read

Masuala Ya Upande Wa Kike

Baadhi ya watu hujiuliza kuhusu Hijab, kwa nini dini ikawajibisha? Wengine huuliza: Je, inafaa mwanamke afanye biashara, au ukulima?

Wengine wanataka kujua, je! mahari ni thamani (bei) ya mwanamke? Na wengine wanauliza kama inafaa mwanamke mmoja aolewe na waume wengi!

Ama kuhusu Hijab, kwa hakika mtazamo wa dini kwa mwanamke ni mtazamo wa kijumla, yaani ujumla mwanamke ni binaadamu na siyo wa kuji­starehesha naye tu.

Kwa hivyo inatubidi tumuangalie ki-upande huo, lakini kwa kuwa yeye ni kivutio kwa sababu ana maumbile mazuri ya kike yanayomvutia mwana­mume, ndipo dini ikafaradhisha Hijab ili kuzuia mwanamke asigeuzwe njia ya kujistarehesha, na hai­fai tumtazame mwanamke kama bidhaa ya kuuzwa au chombo cha starehe kama yanavyofanya maendeleo ya ki-magharibi ambayo yamemvua ubi­nadamu wake na kumbakishia uanamke wake ndipo akafanywa ni kitu cha matangazo ya biashara ili kumvutia mteja. Mwanamke anatumika kwenye biashara kiasi kwamba wanapotaka kuuza gari hum­si­ma­misha msichana mzuri kando ya gari hilo wa­kampiga picha nalo ili lipate kuuzwa.

Isitoshe hata wanapotaka kuuza farasi maalum, wa­tamsi­mamisha msichana mrembo kando ya ran­chi ya farasi ili awavutie wanunuzi wamnunue farasi huyo. Hata kwenye matangazo ya bustani ya kufugwa wanyama mwanamke amekuwa aki­tu­mika! Hivi ndivyo mwanamke anavyotumika kwa faida ya kibinadamu naye huhitajiwa tu pale anapo­kuwa mrembo wa kumezewa mate; ama akiwa mbaya au ameumbwa na uzuri wa kawaida tu, huwa hana thamani kwa sababu huyo hawezi ku­vutia wanaume.

Ama Uislamu haukubali mwanamke atupwe kwenye matamanio, kama alivyosema Imam Ali: “Mwanamke ni rehani na si mtumishi.” Mre­hani lazima uhifadhiwe. Na mwanamke ni almasi lazima athaminiwe. Tunaposema almasi lazima ifichwe ili isiibiwe, je! huko utasema ni kuivunjia heshima almasi au kuichunga? Basi vivyo hivyo mwanamke na Hijab!

Hapana. Hijab si kumtweza mwanamke bali ni kum­chunga kutokana na wizi wa ngono. Na maadam mwanamke anatakiwa na mwanamume kwa mata­manio basi yampasa ajihifadhi maumbile yake ya kike kwa njia ifaayo, nayo ni kuficha vivutio vyake. Mwanamke mzuri ni yule anayejistiri mwili wake na waume wengine na kujionyesha kwa mumewe tu. Mtume (saww) asema: “Bora ya wanawake zenu ni yule mzazi, mwenye mapenzi, mwenye kujisitiri, mwenye kumtii mumewe, mwenye kujichunga na mwengine, anayemsikiza na kumtii amri zake na wanapokuwa faragha, humpa akitakacho.”

Amesema pia: “Mbora wa wanawake wenu ni yule anapokuwa faragha na mumewe huvua vazi la kuona haya.”

Ama kuhusu wanaume ambao hawamtaki ila kwa ajili ya kufaidi tu, Uislamu umemzuia na hilo. Kwa sababu kijana anayemchukulia msichana kama mpita njia tu kwa ukweli huwa hana haja naye ila hutaka kutimiza haja za matamanio yake tu wala hana penzi. Kwa hivyo anachotaka ni kukidhi haja zake tu wala hajali mabaya wala mazuri ya mwanamke huyo.

