Aya 5-9: Wanyama, Farasi, Nyumbu Na Punda
Maana
Na wanyama amewaumba, katika hao mnapata joto na manufaa na wengine mnakula.
Wanyama waliokusudiwa ni wale wa kufugwa amabo ni ngamia, ngombe, mbuzi na kondoo.
Qur’an ilishuka wakati ambao maisha ya kilimo na mengineyo yalikuwa hayapangiki bila wanyama. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja aina mbalimbali za wanyama na faida zake katika Aya kadhaa, kwa makusudio ya kumkumbuka Mwenyezi Mungu na neema zake kwa waja wake ili waweze kumcha Yeye katika matendo yao na kauli zao. Miongoni mwa Aya hizo ni: Juz. 8 (6: 143-144).
Katika Aya hii tuliyo nayo Mwenyezi Mungu ametaja faida tatu za wanyama; Joto kwa maana ya mavazi ya kuzuia baridi yanayotokana na ngozi za wanyama, sufu, manyoya yake n.k. Ametaja manufaa, yakiwa ni pamoja na maziwa, samli na kulima. Ama kauli yake ‘mnakula’ ni nyama pamoja na bidhaa za maziwa ambazo pia ni miongoni mwa manufaa.
Na mnaona raha mnapowarudisha jioni na mnapowapeleka asubuhi.
Makusudio ya kuona raha hapa ni kuona raha ya mandhari ya wanyama hasa wakiwa wamenona. Makusudio ya kuwarudisha jioni ni kuwarudisha zizini kutoka malishoni na kuwapeleka asubuhi ni kuwatoa zizini kwenda malishoni. Mandhari haya kwa hakika ni mazuri yanayoleta raha kwenye nafsi.
Na hubeba mizigo kupeleka kwenye mji msiyoweza kuifikia ila kwa mashaka ya nafsi.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja faida ya wanyama kwa chakula na kivazi, hapa anataja kuwa pia wanyama ni nyenzo ya mawasiliano na uchukuzi kutoka mji mmoja hadi mwengine; na lau si hao basi binadamu angelipata tabu.
Hakika Mola wenu ni Mpole sana Mwenye kurehemu.
Miongoni mwa huruma zake ni kuwatumikisha wanyama kwa masilahi ya watu ilikuweza kurahisisha mambo na kupunguza tabu
Na farasi na nyumbu na punda ili muwapande na pambo.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja manufaa matatu ya wanyama, sasa anataja manufaa ya farasi, nyumbu na punda, ambayo muhimu zaidi ni kupanda na vipambo, katika wakati huo.
Na anaumba msivyovijua.
Kila mwanachuoni ameifasiri jumla hii kulingana na wakati wake na maisha yake. Baadhi ya wakale wamesema kuwa makusudio ni kuwa Mwenyezi Mungu anaumba aina ya wanyama, mimea na vitu vingine vingi sana ambavyo watu hawavijui.
Tabari anasema: Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu atawaumbia watu wa Peponi aina kadha za neema na atawaumbia watu wa motoni aina kadhaa za adhabu ambazo hakuna jicho lililoziona wala sikio lililozisikia au moyo ulioziwazia. Baadhi ya wafasiri wapya, akiwemo Sheikh Al-maraghi, wamesema:
“Hii ni ishara ya ndege, magari n.k.”
Maana yanayonasibiana na mfumo wa maneno – tuonavyo sisi – ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baada ya kutaja manufaa kwa waja wake, anasema kuwa haya ni machache miongoni mwa manufaa mengi msiyoyajua wala kujua idadi yake.
Kwa maneno mengine jumla hii inafanana na kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya ya 18 ya Sura hii: “Na mkizihisabu neema za Mwenyezi Mungu hamuwezi kuzidhibiti.”
Sha’rani amenukuu katika kitabu chake Al-mizani kutoka kwa Abu Hanifa, uharamu wa nyama ya farasi. Na kutoka kwa Shafii, Malik, na Ibn Hambal wamesema ni halali.
Ama nyama ya nyumbu na punda, amenukuu kutoka kwa Shafi, Abu Hanifa na Ibn Hambal kuwa ni haramu. Shia Imamiya wamesema kuwa nyama ya farasi, nyumbu na punda ni halali, lakini ni makruh.
Na ni juu ya Mwenyezi Mungu njia iliyo sawa.
Juu hapa, ni kwa maana ya wajibu. Aya hii inafanana na ile isemayo: “Hakika ni juu yetu kuonyesha uwongofu” (92:12). Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amejilazimisha kuwabainishia watu, kupitia Mitume, njia ya haki na ya uongofu.
Na nyingine ni kombo.
Yaani kuna njia zilizo sawa, kama vile Uislamu, na nyingine ziko kombo kombo, kama dini nyinginezo.
Lau angelipenda angeliwaongoza nyote.
Yaani kama Mwenyezi Mungu angelitaka angeliwaelekeza watu wote kwenye imani kwa nguvu na asingelikufuru yeyote.
Lakini Yeye Mwenyezi Mungu amemwachia mtu hiyari, baada ya kumbainishia njia mbili, kwa kuchukulia utu wake. Angalia Juz. 12 (12: 118).
هُوَ الَّذِي أَنْزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً ۖ لَكُمْ مِنْهُ شَرَابٌ وَمِنْهُ شَجَرٌ فِيهِ تُسِيمُونَ {10}
يُنْبِتُ لَكُمْ بِهِ الزَّرْعَ وَالزَّيْتُونَ وَالنَّخِيلَ وَالْأَعْنَابَ وَمِنْ كُلِّ الثَّمَرَاتِ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ {11}
وَسَخَّرَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ ۖ وَالنُّجُومُ مُسَخَّرَاتٌ بِأَمْرِهِ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَعْقِلُونَ {12}
وَمَا ذَرَأَ لَكُمْ فِي الْأَرْضِ مُخْتَلِفًا أَلْوَانُهُ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِقَوْمٍ يَذَّكَّرُونَ {13}
وَهُوَ الَّذِي سَخَّرَ الْبَحْرَ لِتَأْكُلُوا مِنْهُ لَحْمًا طَرِيًّا وَتَسْتَخْرِجُوا مِنْهُ حِلْيَةً تَلْبَسُونَهَا وَتَرَى الْفُلْكَ مَوَاخِرَ فِيهِ وَلِتَبْتَغُوا مِنْ فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ {14}
وَأَلْقَىٰ فِي الْأَرْضِ رَوَاسِيَ أَنْ تَمِيدَ بِكُمْ وَأَنْهَارًا وَسُبُلًا لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ {15}
وَعَلَامَاتٍ ۚ وَبِالنَّجْمِ هُمْ يَهْتَدُونَ {16}
أَفَمَنْ يَخْلُقُ كَمَنْ لَا يَخْلُقُ ۗ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ {17}
وَإِنْ تَعُدُّوا نِعْمَةَ اللَّهِ لَا تُحْصُوهَا ۗ إِنَّ اللَّهَ لَغَفُورٌ رَحِيمٌ {18}
وَاللَّهُ يَعْلَمُ مَا تُسِرُّونَ وَمَا تُعْلِنُونَ {19}