Aya 43 – 50: Waulizeni Wenye Ukumbusho
Maana
Na hatukutuma kabla yako ila wanaume tuliowapa wahyi.
Washirikina waliukana utume wa Muhammad na wakasema kuwa Mwenyezi Mungu hakutuma mtu kuwa mjumbe. Ndio Mwenyezi Mungu akabatilisha madai yao kwamba mitume na Manabii wote waliotangulia walikuwa ni watu wanaume wakiletewa wahyi; kama vile: Nuh, Ismail, Musa na wengineo. Kwa sababu lengo la kutumwa Mtume haliwezi kutimia ila ikiwa aliyetumwa ni jinsi ya wale waliotumiwa:
وَمَا أَرْسَلْنَا مِنْ رَسُولٍ إِلَّا بِلِسَانِ قَوْمِهِ لِيُبَيِّنَ لَهُمْ ۖ {4}
قُلْ لَوْ كَانَ فِي الْأَرْضِ مَلَائِكَةٌ يَمْشُونَ مُطْمَئِنِّينَ لَنَزَّلْنَا عَلَيْهِمْ مِنَ السَّمَاءِ مَلَكًا رَسُولًا {95}
Basi waulizeni wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui.
Makusudio ya wenye ukumbusho hapa ni wenye elimu wanaochunga haki; ni sawa wawe ni katika Watu wa kitab au wengineo. Maana ni kuwa enyi washirikina! Mkiwa na shaka na maneno yetu, basi waulizeni wajuzi wawambie kuwa mitume wote walikuwa ni watu.
Kwa hoja zilizo wazi na kwa Vitabu.
Yaani Mwenyezi Mungu aliwatuma Mitume wakiwa na hoja zilizowazi ambazo ni dalili na ishara. Na kwa vitabu ambavyo vina ubainifu wa dini, itikadi na sharia.
Na tumekuteremshia ukumbusho ili uwabainishie watu yale waliyoteremshiwa wapate kufikiri.
Maneno anaambiwa Muhammad (s.a.w.). Makusudio ya ukumbusho hapa ni Qur’an. Ilivyo hasa ni kuwa lengo la kutumwa Mitume na kuteremshwa vitabu ni kuwaongoza watu kwenye haki na uadilifu na maisha ya amani na raha.
Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘wapate kufikiri’ ni kuwa wapate kuizingatia vizuri Qur’an na kugundua siri zake na malengo yake wapate kujua kuwa imeteremshwa kwa maslahi yao.
Je, wameaminisha waliofanya vitimbi vya uovu.
Wafasiri wamesema kuwa makusudio ya waliofanya vitimbi hapa ni washirikina wa kiquraish, kwa vile wao ndio waliomfanyia uovu Mtume (s.a.w.) na wakamfanyia njama. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewahofisha na aina nne za adhabu:
1. Kwamba Mwenyezi Mungu awadidimize katika ardhi; kama alivyomfanyia Qarun:
فَخَسَفْنَا بِهِ وَبِدَارِهِ الْأَرْضَ فَمَا كَانَ لَهُ مِنْ فِئَةٍ يَنْصُرُونَهُ مِنْ دُونِ اللَّهِ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُنْتَصِرِينَ {81}
2. Au iwafikie adhabu kutoka wasipopajua, awaangamize ghafla, kama alivyofanya kwa watu wa Lut.
3. Au awakamate katika nyendo zao na wasiweze kuponyoka. Yaani awaangamize wakiwa wanashughulika kutafuta riziki.
4. Au awakamate kidogo kidogo.
Neno kidogo kidogo, limefasiriwa kutokana na neno takhawwuf; kama walivyosema wafasiri wengi wakiongozwa na Tabrasi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hatawaangamiza mara moja bali atawapa balaa ya kupungukiwa na watu na mali kidogo kidogo mpaka wa mwisho wao.
Kwani hakika Mola wenu ni Mpole, Mwenye huruma.
Miongoni mwa huruma zake ni kutowaharakishia adhabu wanayostahiki waasi, kwa kutumai kuwa watatubia na kuongoka.