Mara ngapi tumeona matukio kadha wa kadha katika nchi mbalimbali ambapo msichana amechukuliwa na kijana akatembea naye kisha akamwacha abebe mateso yake.

Kuhusu kufanya kazi, Uislamu haumkatazi mwanamke kufanya kazi yoyote. Uislamu hausemi kwamba ni haramu kwa mwamanke awe mfanyi kazi au mkulima au mfanyi biashara, bali ni haki ya mwanamke afanye kama afanyavyo mwanamume katika kufanya kazi, kulima, biashara n.k. kwa sharti tu awe na “heshima” na kuulinda utu wake.

Uislamu unakataza kwenda tupu na mwanamke ku­jionyesha sehemu za mwili wake, haukatazi kufanya kazi.

Sote tunajua ya kwamba Bi Khadija bint Khuwailid (r.a.) alikuwa tajiri na mfanyi biashara mkubwa na ali­juana na Mtume (saww) kupitia biashara zake ambapo Mtume (saww) alikuwa akifanya kazi kwake.

Mwanamke anaweza kufanya kazi ikiwa atahifadhi Hijab yake kazini, au asichanganyike na wanaume wawezao kumuoa. Kwa sababu bila ya kufanya hivyo atageuka kuwa ni burudani kwa wanaume.

Ama kuhusu mahari, kwa mtazamo wa uislamu, ni alama ya kuonyesha kuwa msichana huyu anata­kiwa na mvulana huyu. Hutolewa mahari ili mwanamke ajihisi kuwa anahitajiwa na mwana­mume na si yeye anayemtaka mume, jambo linalo mtosheleza haya zake alizoumbwa nazo na heshima zake ambazo bila shaka zitavunjika pale yeye ataka­pom­taka mwanamume.

Mahari si thamani ya bei anayolipa mume kuununua mwili wa mwanamke, na ndipo ukaona uislamu haukupanga kiwango cha mahari na kitu chochote chaweza kuwa mahari (k.v. vyombo n.k.) hata kumfundisha hesabu au sura ya Qur’an kunaweza kuwa mahari, au chochote hata kiwe ki­dogo namna gani.

Isitoshe, uislamu unapenda mahari yawe kidogo. Mtume (saww) anasema: “Bora ya wanawake wa umma wangu ni wale wazuri wa uso wenye kutolewa mahari kidogo.” Na kila mahari yanapokuwa kidogo, inaamanisha kwamba huyo msichana (kwani ndiye anayetaja mahari) anamtaka huyo mume mwenyewe na si mali yake, na huyo mume anamtaka mke mwenyewe si kwa sababu amemnunua.

Kuhusu suala la mke na waume wengi, dini imekataza hilo kwa sababu hizi:

Mwanamke hafai kushea ikiwa wewe hufai ku­shea hata kalamu yako, utaridhika kushirikana mkeo?

Suala la kuona ni utangulizi wa kupata watoto, na kuwa na waume wengi ni kuchanganya watoto.

Mwanamke ana hisia za ‘ulinzi’ yeye vyoyote ilivyo anatafuta mtu wa kumlinda. Hebu uliza nchi gani inayotawaliwa na maraisi wawili? Au dola gani ya ndoa inayotawaliwa na waume wawili?

Hata upande wa mume kuoa wake wengi uliuhu­siwa na uislamu kwa sababu ya kutatua matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na idadi ya wanawake kuwa kubwa zaidi ya wanaume. Nchini Merekani pekee, kuna wajane milioni tisa waliofiwa na waume zao, na mamilioni ya washichana ambao hawajaolewa.

Vilevile sababu ya kuwa na wake wengi yaweza kuwa ni kwa ajili ya maslahi ya mwanamke kwa mfano; hebu tuchukulie mke ni tasa, hazai na mumewe anataka watoto na kisha mume tumzuie asiwe na wake wawili (asioe), hii ina maana kwamba tutamruhusu amuache yule mkewe ili aoe wa pili. Hii kwa kweli itakuwa si kwa maslahi ya yule mkewe.

