Kupanga Uzazi… Kwa Nini?
Mnamo mwaka 1965 huko Bombay, India, kulianzishwa shirikisho la kimataifa la kupanga uzazi (Family Planning), ambalo baadhi ya nchi za kiislamu zilijiunga. Sababu walizozitoa za kuanzishwa kwa shirikisho hilo ni kama ifuatayo.
Tatizo la makazi:
Ongezelo kubwa la watu duniani kila mwaka halilingani na uzalishaji mdogo wa chakula duniani, kwa hivyo ni lazima kupunguza ongezeko hilo ili kujiepusha na njaa.
Umuhimu wa malezi ya watoto:
Familia inayoweza kulea watoto watano mathalan katika hali ya kawaida, itaweza kulea watoto wawili kwa vizuri zaidi.
Kuinua hali ya maisha:
Familia yenye kipato cha chini haiwezi kukidhi mahitaji ya lazima kwa idadi kubwa ya watu iliyonayo.
Kumkomboa mwanamke kutokana na majukumu ya ulezi katika kupanga uzazi kuna uhusiano mkubwa baina ya mwanamke kuzaa sana kukombolewa kwa sababu mke mwenye mtoto mmoja anaepukika na ulezi wa mtoto kwa zaidi ya miaka mitano, hivyo anakuwa amepumzika na majukuma yake.
Hizi ndizo sababu kuu wanazozitoa hao wanaopigania na kusimama upangaji uzazi. Nasi tunajibu hapa kwa ufafanuzi:
Kuhusu tatizo la ongezeko la wakaazi, hilo halipo ila kwao hao wanaodai hivyo, dunia, kama tujuavyo, ina uwezo wa kuzalisha chakula maradufu ya mahitaji ya wakaazi wake; kwa hiyo hakuna hoja ya kwamba ni dharura kupigana vita kumaliza watu kwa ajili ya maisha yao!
Kuhusu malezi ya watoto, haya ni madai ya fitna tu kwani malezi ya watoto hayana uhusiano wowote na kuzaa watoto wengi au wachache kwani familia ikiwa nzuri inaweza kulea idadi yoyote ya watoto, na ikiwa mbaya haiwezi kulea hata mtoto mmoja. Isitoshe, kukata kizazi ni kosa kubwa kwa jamii ya watu, kwani inawezekana, pengine yule mtoto, aliyezuiliwa na mamake asijaliwe, angelikuwa mtu mkubwa sana katika jamii kama angeachiliwa aishi. Angalia, lau Abu Talib, babaye Ali bin Abi Talib angefunga kizazi chake baada ya kuzaliwa Aqil (kakake Ali) je! ni kosa kubwa kiasi gani angeliifanyia jamii ya watu.
Ama kuhusu kuinua hali ya maisha, inaweza kuwa hoja sahihi kama watu kuangalia kwa makini na kwamba mikutano ya kimataifa iweze baada ya kulipa umuhimu suala la ‘kupanga uzazi’ wangelipa kipaumbele suala la kuongeza makao ili yalingane na jinsi watu wanavyoongezeka.
Na kuhusu suala la kuhusisha upangaji wa uzazi na ‘kumkomboa’ mwanamke ni kweli lakini nani kasema kwamba inapasa mwanamke ajikomboe na majukumu na wajibu wake? Kuzaa kwa mpango si jambo lililo chini ya uwezo wa mwanamke tu, bali ni jambo lilio chini ya uwezo wa jamii, na jaribio lolote la kuzuia wasizaliwe watu wema kwa jamii ni kwenda kinyume na ubinaadamu wote ambapo huko kumkomboa mwanamke kwa maneno mengine, tayari anakombolewa kwa kuwaweka vifaa ili kumrahisishia kazi.
Hizi ndio sababu wanazozitoa, (tulizozijua) kwa ajili ya kupanga uzazi. Na maadam sababu hizi hazina hoja ya nguvu, basi nasi ni haki yetu kuuliza swali hili: hawa wanaofanya kampeni ya kupanga uzazi wanakusudia nini? Je! kweli wanataka mwanamke aende kulingana na ratiba iliyopangwa ya malezi mazuri zaidi ili aweze kutoa huduma nzuri zaidi?
Mmoja kati ya viongozi wao, katika nchi moja ya Kiarabu anajibu “kwa hakika kazi ya kufanya kampeni ya upangaji uzazi lengo lake kubwa ni kuondoa desturi walizonazo watu; na ili tuweze kufanya kazi hii barabara ni lazima tuondoe zile fikra zinazokwamisha mpango huu.”