Je hawavioni vitu alivyoviumba Mwenyezi Mungu vivuli vyao vinaelekea kuliani na kushotoni vikimsujudia Mwenyezi Mungu na vikimnyenyekea.
Wanaoambiwa hapa ni wale waliofanya vitimbi vya uovu, waliotajwa katika Aya iliyotangulia na pia inawezekana wanaambiwa watu wote. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema kwa kuwatahayariza wapinzani wenye inadi.
Makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Vivuli vinaelekea’ ni kuwa kila kitu kina kivuli; kama vile milima, miti, wanyama, majengo n.k. Na kauli yake: ‘kuliani na kushotoni’ ni ishara ya upande wa kitu kilicho na kivuli. Kwa sababu kivuli cha kitu kinakuwa upande mmoja kuanzia mawiyo hadi Adhuhuri na kinageuka upande wa pili kuanzia adhuhri hadi machweo.
Kwa hiyo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akaleta ibara ya kulia kwa upande mmoja na ibara ya kushoto kwa upande wa pili. Ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu: “ Na vivuli vyao asubuhi na jioni” Juz. 13 (13: 15) Ama kauli yake vikimsujudia Mwenyezi Mungu ni fumbo la utiifu. Unaweza kuuliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu alipotaja kulia ametaja kwa tamko la umoja na alipotaja kushoto akatumia tamko la wingi (yamin wa shamail)1 ?
Wafasiri wamelijibu hilo kwa majibu ambayo la karibu zaidi ni kuwa mfumo wa fasihi ya kiarabu wakitaja vitu viwili vyenye maana mbili tofauti kimoja kinatajwa kwa umoja na kingine kwa wingi; kama kusema kwake Mwenyezi Mungu: “Amejaalia viza na mwanga.”
Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baada ya kuwahadharisha washirikina na wenye inadi, anasema katika Aya hii, kwamba kila kilicho ulimwenguni – isipokuwa washirikina na wenye inadi – vinamnyenyekea na kufuata amri yake.
Na vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini katika wanyama na Malaika nao hawatakabari.
Viumbe vyote vya juu na chini vinafahamisha waziwazi kuweko aliyevifanya na kufahamisha uweza wake, elimu yake na hekima yake na dalili hii ndio tasbihi, tahmid, sujudi na rukui kwa muumbaji.
Pia haya ndio makusudio ya kusujudi kwa viumbe visivyo na akili; kama ambavyo ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na hakuna kitu chochote ila kinamtakasa kwa sifa zake” (17: 44). Lengo la kutaja wanyama na Malaika, baada ya kutaja vilivyo katika mbingu na ardhi, ni ubainifu wa kuchanganya aina zote za viumbe. Yametangulia maelezo yake katika Juz. 13 (13:13-25).
Wanamhofia Mola wao aliye juu yao na wanafanya wanayoamriwa.
Aya hii inafahamisha waziwazi kwamba mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu humhofia na hutii amri yake na makatazo yake, na inafahamisha katika madhumuni yake kwamba mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu kisha akadai kuwa anamwamini na anamhofia, basi huyo ni mwongo katika madai yake.
وَقَالَ اللَّهُ لَا تَتَّخِذُوا إِلَٰهَيْنِ اثْنَيْنِ ۖ إِنَّمَا هُوَ إِلَٰهٌ وَاحِدٌ ۖ فَإِيَّايَ فَارْهَبُونِ {51}
وَلَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَهُ الدِّينُ وَاصِبًا ۚ أَفَغَيْرَ اللَّهِ تَتَّقُونَ {52}
وَمَا بِكُمْ مِنْ نِعْمَةٍ فَمِنَ اللَّهِ ۖ ثُمَّ إِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فَإِلَيْهِ تَجْأَرُونَ {53}
ثُمَّ إِذَا كَشَفَ الضُّرَّ عَنْكُمْ إِذَا فَرِيقٌ مِنْكُمْ بِرَبِّهِمْ يُشْرِكُونَ {54}
لِيَكْفُرُوا بِمَا آتَيْنَاهُمْ ۚ فَتَمَتَّعُوا ۖ فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ {55}
- 1. Katika Kiswahili hakuna wingi wa kulia wala kushoto, lakini kwenye kiarabu uko-Mtarjumu.