Hili ndilo suala la mwanamke, ambaye ana heshima yake katika uislamu, kwa sababu yeye ni kiumbe cha Mungu, na amejaaliwa hivyo na Mungu muumba kwa ajili ya kujuana kama isemavyo Qur’an:

“Enyi watu! Hakika tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekufanyeni mataifa na makabila (mbali mbali) ili mjuane. Hakika ahishimiwaye zaidi miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule am­cha­ye Mungu zaidi..” (49:13)

Ama maendeleo ya kimagharibi (Ulaya) heshima ya mwanamke imevunjwa, amekuwa ni thamani tu ya kibiashara au burudani ya ki-ngono mambo yana­youtweza utu wake na hili sisi hatuliridhii wala hatutaki limpate mwanamke.

Wanamuua mwanamke siyo!

Siku moja Mtume (saw) alikuwa ameketi na baadhi ya maswahaba zake kwenye changarawe akachora kwa kidole chake ardhini mstari ulionyooka, kisha kando ya msitari huo akachora msitari ya mshazari, mmoja upande wa kulia na mmoja wa kushoto, akaashiria kwenye ule msitari wa kwanza ulionyooka akasema: “Hii ni njia ya Mwenyezi Mungu, kisha akaashiria kwenye ile mistari mingine akisema: “Na hizi ni njia zingine ambazo juu ya kila njia pana shetani anayewaita watu waifuate. Kisha akafumba macho kwa muda mfupi kidogo, kisha akasema: “Kwa hakika hii ndiyo njia yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Wala msifuate njia zingine mtafarikiana na njia ya Mwenyezi Mungu.”

Kwa hivyo hapa Mtume ameeleza upotofu wa kila njia isiyolingana na njia ya Mungu kama vile alivyoonyesha jinsi njia ya Mungu inavyojitenga kimsingi na njia za shetani. Sasa basi, tunapotaka kuigundua njia ya Mungu kuhusu masuala ya mwanamke tusiwaulize mashetani, na maana ya mashetani hapa ni wote walioanguka chini ya matamanio. Yatupasa tuangalie kwenye maneno ya Mwenyezi Mungu na Mtume, kwa sababu mapenzi ya nafsi daima hufikiria lile jambo ilitakalo na haya­fikiri ukweli ulivyo.

Mtu akisema ‘Hijab hakuna katika uislamu’ wakati yeye anasoma jinsi Qur’an inavyosema: “…na mnapowauliza kitu basi waulizeni nyuma ya pazia (hijab), mtu huyo hakusudii hijab kama ilivyo kwenye uislamu ila ni kwa kuwa hijab haiku­ridhisha matakwa yake, ya kimwili ndiyo maana akasema hakuna hijab.

Hivyo ndivyo ilivyo, na kwa hakika uislamu ndio unaopanga njia ya Mwenyezi Mungu na si watu wengine, na ndipo hapa tunakuta kwamba Mwenyezi Mungu anaweka orodha ndefu kuhusiana na masuala ya mwanamke:

Maisha ya mwanamke ya kipekee

Masuala ya mwanamke ya kijamii

Masuala ya mwanamke ya kifamilia

Masuala ya mwanamke ya ki-jinsiya

Ufafanuzi wa masuala haya ni kama ifuatavyo:

Kuhusu masuala yamhusuyo ni kwamba yeye anapaswa kutenda yale yapasayo mwanamume kuyatenda kama kufanya ibada, kuwa na tabia nzuri n.k.

Mwanamke ana haki zote za kijamii na anaweza kufanya biashara, kulima na kufanya kazi mradi tu ahifadhi heshima yake ya kike.

Kifamilia, mwanamke ni msimamizi wa utekelezaji ndani ya nyumba ambapo mume anakuwa ni kiongozi wa taasisi ya familia. Aya isemayo: “Wanaume ni wasimamizi wa wanawake” haimaanishi mwanamume atumie mabavu na kulazimisha mambo; Uislamu hau­mu­an­galii mwanamke kama mtumishi au si bandia wa anayefaa atwishwe mizigo ili mwana­mume ajinufaishe.

