Ratiba Kwa Vijana
Imam Ali (a.s) amesema: “Waangalieni sana vijana, na hasa wale wadogo…”
Amesema pia: “Moyo wa kijana mdogo ni kama ardhi ambayo haijalimwa, kila utakachokipanda kitapokewa (kitamea).”
Kwa hivyo kuwashughulikia wavulana na wasichana ni muhimu sana kuliko kuwashughulikia watu wazima, haifai kuwatelekeza kwa sababu ya umri wao mdogo, huenda ikawa msichana aliyeshikamana na dini wakati wa udogo wake akawa ana nafasi kubwa na akaweza kutoa huduma kubwa sana kwenye njia ya Mwenyezi Mungu.
Kwa maana hiyo mwanamke mwanadini ni lazima awajibike katika kusimamia malezi mazuri na ya kimapinduzi kwa wasichana. Lakini je! ratiba ya kazi hiyo ni ipi? Na itafanywaje?
Majibu yake ni kama ifuatayo.
Suala zima la kuwaweka pamoja. Ni lazima kuwe na jumuiko litakalounganisha wanawake na wasichana; na hilo litapatikana kwa njia ya kuwafundisha Swala, au tafsiri ya Qur’an, au masomo mengine, vilevile kuwapa mafunzo ya ushonaji, upishi na mengineyo, bila ya kusahau jumuia za kila wiki za kujitolea.
Kupanga Nyakati
Ni lazima kupangwe njia maalum za kuzifuata, kwa kupanga vipindi maalum; mathalan, kipindi cha miezi minne ya kwanza kipangwe ni cha kuinua kiwango chao cha masomo kwa daraja maalum. Kisha miezi minne ya pili: kuwajenga wawe wana tabligh, lakini haipasi kuwafahamisha muda.
Mbinu Na Mfumo Mzima Kwa Ujumla
Kinachotakiwa katika sehemu ya kwanza ni kujenga urafiki na wasichana na kujaribu kuwapa umuhimu zaidi katika mazungumzo nao ya ana kwa ana. Ni lazima kwanza vitayarishwe vitabu na kaseti zifaazo kwa kila awamu; mathalan, wale wa awamu ya kwanza watayarishiwe vitabu vya Hadithi na kaseti zinazolingana na umri wao, na kuwafanya wawe na ushindani kati yao kwa kuwawekea zawadi kwa washindi.
Vilevile wazoezwe kutekeleza majukumu yao wanapokuwa majumbani mwao kama vile kuandika, kupeana kaseti, kusoma majarida na kurekodi kanda.
Vilevile kazi za nje, kama mihadhara, kutembelea wagonjwa na kupanga safari maalum za wanawake.
Huu ndio mfumo mzima anaopaswa mwanamke aufuate ili awe kama anavyomtaka Mwenyezi Mungu awe mwanzilishi na mbebaji wa ujumbe, lakini mfumo huu unahitajia ratiba maalum ya kuufuatilia, tunamshukuru Mwenyezi Mungu wa viumbe vyote.