Lakini bwana huyu hayaweki wazi maneno yake juu ya hizo anazoziita ‘fikra’; hizo ni fikra za kiislamu, na desturi hizo ni yale maadili na tabia za familia za kiislamu.
Ama njia ya kuziondoa ni kujaribu kutia shaka ndani ya Uislamu na kuileta misingi ya mambo kimaada (kidunia), ya kilahidi badala ya maadili ya kiislamu. Jambo la kushangaza ni kwamba wale wanaoshadidia mambo ya kupanga uzazi hawaoni umuhimu wowote wa kuenea ukahaba, kama ambavyo zile nchi zinazokampenia upangaji uzazi hazijaribu hata mara moja kuzuia ukahaba.
Je, Nini Maoni Ya Uislamu Katika Kupanga Uzazi?
Bila shaka Uislamu haukubali kupanga uzazi kwa ‘mwito’ wowote ule. Kuna wale wanaopotosha hadith ya Mtume (saww) isemayo: “Oaneni, mzaane ili mpate kuwa wengi, kwani mimi nitajifaharisha kwa watu wa umma zingine siku ya kiyama hata kwa mimba iliyoharibika.” Watu hawa wanadai kuwa makusudio ya Mtume (saww) kusema ‘mpate kuwa wengi’ siyo wengi wa idadi bali wa aina fulani. Ndiyo, ni kweli Uislamu unataka kupanga, lakini nani aliyesema Uislamu unataka kupunguza kwa mpango, na si kuongeza lakini kimpango?
Ama ile hadith ya Mtume (saww) makusudio yake si ‘aina’ (kama wanavyodai) itakuwa na uhusiano gani basi juu ya kujifaharisha Mtume (saww) na aliposema mpate kuwa wengi na aliposema hata mimba iliyoharibika?
Kuhusu suala la ongezeko la wakaazi, Uislamu umekuja na masuluhisho ya aina mbili:
Ufafanuzi wa ki-ujumla
Ufumbuzi maalum wa hali halisi
Kabla hatujafafanua juu ya ufumbuzi wa kwanza ni lazima tukubali kwamba Uislamu umeruhusu baadhi ya familia kupanga uzazi.
Katika maoni ya Uislamu, Mwenyezi Mungu ameumba ardhi kulingana na wanadamu walivyo na daima kuna uhusiano baina ya mwili wa ardhi na mwili wa binaadamu kiasi kwamba haijatokea na wala haitatokea siku ambayo ardhi haitamtosha mwanadamu vilevile, mazao ya dunia daima yanazidi mahitaji ya mwanadamu hata kama watazaana kwa wingi. Qur’an inasema:
“Na Mwenyezi Mungu amekuumbieni wake kwa jinsi yenu, na akakujaalieni kutoka kwa wake zenu watoto na wajukuu, na akakuruzukuni vitu vizuri vizuri. Basi je, wanaamini yasiyokuwa ya haki na kuzikataa neema za Mwenyezi Mungu?” (16:72)
Neema za ardhi hazitakuwa chache kuliko mahitaji ya binaadamu isipokuwa ugawaji mbaya na mpango mbaya wa miji kisiasa ndiyo mambo yaliyosababisha ugumu wa maisha ya baadhi ya watu. Kuna baadhi ya nchi tajiri zenye ardhi zenye rutuba, madini na utajiri wa mali asili, na hali watu wake wanaishi maisha ya dhiki na mfumko mkubwa wa bei.
Pia kuna nchi zingine maskini zenye ardhi kame zinapatana na nchi tajiri lakini watu wake wanataabika na ukosefu wa chakula, njaa na vifo.
Ufumbuzi wake ni mdogo tu, zile nchi tajiri zifunguwe milango yake kwa nchi masikini na mipaka ya kisiasa iondolewe na mashirikisho ya kimataifa yasimamie chakula, hilo litafanya watu wote waishi kwenye ardhi moja wakistarehe na kuneemeka.
Nani aliyesema Amerika lazima kila mwaka iteketeze tani chungu nzima za ngano ya zaidi; ambapo kuna watu duniani kiasi cha milioni moja wanaokufa kwa njaa na ukata?
Nani aliyesema mataifa dunia yatumie milioni ya mapesa katika mashindano ya kujilimbikizia silaha bila ya kujua hatima yake, na hali kuna watu wanashindwa kupata mkate na tone la maji.