Mwanamke ni mshirika wa wanaume, si mtumishi kwa hivyo yampasa mume kwa sa­babu mke ni bibi wa familia amuandalie mshirika wake huyo maisha mema ya ki-­binadamu.

Yampasa mke aishi vizuri na mumewe na amtosheleze na starehe za jinsiya inavyotakiwa na kwa ndoa ya kisheria, na uislamu una orodha na miongozo mirefu juu ya suala hili linalo fafanua kwa usawa kwa mume na mke njia za kuonana kimwili1; nayo ni miongozo iliyofafanuliwa inayoeleza hata namna ya kufanya tendo la ndoa na wakati muwafaka wa hilo.

Kwenye orodha hizi zinazohusu masuala ya mwanamke katika uislamu tunagundua kwamba zinamuangalia mwanamke kuwa ni mwanadamu, mwenye haki ya kuishi kwa usawa na mwanamume.

Lakini kuna zingine zisizokuwa za kiislamu ambazo zamuangalia mwanamke kama mwanaserere (kiji­sanamu) wa kujistareheshwa naye tu kamili.

Na kama tulivyoona, ni kwamba Uislamu unafanya juhudi kuona kwamba umedhibiti starehe za kimwili kwenye familia na maisha ya ndoa. Uislamu hauru­husu starehe hizo kutangazwa sokoni, barabarani, mabarazani au kwenye mikusanyiko. Pia hauruhusu kwenda uchi, kujionyesha mapambo, au kuchanga­nyika kiovu kwa wake na waume na kukaa faragha. Hayo yote yanaambatanishwa na adabu, desturi na hukmu maalum.

Hivi ndivyo Uislamu unavyoipa suala la jinsiya la mwanamke picha yake halisi na kuipa umuhimu kama yalivyo masuala mengine; yawe ya kijamii au ya ki­familia. Hivyo ndivyo uzani wa usawa unapohifadhika na kuzuia mwanamke asitumiwe kama chombo cha madhambi au kisanamu cha ku­chezewa.

Ama mifano mingine (isiyo ya Kiislamu) yenye mi­singi na hukmu ambayo inaendelea hivi leo chini ya kivuli cha ‘maendeleo’ (kompyuta na elektroniki) inafanya juhudi za kufanya mwanamke awe ni ‘jinsi nyingine’. Asipotimiza wayatakayo basi hapana haja aweko. Kwa msingi hii haya yote yamepangwa juu ya desturi za mambo hayo, ambapo baadaye hakuna kizuizi kwa mwanamke kuyafuata kama kusam­baratika kwa familia, kuzaa nje ya ndoa, kuenea zi­naa n.k.

Kwa hivyo mwanadamu leo yampasa achague moja kati ya njia mbili. Ama njia ya kujizuia, (maisha ya ki-familia ya ndoa) au njia ya zinaa (kuharibika kwa familia).

Njia ya kwanza ni ya Mungu na ya pili ni ya shetani. Wale wanaochagua njia ya pili, yawapasa wafahamu kwamba jambo haliishi kwa wao kuifuata kando kando (bora wasifuate kabisa). Ama kujaribu ku­changanya baina ya njia mbili hakufai ila ufuate njia ya Mungu tu. Kwa sababu njia ya shetani ni njia ya matamanio nayo hayana mwisho mwema. Kila mwanadamu anapo potea humo, matamanio nayo humwambia; vipi nyongeza!

Suala: Je! yapasa kumpendelea mwanamume zaidi ya mwanamke kiasi cha kumnyima mwanamke haki nyingi za kisiasa na kijamii?

Jibu: Lau kama mwanamke hatofautiana na mwanamume upande wa maumbile yake ya ki­mwili, kiakili na kifikra, hapa suala la kupendelewa lingeingia mahali pake. Lakini kwa kuwa mwanamke kimsingi anatofautiana na mwanamume hapa suala si ‘kupendelewa’ bali suala ni ‘kuhu­sishwa’ na kuweka kila jambo pale panapofaa. Hivi hasa ndivyo inavyoafikiana na maoni na mfumo wa Uislamu. Mwanamke kwenye Uislamu ana nafasi zake maalum, kwa sababu sehemu hizo zahitaji ahu­sishwe nazo yeye hasa.

