Haki za Ndoa
Kwa mtazamo wa dini, mke ni mshirika katika maisha; yeye ndiye anayemkamilisha mume na mume ndiye anayemkamilisha mke. Wewe wamuhitajia, naye pia akuhitajia. Mke si mtumishi, bali ni ‘mke’ kwa hivyo anafaa kutumikiwa.
Ama haki ambazo mwanamke lazima amtekelezee mumewe ni mbili tu. Ya kwanza ni haki ya kitandani (tendo la ndoa), yaani kuonana kimwili (ngono), kumpa mwili wake mumewe anapotaka. Pia Uislamu hapo wasema mtu ajiandae kwa mkewe kama ambavyo mke ajiandae kwa mumewe (kabla ya kuonana). Mume anapoomba hilo na hali zinaruhusu, basi mke ni lazima awe amejiandaa. Sayyidna Ali (k.w.) amesema: “Mke aliye muovu zaidi ni yule amnyimaye mumewe (tendo la ndoa).”
Haki ya pili ni mume kujua mke anapotoka nyumbani, yaani ajue mke anakokwenda. Haifai katika Uislam mke ajiendee tu popote au vyovyote atakavyo huku mumewe hataki. Mtume (saww) amesema: “Mke yeyote atakayetoka nyumbani kwa mumewe bila ya idhini ya mumewe, basi huyo hulaaniwa na kila kitu kinacho chomozewa na jua na mwezi mpaka mumewe amridhie.” Kwa kuwa ajua sababu iliyomfanya atoke ni nzuri hawezi kumficha mumewe. Na ikiwa mume ni mtu muúmini haamrishi wala hakatazi ila kwa sababu ya maana. Basi mke anapotoka bila ya idhini yake kila kitu kitamlaani mpaka mume ajue sababu ya kutoka kwake na aridhike. Hizi ndizo haki mbili za mume kwa mkewe.
Ama haki za mke kwa mumewe ni nyingi:
Mume amfurahishe mkewe ki-ngono, na kimapenzi na haifai mume aache kabisa kabisa kuonana na mkewe kimwili. Haifai asionekane kwa muda mrefu bila ya udhuru wa maana.
Ni juu ya mume amtimizie mkewe mahitaji ya lazima, nyumba inayofaa, mavazi yafaayo na chakula.
Mke si mali ya mume bali ni mshirika wake katika maisha; anaingia mkataba na mume kwa ajili ya kuishi pamoja na kupendana pamoja na kubeba mzigo wa watoto pamoja.
Kwa hivyo, mke si katika majukumu yake kumtumikia mumewe bali kinyume chake. Mume anakalifiwa kisheria na kibinadamu kutosheleza mahitaji yote yanayohitajika.
Ama kupika, kufagia, kufua au kuajiriwa ili kupata pesa, haya yote si wajibu wa mke. Anaweza asipike, asifagie, hata asimnyonyeshe mtoto. Kwani haki yake kwa mtazamo wa dini, mume amlipe kwa kuwa maziwa anayompa mtoto ni sehemu ya maisha na mwili wake. Baba ndiye mwenye jukumu la ulezi wa mtoto, kwa hivyo ni haki yake mke alipwe kwa kunyonyesha.
Mke ni “mke” wala si mtumishi, atakapojitolea kufagia, kupika, kunyonyesha na kulea si haki yake bali aweza kujizuia na hayo na haijuzu mume kwa vyovyote kumtenza nguvu apike, afagie afue au aoshe vyombo.
Akijitolea naye mume asimpatilize mathalan kwa kuzidi kutia chumvi kwenye chakula au maji si baridi, nyumba chafu au haikusafishwa vizuri. Kwa sababu hawajibiki na hayo yote, madhali amejitolea basi afanye ni hisani kwa mume. Na kwa sababu hii ndipo tunakuta historia yasema kwamba Mtume (saww) hakulaumu katu mapishi ya chakula katika maisha yake. Alikuwa akishirikiana na wakeze kupika na kufagia na akisema: “Wale wafanyao kazi nyumbani mwao ndio wa kweli katika umma wangu.”
Ama hali ya tatu ya mwanamke ni pale anapokuwa mama, uislamu unawalazimisha watoto kumheshimu, inasema Qur’an: “Wala usiwaambie Ah!…” (17:23)
Kijana mmoja alikwenda kwa Mtume (saww) akasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni yupi aliye bora zaidi kwangu nimtendee mama?” Mtume akamjibu: “mamako.” Yule kijana akauliza “kisha nani?” Mtume akajibu: “kisha mamako.” Akuliza tena: “Kisha nani?” Akajibu: “Kisha mamako” akauliza (mara ya nne): “Kisha nani?” Akamjibu: ”Kisha babako.”
Yaani hii ni kuonyesha kwamba haki za mama ni nyingi zaidi kuliko za baba mara tatu zaidi.
Alikwenda kijana mwingine kwa Imam Sadiq (a.s) akasema: “Ee mjukuu wa Mtume, mimi nilimbeba mama yangu mgongoni kwangu na kuhiji naye mara nyingi akiwa mgongoni kutoka Madina hadi Makka; je! nimetekeleza haki zake?” Akatabasamu Imam Sadiq (a.s) akamjibu: “Wallahi bado hujatekeleza haki yake hata ya usiku mmoja alipoamka akakuwekea titi lake mdomoni ukanyonya.”
Hivi ndivyo ilivyo, utaona kwamba Uislamu unaangalia mwanamke kama mwanadamu aliyeumbwa na Mungu kwa matakwa haswa ya muumba, kama alivyoumba mwanamume kwa kutoka kwake yeye muumba na ndio maana akaamrisha mwanamke ahishimiwe.
Anapokuwa msichana, dini yakwambia mheshimu. Anapoolewa, dini yakwambia mheshimu, na anapokuwa mama, dini yakwambia mheshimu.
Dini inawatahadharisha wale wanaowapiga wake zao, inasema: “Mwenye kunyoosha mkono wake ili amzabe kofi mwanamke huyo ni kama aliyeunyoosha mkono wake motoni.”
Pili inasema: “Mkeo asiwe ni mtu umchukiaye, kwa kuwa mwanamke ni ua la mrehani si mtumishi. Na jiepusheni na wivu pasipo mahali pake, kwani kufanya hivyo humfanya yule mzima akapata maradhi, na asiye na hatia kumtia kwenye shaka.”