Takwimu za uchumi wa kijeshi na mashindano ya silaha duniani zinaonyesha kwamba gharama za matumizi ya kijeshi duniani zinazidi, kwa kiwango kikubwa, kuliko gharama za maisha katika sekta za kiafya, kielimu, chakula na kijamii. Tarakimu hizo zinafafanua kwamba matumizi ya kijeshi duniani katika mwaka 1966 na 1967 yalifikia dola milioni mia moja na themanini na mbili ($182) kila mwaka, na kwamba kiwango hiki kitapanda hadi kufikia dola milioni mia nne na tisini na tisa ($499) kabla ya kufikia mwaka 1977.
Na kulingana na tarakimu za shirika la UNESCO, Gemini News Service, England, matumizi ya kijeshi ya dunia yanazidi matunzo ya kielimu dunia kwa wastani wa asilimia arubaini (40%).
Miongoni mwa mambo yaliyofichuliwa na UNESCO ni kama ifuatayo:
Gharama za kumsomesha shuleni mtoto mmoja kwa mwaka hazizidi dola mia moja ($100) ambapo gharama zinazotumika kwa mwanajeshi mmoja tu praiveti zinafika dola elfu saba na mia nane ($7800).
Msaada (huo) anaotoa mtu katika nchi tajiri kuzipatia nchi masikini hauzidi hata dola nane ($8), ambapo kwa wastani anagharamika zaidi ya dola mia moja na sabiini ($170) kwa matumizi ya kijeshi!
Misaada ya kijeshi inayopokea nchi maskini kutoka nchi tajiri imeongezeka.
Hii ni kuongezea kwamba bado kuna utajiri mwingi sana wa mali asili ambazo haujavumbuliwa au haujatumika, utajiri ambao wataalamu wanakisia kwamba utakapogunduliwa utaweza kumuongezea mahitaji zaidi ishirini elfu ya wakaazi duniani kwa kila wanachokihitaji.
Hebu tuangalie utajiri ulioko baharini:
Kadri idadi ya watu inavyoongezeka duniani ndiyo matumizi ya nchi asili yanavyozidi kuongezeka kwa kasi na kwa wingi mno na watu wanaelekea zaidi baharini ambamo mna hazina kubwa sana ambayo bado haijatumika. Hivi sasa zaidi ya tani milioni hamsini za samaki huvuliwa kila mwaka na hiyo ni sehemu ndogo tu kama tone la utajiri ulioko baharini ambao kwa ujumla unaweza kufikia tani bilioni ishirini, mbali na mimea ipatikanayo baharini. Bidhaa zinazopatikana baharini zikitumiwa vizuri unaweza kuondoa tatizo la ukosefu wa Vitamin, Protini na mafuta katika chakula cha binaadamu.
Isitoshe, baharini mna hazina isiyokwisha ya madini mbalimbali wachilia mbali hazina za meli na majahazi yaliyozama ambazo ni kidogo sana kulinganisha na hazina zilizomo humo.
Chini ya bahari kunapatikana mabilioni ya tani za chuma na manganese, Nickel (madini kama fedha), shaba na madini nyingi mbalimbali. Uvumbuzi wa hivi karibuni umeonyesha kwamba kuna hazina ya kutosha ya mafuta baharini, na dhahabu iliyomo chini ya bahari ikiwa itagawanywa itatosheleza kila mtu duniani kupata tani tatu.
Isitoshe, maji ya bahari yanaweza kuzalisha umeme katika siku zijazo.
Ikiwa utajiri wa dunia ni mkubwa kiasi hiki kwa nini basi kuwe na kutaka kukata kizazi? Uislamu unaposema ‘la’ hakuna kupanga uzazi hautegemei hoja tasa, bali ukweli ulivyo kwa dunia na watu wenyewe.
Ah! Mangapi mazuri yatapatikana lau Uislamu utarudi?
Kuna mamia ya watu wanaokufa njaa nchini ya kivuli cha ulahidi. Mamia wengine wananyimwa kibali cha kuingia kwenye maisha kwa ajili ya kile wanachokiita ‘kupanga uzazi.’
Lakini, kwa sababu Uislamu hauamini kama wanavyoamini watu wa ki-maada wa kisasa kwamba, mwanadamu ni manyasi ya jangwani anayetoka tumboni kwa mama yake, si muhimu, awe na njaa, kiu, au hata afe..!