Mathalan; kama ambavyo si sahihi daktari asomeshe mambo ya uhandisi (uinjinia), au kipofu achukuliwe kuwa muongozaji rada! Basi vile vile si sahihi mwanamke abebeshwe majukumu asiyoweza kuya­beba. Hata sayansi inatuonyesha kimsingi jinsi mwanamke alivyo tofauti na mwanamume.

Dkt. Casius Carel, mshindi wa tuzo la Nobel katika sayansi anasema: “Mambo yanayomtofautisha mwanamume na mwanamke hayaishii kwenye maumbile ya viungo vyao vya uzazi tu, au tofauti katika malezi yao tu, bali kuna mambo mengi. Tofauti hizo zina maumbile ya kimsingi zinazoanzia kwenye mpangilio wa kimwili, mwanamke katika kila kiungo cha mwili wake ana vitu vya maji maji vya kemikali vinavyorutubisha uzao. Wale wanaodai kuwa na malezi sawa, elimu na kazi baina ya wanaume na wanawake hawazijui tofauti hizi kabisa; tofauti za kimsingi. Mwanamke alivyo hasa ana tofauti kubwa na mwanamume kwani kila chembe chembe (cell) katika mwili wake ina umbile la kike, hata mpangilio wa mishipa yake uko tofauti.”

Anaendelea Dkt Carel: “Utaratibu na kazi za viungo vya mwili una mpangilio maalum kama vile elimu ya nyota na hesabu. Haiwezekani kufanya badiliko lolote kwa kuwa tu mwanadamu anataka kubadilisha. Kwa hivyo letu sisi ni kukubali kama ilivyo. Na wanawake nao ni lazima wakuze vipawa vyao kulingana na maumbile yao, na waache kuwaiga wanaume kiholela. Nafasi yao katika maendeleo ni kubwa kuliko ya mwanamume na haifai kuiacha.”2

Maadam majaribio ya kisayansi yameonyesha tofauti hizo za kimaumbile, basi yapasa kutenganisha suala la mwanamume na la mwanamke. Kila mmoja wao apewe wadhifa ule utakaolingana na sifa zake. Mwanamke ana sifa za huruma basi ni lazima kazi ya kulea watoto aachiwe yeye, kwa sababu kazi hiyo inahitajia huruma. Na mwanamume kwa kuwa ana nguvu za kubeba majukumu mazito, basi hapana budi apewe uongozi wa kusimamia nyumba na nchi.

Isitoshe, inapasa ratiba ya masomo ya mwanamke ibadilishwe ili iambatane na tabia, umbile na akili yake.

Vilevile hapana budi majukumu yake katika maisha ibadilishwe ili yalingane na shakhsiya yake ya huruma.

Tutakapomweka mwanamke kwenye nafasi yake ifaayo basi tutaweza kuinua hali ya nchi iliyoporomoka. Kwani kumpa kila mtu nafasi yake anayohusika nayo ndiko kumwezesha kupata fursa kwenye jamii ya kufikia maendeleo.

Jamii ya mwanadamu ina mfumo wa “kutofau­tiana.” Ama jamii ya wanyama ina mfumo wa “kuwa sawa.” “Kutofautiana” ina maana ni kuto­fautiana watu na kila aliye na sifa fulani kumfanyia na kumkamilishia mwingine ambapo “kuwa sawa” maana yake ni kuwa sawa bila ya kushughulikiana. Kwa hivyo hapa, utaona kuwa mwanamume ana­muhitajia sana mwanamke na mwanamke anamu­hitajia sana mwanamume. Lau ingelikuwa mwana­mume na mwanamke “wako sawa”, basi mmoja asingelimu­hitajia mwengine.

