumu mwanamke kwa jambo ambalo hakulichagua yeye mwenyewe (la kuwa mwanamke)?
Kwa hakika dini ya Kiislamu yapinga vikali kila aina ya ubaguzi wa jinsi ya mtu alivyozaliwa bila ya kujiamulia mwenyewe. Mathalan ubaguzi wa rangi (mtu hakukhiyari awe mweupe au mweusi), ubaguzi wa lugha, n.k. Dini haibagui mweusi wa Afrika wala mweupe wa Ulaya, wala haibagui kati ya anayezungumza lugha ya Kiingereza au Kijerumani au lugha nyengine. Wala haibagui aliyezaliwa nchi fulani au nyengine, kwa sababu kuchagua rangi, jamii au nchi anayozaliwa mtu hakuko chini ya uwezo wa mtu huyo. Aidha dini haibagui kati ya mume na mke kwa sababu kuchagua jinsi ya kuwa mume au mke hakuko kwenye uwezo wa mwanadamu.
Ama kuhusu kutenda mema dini haibagui katu, hapa yafafanua:
“...Hakika sitapoteza amali ya mtendaji mema miongoni mwenu awe mwanamume au mwanamke.” (3:195)
Aya nyengine yafafanua:
“Na watakaofanya mema wakiwa wanaume au wanawake hali wao ni wenye kuamini basi hao wataingia peponi.” (4:124)
Vilevile dini yakwambia kwamba, uwezo wa mtu kujichagulia awe mume au mke uko kwa Mwenyezi Mungu.
“Yeye ameumba namna mbili mume na mke.” (53:45)
Na yamkemea vikali anayebagua kati ya mume na mke:
“Na mmoja katika wao anapopewa khabari ya (kuzaliwa kwake) mtoto wa kike uso wake huwa mweusi akajaa sikitiko. Akawa anajificha watu (wasimuone) kwa sababu ya khabari ile mbaya aliyoambiwa! (anawaza) Je! akae naye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni (kaburini akiwa hai)? Sikilizeni! Ni mbaya mno hukumu yao hiyo.” (16:58-59)
(Mambo haya yalikuwa yakifanywa wakati wa ujahiliyya kabla ya Uislamu).
Hii ndiyo picha jumla ya mtazamo wa dini juu ya mwanamke. Na sasa hebu tuangalie kwa ufafanuzi dini isemavyo:
Tukiuliza dini, je! una maoni gani au kwa maelezo ya ndani zaidi, nini mtazamo wako juu ya mwanamke? Tunaiona hapa dini ikijibu: Mwanamke yu hali tatu:
Mwanamke anapokuwa mdogo na msimamo wa baba yake kwake.
Mwanamke anapo olewa na msimamo wa mumewe kwake.
Mwanamke anapokuwa mama na msimamo wa wanawe kwake.
Katika hali ya kwanza (anapokuwa mdogo) twaona kwamba Uislamu wamwambia babake kupitia kwa Mtume (saww) akisema: “Mtoto wa kike ni rehma na wa kiume ni neema.” Mtume (saww) pia amesema: “Kumbusu binti yako ni jambo jema.” Amesema pia: “Bora ya watoto wenu ni mabinti.” Amesema pia: “Bora ya watoto ni mabinti wenye kujisitiri.”
Imepokewa Hadith nyingine kwamba: Mtume (saww) alipopewa bishara ya kuzaliwa mtoto wa kike, aliwa angalia maswahaba nyusoni akawaona wamechukizwa, akawaambia: “Mna nini nyinyi? Hilo ni ua la rehani ninalolinusa na aliloniruzuku Mwenyezi Mungu.”
Vile vile twaona katika maisha ya Mtume (saww) kwamba yeye hajawahi kubusu mkono wowote ila mikono ya watu wawili tu:
Mkono wa bintiye Fatima Zahra alipokuwa na miaka tisa, ilikuwa kila aingiapo kwa babake, alikuwa akisimamiwa na babake (Mtume (saww)) kumbusu mkono wake na akimketisha mahali pake; na hilo alilifanya hasa kwa ajili ya kuwazoezesha na kuwafundisha umma wake.
Mkono wa mchapa kazi, aliyekwenda kwa Mtume (saww) akampa mkono, Mtume (saww) akahisi usugu wa mkono wa mtu yule, akamuuliza, “Mbona hivi?” Yule mtu akajibu: “Huu usugu ni kwa sababu ya kuchapa kazi ee Mtume wa Mwenyezi Mungu.”
