read

Wasiya Kwa Mwanamke Mu’umin

Katika historia yetu adhimu, mwanamke ana sehemu kubwa na ya kijasiri, ambayo mara nyingine yamu­onyesha akiwa kwenye uwanja wa mapambano, na wakati mwingine kwenye medani ya kupambana na ubatili, kuanzia bibi Maryam, bibi Khadija, bibi Fatima, bibi Zainab, Ummu Ammar na wengineo.

Kwa kweli mwanamke, pamoja na kazi zake za kawaida bado ana kazi kubwa ya kupambana na kubeba mas’uliya (majukumu). Wanawake wangapi walioviporomosha viti vya enzi vya mataghuti? Wanawake wangapi wameshinda madhalimu? Na kwa sababu hiyo, si ajabu kuwa katika Qur’an, neno kali dhidi ya ufalme na utaghuti lilitamkwa na mwanamke pale aliposema:

“(Malkia) akasema:

“Hakika wafalme wanapoingia mji (wa watu) huuharibu na wanawafanya watukufu wake kuwa dhalili; hivi ndivyo wanavyofanya (daima).” (27:34)

Ewe mwanamke mu’min!

Daima kumbuka kuwa Mungu wako na Mungu wa mwanamume ni mmoja, na uwezo aliokupa wewe ndio aliompa mwanamume. Majukumu mamoja, haki moja na marejeo yenu mwishowe ni mamoja tu.

Ama tofauti za ki-maumbile zilizoko kati yenu, hazimaanishi kwamba wewe ni madini ya feruzi (isiyo na thamani) na yeye ni almasi. Nyote mwato­kana na Adam na Adam atokana na udongo.

“Enyi watu! Hakika tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekufanyeni mataifa na makabila (mbali mbali) ili mjuane. Hakika ahishimiwaye zaidi miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule am­cha­ye Mungu zaidi..” (49:13)

Kuwa mume siyo fahari na ubora kama vile ambavyo kuwa mke si udhalili na aibu, bali kuwa hivyo ni njia tu ya kujuana na hivyo kuweza kushirikiana katika kubeba majukumu. Kama vile ambavyo haifai kwa mtu wa kabila fulani ajione bora kuliko mtu wa kabila nyingine kwa ajili ya nasaba na ukoo wake, au watu wa nchi fulani wajione bora kuliko watu wengine kijografia au kilugha, basi hata kwa mwanamke si haki ajione bora kuliko mwanamke mwingine au kinyume chake, ila kwa kumcha Mungu tu.

“…Kwa hakika aliye mbora zaidi kwa Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi.” (49:13)

Kwa hivyo basi, ni lazima kwa mwanamume amtilie manani sana mwanamke, kwani kuwapenda wanawake ni katika imani, na kadri mtu anavyozidi kuwa na imani kama asemavyo Mtume (saww) ndivyo anavyozidi kuwapenda wanawake. Siyo penzi dhaifu la kimwili bali penzi tukufu la kidini! Mtume (saww) wa Mwenyezi Mungu pia amesema mara nyingi: “Nawausia juu ya wanawake.”

Ewe mwanamke mu’umin! Ewe Mtetezi wa Mwenyezi Mungu, usiwe na kipenzi ila Mwenyezi Mungu, kwani yeye humpenda yule ajipendekezaye kwake. Na ufunge milango yako ya duniani ili Mwenyezi Mungu akufungulie milango ya mbinguni! Wacha maneno ya kipuuzi, wacha matamanio na ujue ya kwamba hakuna uokovu mwingine ila wa Mwenyezi Mungu tu na Mungu hana khiyana yeye ndiye mbora, mwenye kunusuru, kata uhusiano wako wa upuuzi na ufanye uhusiano na jihadi na kina dada wana-dini.

Heshimika na hijab yako na uifanye kuwa ndiyo silaha ya kuwapinga mataghuti wanao kutaka uwe kama mwanaserere (kijisanamu). Ukiwa na hijab yako, geuka uwe mwangaza wa uchan­gamfu, kwani hijab siyo jela na kaburi la kuzikia uwezo wako, bali ni njia ya kuwa huru na ku­tenda. Usitosheke na kuwa mtumwa mwenye thamani tu, bali uwe mwenye nafasi yenye tha­mani.