Dkt. Maranon anasema: “Jambo linalothibiti ni kwamba, ukamilifu wa mwanadamu utatimia, na lazima utimie, kwa kuziainisha tofauti zao, yaani mwanamume ajione zaidi ni mwanamume, na mwanamke ajione zaidi kuwa ni mwanamke.”3

Kwa hivyo ni upumbavu wanawake wawaige wanaume, na wanaume nao kuwaiga wanawake.

Msichana aliye baleghe hapendezi mbele ya mwanamume pale anapovaa Mini au Kaptula (Short pants) kama vile mwanamume avae gauni, viatu vya mchuchumio (High heels) pochi kwapani na ajitie manukato ya kike ya ki-Faransa!

Takwimu zimeonyesha kwamba wanaume hupendelea sana wanawake wenye kujiheshimu kuliko wenye kujidhihirisha wazi wazi. Ndiyo, ni kweli mvulana mhuni hupata kumchezea msichana anayevaa Mini anapompitia mbele yake barabarani.

Lakini penzi liko mbali na suala la ndoa ya daima, kwani mwanamume katu hawezi kumuoa msichana mwenda-uchi. Anajua wanawe atakaozaa naye wa­taharibika kwa sababu mama atakayewalea ata­penda zaidi kujipamba kwa ajili ya wanaume wen­gine ili awavutie, kuliko kuwalea wanawe.

Na msichana apendaye kuangaliwa na maelfu ya ma­cho yenye njaa naye hajaolewa, basi hata atakapoolewa atapenda zaidi macho ya watu yamuangalie. Haitai­shia hapo, mwisho itafikia kupokea wanaume!

Familia nyingi zimesambaratika kwa sababu mwanamke si mwenye kujistahi. Kwa kweli ni ujinga wa mwisho mwanamke avunje heshima yake kwa sababu tu watu maarufu wa Ujerumani wanafanya hivyo, au vijana wajifanye kama watu washuhuri wa Marekani wafanyavyo.

Suala hapa si maendeleo kama wanavyodai bali suala ni uigaji wa kiholela. Hebu niambie - kwa haki ya Mola wako - maendeleo yako wapi kulea watu wanaofanana na ramani ya Italia?

Maendeleo ya wapi, mvulana anapojitia rangi ya mdomo na kuvaa mikanda ya wacheza sinema wa zamani?

Maendeleo gani wanafunzi wa kike wakutane chooni wapeane tembe za kuzuia mimba?

Maendeleo gani mvulana amuazime dadake nguo ili aende kwenye tafrija fulani, kama ilivyozoeleka hivi sasa Ulaya?

Watu wengi waliteleza wakaporomoka kwenye mashimo ya upotevu wa kijinsiya na matokeo ya kuteleza kwao yalionekana baada ya kupita muda. Kwa nini basi nasi turudie makosa waliyofanya wengine?

Njia ya maendeleo haijapotea mwituni, watu wote wanajua kuwa ni njia ya kujistahi, amali njema na tabia nzuri.

Vilevile njia ya maangamivu haijapotea, na watu wote wanajua kuwa ni njia ya uovu, ulevi na tabia mbaya.

Ripoti zinasema: “Vijana wamefuata njia mbaya inayopelekea kukata tamaa na kupotea na wanajiona kuwa hawana thamani wala maana, na wanahisi kupotea na chuki.” Ripoti za hivi karibuni zinasema kwamba paketi bilioni moja za madawa ya kulevya aina ya ‘L.S.D.’ hutumiwa na vijana kila mwaka mjini London. Vile vile zaidi ya watumiaji wa bangi laki moja nchini Marekani wameshikwa na wazimu, baadhi yao wamepelekwa kwenye mahospitalli ya wendawazimu au wengine wamefariki barabarani.4

Ikiwa mmoja wetu anahofia yasitokee haya basi inampasa aizibe njia ya kuelekea kwenye mkondo huo kabla haujaanza kwenda. Upepo unavuma kwa kasi sana katika zama zetu hizi. Wala si muda mrefu vijana wetu nao pia yatawapata yaliyowapata vijana wa Marekani na London iwapo wataendelea kuranda randa kwenye njia ya ngono na maovu.