Mtume (saww) akainama, akambusu mkono wake huo akasema: “Huu ndiyo mkono unaopendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake!”
Vilevile unahimiza baba anaponunua zawadi za watoto wake, mtoto wa kike apate mbili na wakiume apate moja. Au binti atangulie kupata kabla ya mvulana.
Imepokewa Hadith kutoka kwa Ibni Abbas; Mtume (saww) amesema: “Atakayekwenda sokoni na kununua zawadi akenda nayo kwa familia yake (nyumbani) huyo ni kama aliyechukua sadaka na kuwapelekea wahitaji, basi na aanze kwa kuwapa watoto wa kike kabla ya watoto wa kiume, kwani atakayemfurahisha binti yake ni kama aliyemwacha huru mmoja miongoni mwa wana wa Ismail (a.s). Na mwenye kumfurahisha mtoto wa kiume, mtu huyo ni kama anayelia kwa kumcha Mwenyezi Mungu.”
Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba watu wengi humtanguliza mtoto wa kiume kuliko mtoto wa kike katika maneno na vitendo vinavyohusu mambo yote ya nyumbani. Mtu humnunulia mtoto wake wa kiume akamwacha wa kike au anaposhauri, kuhusu mambo ya ndani ya nyumbani kwake humshauri mtoto wake wa kiume na asimshauri wa kike.
Wazazi wengi wanawapa kipaumbele watoto wa kiume na kuwashughulikia sana kuliko watoto wa kike jambo linalowafanya watoto wa kike wajihisi kuwa wanadharauliwa na hilo huwafanya wakawa na chuki. Kufanya hivi, licha ya kuwa haifai kisheria, vilevile huacha athari mbaya kwenye uhusiano wa wavulana na wasichana na hasa pale kila mmoja wao anapokuwa mwenye familia yake mwenyewe. Jambo hilo twaweza kuligundua tunapochunguza zile familia zenye aidha wasichana tu au wavulana pekee; ambapo utaona watoto wataishi wakiwa wameshikamana, ama wanapokuwa chini ya baba yao, ama kila mmoja anapokuwa tayari ana familia yake, kwa sababu watoto hao hawakubaguliwa kijinsiya. Lakini kinyume nao, wale watoto walio onja ubaguzi wa kijinsiya utawaona hawana mshikamano pale wanapofikia kila mtu wakati wa kujitegemea.
Mtume (saww) asema: “Mtu atakayekuwa na mtoto wa kike na hakumdhalilisha wala hakumtanguliza mwanawe wa kiume zaidi ya huyo wa kike, basi Mwenyezi Mungu atamwingiza peponi.”
Ama hali ya pili: Mwanamke anapokuwa mke wa mtu (rejea nyuma kidogo ili kufahamu zaidi) tutaona kwamba dini ya Kiislamu yamwambia mumewe hivi: “Mcheni Mwenyezi Mungu juu ya wanawake kwani wao ni amana iliyoko kati ya mikono yenu, mmewachukua wao kuwa ni amana ya Mwenyezi Mungu, basi waoneeni huruma na zifurahisheni nyoyo zao mpaka wasimame pamoja nanyi.” Mtume Muhammad (saww).
Vile vile amesema (saww): “Mbora wenu, ni yule aliye mbora kwa mke wake, nami ni mbora kwa wake zangu.”
Anaendelea kusema Mtume (saww): “Mja hatazidi kuwa na imani ila atazidi pia na kuwapenda wanawake.”
Katika Hadith nyengine nyingi asema:
“Mtu atakayemuoa mwanamke basi na amheshimu.”
“Dunia ni starehe, na bora ya starehe za dunia ni mke mwema.”
“Mambo matatu mtu akiyapata amefaulu: mke mtiifu, nyumba yenye nafasi na mnyama mwenye kasi.”
Katika Hadith nyingine! “Jibril hakuwacha kuniusia kuhusu wanawake mpaka nikadhani itakuwa haram kuwaacha.”
Imam Ali (k.w.) naye asema: “Ama haki za mkeo, ni wewe ujue ya kwamba Mwenyezi Mungu amemjaalia kuwa ni kitulizo na liwazo kwako, na ujue hiyo ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwako.”