Zielewe mbinu za mataghuti za kusaga shaksiya ya mwanamke, kwani mbinu zake ni chafu na zenye mizunguko mingi, mara nyingi hutumiwa mbinu zitakazofurahisha kuliko zitakazochukiza. Taghuti ni bidhaa isiyochoka ya Iblis. Taghuti hutumia vitimbi, mizunguko na udanganyifu, yeye huyachochoea matamanio ili azivunje heshima, na anasa ili kuivua heshima na hutumia ngoma na muziki ili kuiba imani za ucha Mungu.
Na ili uihifadhi heshima yako, basi ni lazima upambane na njia potofu ambayo ni nafsi inayoamrisha maovu na utahadhari na mata­manio yako. Kisha jiulize: ni mwanamke gani anayeogopewa na taghuti? Je! Ni yule ambaye asubuhi akitafuta virembesho, marinda mazuri na hutoka akiwaonyesha watu wenye “Kiu” ma­pambo yake? Au ni yule anayekwenda kwenye duka la vitabu akatafuta magazeti yenye fedheha na visa vya uongo vya mapenzi? Au je! ni yule anapokuwa kwenye sherehe ataka awe mithili ya tausi akiringia nakshi za nguo zake na alivyo­tengeza nywele na mipaka ya muhimu kwake ni Jiografia ya mwili wake tu (alivyoumbika)? Au mwanamke anayeogopewa na Taghuti ni yule mpiganaji jihadi anayetafuta medani ya mapa­mbano, kama kipepeo atafutaye ngome ili awe kama askari mwenye tahadhari.

Usiabudu virembesho na mapambo, kwani wewe ni mkuu kuliko chupa ya manukato au mti wa kupakia wanja, au kitambaa cha rinda, na fahamu ya kuwa uzuri wa roho ndio wanaowaunganisha watu na si uzuri wa mwili. Jipambe na tafakuri na hisia zako zitie huruma kwa familia maskini, kwani moyo ni kama mmea, mtu asipouangalia kwa huruma na upole utakufa.

Tahadhari sana na kushindwa, kwa sababu silaha kubwa ya mkoloni ni kushindwa kwa watu, yaani ndiko kushindwa kwa mwanamke; na ikiwa mwanamke ameshindwa, ni kizazi gani basi kitakacholelewa ila kitakuwa ni kizazi cha walioshindwa tu?

Kuwa ni mwenye kutengeza mustakbali, na uingie kwenye mapambano ya kishujaa, kwani jihadi ni wajibu wako wa kimsingi na zama hizi tunazoishi ni zama za hujuma za kikafiri dhidi ya Uislamu, kwa hivyo kujilinda hakuhitaji ruhusa!

Shiriki kwenye mipango na wanaume, kwani si haramu kuzungumza na wanaume na kukaa nao maadam muko katika njia ya Mwenyezi Mungu na uchunge heshima ya kisharia.

Mbele ya mataghuti: toa hoja ya nguvu, kataa, piga kelele. Kumbuka kuwa mataghuti wengi wameanguka kutokana na upinzani wa kina Zainab na mikono yao ya chuma.

Toka kwenye upenu wa khofu uliotiwa na vibaraka wa wakoloni, au kulala na kuzunguka jikoni tu kama wanavyokutaka uwe.

Ewe mwanamke mu’umin!
Wakati tunaposoma Qur’an tukufu kuhusu mwanamke tunapata ukweli ufuatao:
Mwanamke na mwanamume kwa pamoja wana jukumu la kuchunga nafsi na watu. Mwenyezi Mungu amesema:

“Waambie waislamu wanaume wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, hili ni takaso kwao, bila shaka Mwenyezi Mungu anazo habari za (yote) wayafanyayo. Na waambie waislamu wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao.” (24: 30-31)

Kwa hakika mwanamke na mwanamume ni vipenzi wao kwa wao, mwanamume yampasa amthamini mwanamke na kumtakia mema, na mwanamke pia afanye hivyo hivyo.

“Na waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki (vipenzi) wao kwa wao. Huamrisha mema na hukataza mabaya, na husimamisha Swala na kutoa Zaka na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake; hao ndio Mwenyezi Mungu ataware­hemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.” (9:71)

Mwanamke na mwanamume wana haki ya ku­pata sawa kulingana na wajibu wao watakao­utekeleza, na Mwenyezi Mungu anahifadhi haki ya mwanamke kama anavyohifadhi ya mwanamume, kama alivyosema katika Qur’an:

“Na watakaofanya vitendo vizuri wakiwa ni wanaume au wanawake hali wao ni wenye kuamini, basi hao wataingia peponi wala hawatadhulumiwa hata kokwa (konde) ya tende.” (4:124)

Amesema tena Mwenyezi Mungu:

“Mola wao akawakubalia (kwa kusema): “Hakika mimi sitapoteza amali ya mfanya juhudi miongoni mwenu awe mwanamume au mwanamke..” (3:195)

“Wafanya wema wanaume au wanawake hali ya kuwa ni waislamu, tutamhuisha maisha mema, na tutawapa ujira wao (akhera) mkubwa kabisa kwa sababu ya yale mema waliyokuwa wakiyatenda.” (16:97)

“Siku utakapowaona waislamu wanaume na wais­lamu wanawake, nuru zao zitakwenda mbele yao na kuliani kwao (wanaambiwa): “Furaha yenu leo (mnapewa) mabustani yapitayo mito mbele yake ku­kaa humo daima, huku ndiko kufaulu kukubwa.” (57:12)

Hapana tofauti kati ya mwanamume na mwanamke katika uharamu wa kuingilia haki zao. Mwenyezi Mungu amesema:

