read

Aya 32 – 44: Mungu Anauliza Na Iblisi Anajibu

Maana

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwaamuru Malaika kumsujudia Adam kwa sijda ya kimaamkuzi sio ya kiibada. Wakatii wote, lakini Ibilisi akaasi. Maulamaa wamehitilafiana kuhusu jinsia ya Iblisi, kuwa je, alikuwa Malaika kisha akafukuzwa au alikuwa shetani tangu mwanzo?

Mzozo huu ni tasa. Maadam Ibilisi kwa hali yoyote ni mwenye kulaumiwa na mwenye kufurushwa. Alpojizuia kusujudu Mola Mtukufu alimuuliza:

Akasema(Mwenyezi Mungu): Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na waliosujudu?
Je, wewe una cheo zaidi au ni mtukufu sana kuliko waliomsujudia Adam?
Akasema (Iblis): “Haiwi mimi kumsujudia uliyemuumba kutokana na udongo mkavu kwa matope meusi yenye kufinyangwa.”

Iblisi aliasi na kufanya jeuri, sio kwa kitu kingine isipokuwa ni ubaguzi wa rangi tu. Na kila mwenye kufanya ubaguzi kwa sababu ya asili yake na jinsia yake, basi ni mwenye kulaaniwa, kufukuzwa na kulaumiwa; sawa na Iblisi.

Akasema (Mwenyezi Mungu): Basi toka humo, kwani hakika wewe ni mwenye kufukuzwa na hakika itakuwa juu yako laana mpaka siku ya malipo.

Humo, ni humo mwenye daraja ya juu. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu alimfukuza Iblisi kutoka kwenye rehema yake hadi kwenye adhabu yake na akamfanya ni maluuni kwa ndimi zote mpaka siku ya Kiyama, ikiwa ni malipo ya kiburi chake na kuacha kwake kumtii Mwenyezi Mungu.

Akasema (Iblisi): “Mola wangu! Nipe muda mpaka siku watakapofufuliwa.”

Alitaka muda huu kwa haja yake aliyoikusudia, tutakayoifafanua mbele (Mwenyezi Mungu) akasema: Basi hakika wewe ni katika waliopewa muda mpaka siku ya wakati maalum.

Hiyo ni siku ya kupuliziwa parapanda ambayo inafahamishwa na Aya isemayo:

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَنْ فِي السَّمَاوَاتِ وَمَنْ فِي الْأَرْضِ{68}

“Na itakapopuziwa parapanda wazimie waliomo mbinguni na waliomo ardhini” (39:68)

Akasema (Iblisi): Kwa ulivyonipoteza,

Yaani kwa sababu ya kunitia mtihani wa amri ya kumsujudia Adam ambayo imeniingiza katika upotevu na uasi, basi nitahakikisha ninawazaini hapa ardhini na nitawapoteza wote, isipokuwa waja wako waliosafishwa.

Iblisi alichukua ahadi ya kuchukua kisasi cha maafa yake kwa kiumbe hiki kilichokuwa ni sababu ya kufukuzwa kwake kutoka rehema ya Mola wake hadi kwenye laana yake.

Akasema (Mwenyezi Mungu): Hii ni njia juu yangu mimi iliyonyooka.

Hii ni ishara ya kujichunga wale wenye ikhlasi kutokana na shetani na upotevu wake.

‘Juu yangu mimi,’ yaani ni yenye kuthibiti kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu; mfano kauli yake Mwenyezi Mungu: “Mola wenu amejilazimisha rehema” Juz. 7 (6:54).

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amejilazimishia kwamba ikhlasi ndiyo njia ya kunyooka. Mwenye kuifuata ataokoka na mwenye kukengeuka nayo ameangamia.

Hakika waja wangu hutakuwa na mamlaka nao, isipokuwa wale wapotofu waliokufuata.

Wale wanaoabudu pesa wakiuza dini na nchi kwa kila atakayetoa pesa. Ama wale wema wenye ikhlasi, hawawezi hata kusogelewa na Iblisi, sikwambii kuwa na mamlaka nao. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 8 (7:11- 18).

Na hakika Jahannam ndipo mahali pao walipoahidiwa wote.

Huko kwenye shimo la Jahannam watakutana wote, Iblisi na wafuasi wake. Kila mmoja atamlaani mwenzake na kumkana; mfuaswa atamkana mfuasi. Kwa maelezo zaidi angalia kifungu cha ‘Hotuba ya shetani’ katika Juz. 13 (14:22)

Ina milango saba, kila mlango una sehemu waliyotengewa.
Imesemekana kuwa makusudio ya milango ni milango hasa kwa maana ya tamko lenyewe. Wengine wakasema makusudio ni tabaka na kwamba baadhi ya moto uko juu ya baadhi ya mwingine; na kuwa kila tabaka ina jina lake inalolihusu; kama vile Jahnnam, Jahim, Ladhaa, Saqar, Hutama n.k.

Vyovyote yatakavyokuwa makusudio, hali halisi inajulikana; kwamba maovu yana daraja; kuna yaliyo makubwa ya hatari, yaliyo madogo yasiyo na hatari na yale ya katikati. Kila ovu lina adhabu yake inayolistahili bila ya kuzidi. Tumefafanua katika Juz. 13 (46 – 52). Kifungu cha ‘Jahannam na silaha za maangamizi.’

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ {45}

Hakika wenye takua watakuwa katika Bustani (Pepo) na chemchemi.

ادْخُلُوهَا بِسَلَامٍ آمِنِينَ {46}

(Wataambiwa): Ingieni kwa salama mkiwa na amani.

وَنَزَعْنَا مَا فِي صُدُورِهِمْ مِنْ غِلٍّ إِخْوَانًا عَلَىٰ سُرُرٍ مُتَقَابِلِينَ {47}

Na tutaondoa chuki iliyokuwamo vifuani mwao wawe ndugu, juu ya viti wakielekeana.

لَا يَمَسُّهُمْ فِيهَا نَصَبٌ وَمَا هُمْ مِنْهَا بِمُخْرَجِينَ {48}

Humo hayatawagusa machovu wala hawatatolewa humo.

نَبِّئْ عِبَادِي أَنِّي أَنَا الْغَفُورُ الرَّحِيمُ {49}

Watanabahishe waja wangu ya kwamba mimi ndiye Mwenye kughufiria, mwenye kurehemu.

وَأَنَّ عَذَابِي هُوَ الْعَذَابُ الْأَلِيمُ {50}

Na kwamba adhabu yangu ndiyo adhabu iliyo chungu.