Vilevile wasichana wetu yatawapata kama wakifuata njia hiyo hiyo, yaliyowapata wasichana wa Ulaya kiasi kwamba leo imekuwa huko Ulaya msichana amuoa msichana mwenzake yaani mmoja ni “mume” na mwingine ni “mkewe” na kisha ‘hulala’ naye. Madhambi haya yanafanywa hivi leo na wasichana Amerika na Urusi.

Wasichana wawili wa Marekani mmoja akiwa na umri wa miaka ishirini na tano na mwengine wa miaka ishirini na tisa waliomba waruhusiwe kuoana, naye mkuu wa jimbo lao analichunguza ombi lao hilo. Hata hivyo yule msichana mdogo ‘mke mtarajiwa’ (ambaye hucheza kwenye vilabu vya usiku) ameeleza kwamba yeye haogopi maneno ya watu, bali tatizo pekee anawaogopa wavulana wa ‘mchumba wake’ ambaye ana wavulana watatu mmoja wao mwanajeshi wa majini wa Amerika.5

Wanasema!!

Wanasema kwamba: “Mwanamke lazima asome.” Ndio, sawa lakini basi ndio aende uchi? Kwa kawaida herufi zinaandikwa kwenye kurasa za vitabu, iweje vijana kwenye vyuo vikuu wazisome miguuni mwa wasichana?

Mtume Muhammad (saww) amesema kabla ya zaidi ya miaka elfu kwamba; “kutafuta elimu ni lazima kwa kila Muislamu mwanamume na mwanamke.” Ni wazi kwamba hilo laweza kuwa bila ya kwenda uchi, msisimko au matatizo yoyote. Kwa nini basi shule mnazifanya za mchanganyiko? Kwani msichana hawezi kufahamu kusoma mpaka akae pembeni mwa mvulana saa zote akimkonyeza?

Au barabara haifikiki nyumbani mpaka wakutane wanafunzi wa kike na wa kiume na mikono ya wasichana kutiwa kwapani mwa wavulana?

Wanasema: “Hali imebadilika! Hizi ni enzi za kwenda angani na Atomiki, hatuwezi kuishi kizamani, ambazo ilikuwa ukisafiri mpaka upande punda na kina baba kuwaficha mabinti zao wasijidhihirishe...!”

Lakini ee jamani huko kwenda angani ndiko kunakomfanya msichana aidhihirishe miguu? Au mwanamke akivaa hijab, ndege haitaruka, hata mtu apande punda?

Na je, Atomiki imegundua kwamba sasa mwanamke aonyeshe mwili wake mbele za watu?

Hebu ijaribuni heshima na kujistahi, mtaona kwamba hizi zama za kwenda angani hazitarudi kuwa za kwenda ardhini (ikiwa mwanamke atajiheshimu na akajichunga). Na hiyo Atomiki pia haitageuka ikiwa mwanamke atarudi kuangalia anayekwenda uchi.

Jaribuni hivyo mtaona kuwa mwanadamu amekuwa na ubinaadamu sana pale anapofanya ngono kulingana na mipaka, vipimo na misingi yake bila ya kupetuka mipaka ya dini na akili.

Pia wanasema: “Sisi twampenda mwanamke, kwa hivyo twataka tumuone yeye na manukato yake kila mahali.”

Je! kumpenda ndio kumtangaza barabarani? Je! kumpenda ndio kulichukua ua liliochanua na kulianika kwenye madirisha yote? ...Hapana... Nyinyi hamumpendi mwanamke, bali nafsi zenu! Nyinyi mwamuua mwanamke, mwamuua! Ama sivyo?

  • 1. Soma mlango wa Nikah (ndoa) katika vitabu vyote vya Fiqh
  • 2. Man the Unknown. Page.98
  • 3. Presence le Corps et I’Ane R.Beit
  • 4. Jar ida la “Assuruuq” Toleo No.4 mwaka wa 1
  • 5. Jar ida la “Assuruuq” Toleo No.1 mwaka wa 1