“Hakika wale walio wafitini (waliowaudhi) Waumini wanaume na Waumini wanawake, kisha hawakutubu, basi watapata adhabu ya Jahannamu na watapata adhabu ya kuungua.” (85:10)

Na kuna Aya nyingi ambazo kwanza Mwenyezi Mungu anazungumza na Mtume wake juu ya mwanamke mwislamu, akimtaka Mtume aku­bali kuahidi kwao kubeba majukumu, amesema (s.w.t.):

Ewe Nabii! Watakapokuja wanawake walioamini wanaokuahidi ya kwamba hawatamshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote, wala hawataiba wala hawatazini, wala hawataua watoto wao, wala hawa­taleta uzushi wanaozusha tu wenyewe baina ya mi­kono yao na miguu yao wala hawatakuasi katika jambo jema, basi peana ahadi nao na uwatakie maghfira kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghfira, mwingi wa rehma.” (60:12)

Ingia kwenye sehemu yako aliyoitaka kwako Mwenyezi Mungu ya ukhalifa wa dunia na ku­jenga maisha na usingoje wanaume wakwambie la kufanya katika kutetea na ujipatie nguvu za wanaume kwa uthabiti wao. Na uizuwie dhulma ya wanaume kwa matakwa yao; na ujue ya kwamba mwanamke anaweza kufanya mambo mengi na kutoa mchango wake katika mambo mema. Na mwanamke ni mtukufu pale anapojuwa kuwa yeye ni mtukufu.

Pambana na ada na desturi potofu za kijamii ambazo Mwenyezi Mungu hakuteremsha uhalali wake hasa zifanywazo katika nyanja za kijamii k.v. kwenye harusi ambapo mwanamke hukubali bei rahisi au kujiuza kwa vitu vya anasa tu. Fikiri sana juu ya mali ya mumeo, ibadilishe hali yake, mwenendo wake, badili washirika wake wasiofaa, na katika mali yake badilisha mfumo wake.

Kazi yako si kulea watoto tu, kama wasemavyo, bali kazi hiyo ni jukumu lako na mumeo, wajibu wako ni kama ule wa mwanamume katika nyanja zote. Usikubali kuchukua nafasi ya pili kuwekwa pembeni; ondoa fikra za kufuata. Jivishe vazi la uongozi usijiweke nyuma katika njia ya uongofu.

Muige mwanamke mtukufu katika Historia, muige bibi Maryam bint Imran, mamake Masih (Isa (a.s)) mtetezi, mpambanaji aliyawakemea Waisrael. Au muige bibi Asya bint Muzahim, mke wa dikteta Fir’aun, mwanamke aliye muamini Musa (a.s) na kufa shahid katika njia ya haki akikataa maisha ya anasa duni. Au uwe mfano wa bibi Khadija ambaye alimcha Mungu na cha kaizari pia alimpa Mungu! Aliyejitolea kwa hali na mali kwa ajili ya uka­ndamizwaji. Au pia uwe mithili ya bibi Fatima ali­yehama (Hijra) akapambana kwa jihad, akake­mea, akatoa hoja za nguvu na kuwanyima usi­ngizi matapeli. Au pia jifanye kama bibi Zainab, sauti ya kimapinduzi iliyo kataa kusalimu amri kwenye huzuni, kukata tamaa na kutishwa.

Usikubali kuvunjwa moyo na nduguzo, jamaa zako au marafiki juu ya kufuata njia ya jihadi na kupambana na taghuti, kwani kumridhisha Mwenyezi Mungu ndilo jambo la kwanza kabla ya viumbe, na watu wako hawana mamlaka ya kupigana na hukmu ya Allah.

Jiweke kwenye kushiriki na wanaume na wanawake, na uwe na nafasi muhimu kwani lau kama Mwenyezi Mungu hakutaka mwanamke awe na nafasi muhimu asingemuumba mwanamume kwa njia ya mwanamke.

Uwe mume, pale panapokosekana mwana­mume, kwani uume si mwili bali ni wa mwamko na msimamo. Wanawake wangapi wana nguvu kushinda wanaume elfu, na kuna wanaume wangapi walio madhaifu kuliko wanawake.

Kuwa mwana mapinduzi. Kuwa mpiganaji. Kuwa kila kitu lakini usiwe pambo la jikoni au godoro la kitandani au sahani iliyoangikwa ukutani, au sauti katika nyimbo, au picha ya kupamba ukurasa wa jarida.

Jisome sana, fikiri sana, kwani “Kufikiri saa moja ni bora kuliko ibada sabini.”

Ukuze mwamko wa leo wa kisiasa kwa kusoma vitabu vya siasa, na kufuatilia matukio ya kila siku, kwani yule anayezijua zama zake na hali zilivyo, hawezi kuvamiwa na majanga na kushtuliwa na matukio.

Jizoeze mbinu za mapambano, kwani mwanamke mwislamu mwenye nguvu ni bora kuliko mwanamke mwislamu dhaifu, na hivyo hivyo mwanamume mwislamu mwenye nguvu ni bora kuliko asiye na nguvu.