Kwa matazamo ya Uislamu, mwanadamu ana heshima yake maalum; kubwa zaidi ya heshima ya dunia, hata kilenge kilicho tumboni kina heshima yake. Kwa hivyo utaratibu wa kiislamu umetosheleza kila mtu maisha mazuri vyovyote itakavyokuwa.
Uislamu, kwa kiasi kikubwa, unafanya juhudi kumuandalia kila mtu shughuli njema ili aweze kuitosheleza familia yake, na asipopata kazi basi mtu aliye karibu naye amsaidie kimaisha, si kwa huruma na hisani, la, bali ni wajibu uliofaradhiwa na Uislamu.
Na kukiwa na familia maskini isiyo na uwezo na haina jamaa zakusaidia basi dola ya kiislamu ndiyo itakayowasimamia mahitaji yao ya kimalezi, kiafya na kijamii.
Maadam Uislamu hautambui mipaka ya kikoloni baina ya dola za kiislamu, au hata mipaka ya duniani, na maadam mwanadamu kwa mtazamo wa kiislamu ni ‘mwanadamu’ basi nchi haziwezi kuwa na matatizo kwa wingi wa makazi. Hebu tupige mfano, mathalan nchi ya Misri imezidiwa na watu kisha nchi ishindwe kuwatosheleza mahitaji ya lazima ya watu wake, hakuna tatizo, wafungulieni wamisri mipaka ya Sudan ambayo ina ardhi kubwa na hali nzuri ya hewa kisha muwagawanyie pesa za mafuta za Libya kisha muwaache wajiendeleze…!
Hii ni kwa upande wa kutatua matatizo ya kiislamu ki-ujumla.
Ama kuhusu kutatua matatizo yaliyopo hivi sasa, kile kinachotoa Uislamu ni rahisi kupatikana. Ardhi ya Kiislamu kama tujuavyo si ndogo bali ni kubwa na masafa yake yanatosha kwa kuishi na kuwaajiri watu wote duniani, isitoshe, ardhi hiyo si maskini kwa sababu ina madini, maji na rutuba. Mwenyezi Mungu ameumba petroli sehemu nyingine na nchi nyingine hakuweka, vilevile kwingine ameweka mito na kwingine hakuweka; naye alipoumba hivi hakuweka mipaka bali alimwambia ‘hii ardhi ni kwa ajili yenu, shikaneni na muishi kwa amani’ bali watu ndio walioweka mipaka, umma mmoja wakaufanya ziwe ishirini, na taifa moja wameligawanya kwenye mataifa ishirini.
Nasi si wajinga kiasi kwamba tupendekeze ufumbuzi wa tatizo la wingi wa watu kwa njia ya kuondoa mipaka ghafla katika nchi za kiislamu, kwa sababu zoezi hilo si rahisi hivi sasa, kama si muhali. Lakini pia sisi si wajinga kiasi kwamba tuamini kwamba haiwezekani kukusanya pesa za Kiislamu zinazotumika mahotelini kwa ufuska kwa ajili ya kufungua viwanda vikubwa ambavyo vitawaajiri mamilioni ya watu kwenye mji wa Kiislamu wanaotafuta chochote na hawakipati!
Kwa hivyo basi sisi tunapinga ‘kupanga kizazi’ kwa maana ya kuzuia watu wazaane kwa sababu hizo, upingaji huu unaukosea umma wa kiislamu ambao unabeba majukumu mazito ya ulimwengu, ya kuutoa kwenye udhalili na kuweka kwenye uadilifu, uhuru na amani, na kisha kumtoa mwanadamu kumpeleka kwenye anga ambao hajaijua upeo wake, na hatuamini kama watu milioni mia nane wanatosha kutekeleza majukumu haya.
Jambo la kushangaza ni kwamba propaganda za ‘upangaji uzazi’ zinaongezeka upande wa mashariki ya nchi za kiislamu kila kunapokuwa na mapambano kati ya nguvu za kikoloni, kilahidi na waislamu, na hasa wanapohisi kuwa nguvu hizo zinashindwa kutokana nguvu za waislamu.
Na jambo jingine la kushangaza; utafiti juu ya ongezeko la wakazi katika nchi za kiislamu kwanza huonekana kwenye magazeti ya kikoloni nchi za mashariki na magharibi kisha unaonekana katika magazeti ya nchi za kiislamuna watu wakavalia ujinga?
Lakini msisahau kwamba Ulaya mashariki na ulimwengu wa kiyahudi wanafanya juhudi kubwa ya kuongeza uzazi badala ya kupanga!