Aya 8-20: Wanafiki
Kwanza Mwenyezi Mungu amewataja waumini, hao ni ambao wameifanyia ikhlas haki kwa ndani na nje. Kisha akawataja makafiri ambao wamefanya ukafiri ndani na nje.
Hivi sasa imekuja zamu ya wanafiki ambao wamedhihirisha Imani na kumbe sio waumini; kufuru ya hawa ni chafu zaidi ya ukafiri na ameichukia zaidi Mwenyezi Mungu; ndio maana Mwenyezi Mungu amewataja sana katika Aya kumi na tatu, wakati ambapo amefupiliza kuwataja makafiri katika Aya mbili tu.
Si hivyo tu, bali hata ameteremsha Sura maalum ya wanafiki. Aya hizi ziko wazi kabisa hazihitaji taawili wala ufafanuzi; ni kama Aya inayosema:
فَإِنَّ اللَّهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا {54}
Kwa hivyotutatoshekanamaelezohaya yanayofuatia:-
Ni Nani Mnafiki?
Kila mmoja wetu anataka awe anatajika katika watu; angalau watu wasimpinge katika mambo yake wala wasimtusi; hasa ikiwa maisha yake na kazi yake inategemea watu watakavyomwamini.
Kwa hivyo basi mtu wa namna hii siku zote anakuwa na shaka hata kama halikutokea jambo la kumtilia shaka, ijapokuwa kuna kawaida ya kuchukulia usahihi juu ya kitendo cha Mwislamu.1
Kwa vyovyote iwavyo kila anayewaficha watu, na kujidhihirisha na mambo asiyokuwa nayo na akaogopa siri isifichuke, basi huyo ni mwongo, mnafiki, mwenye kujionyesha na mwenye hadaa; hata kama atapata kuaminiwa na watu wote, bali huko kuaminiwa kunazidisha kosa lake na ni balaa mbele za Mwenyezi Mungu na pia ni balaa mbele za watu siku siri ikifichuka.
Unaweza kuuliza, kama watu wakiitakidi kuwa kitu fulani ni haramu na mtu mwengine akaitakidi kati yake na Mwenyezi Mungu kuwa ni halali, akawa anakifanya kwa kujificha kwa kuogopa maneno ya watu je, atahisabiwa ni mnafiki? Je, ni wajibu awabainishie watu yale anayoitakidi? Je atakuwa ana lawama kama akinyamazia makosa yao?
Jibu: Hakuna ubaya wowote wa kufanya lile ambalo mtu anaitakidi kuwa ni halali; wala hawezi kuhesabiwa kuwa ni katika wanafiki maadamu roho yake imetulia.
Kwa sababu taklifa ya jambo hasa inafungamana na yeye sio watu, bali hata anasamehewa katika makosa. Kwani hakuna dhambi katika kufanya jambo kwa makosa bila ya kukusudia.
Ama kubainisha uhakika ni wajibu kwake kwa upande wa kuamrisha mema na kukataza mabaya; kwa sababu kosa liko katika hukumu sio katika maudhui.2
Aya tulizonazo zinazungumzia wanafiki ambao iliwathibitikia hoja na haki ya Utume wa Muhammad (s.a.w.) lakini waling’ang’ania upinzani tu kwa inadi, kama ilivyokuwa kwa washirikina ambao walifanya inadi na wakapigana vita. Tofauti iliyopo kati ya washirikina na wanafiki, ni kwamba washirikina walitangaza upinzani wao na wakasema wazi:
“Hatuifuati haki kwa sababu mafukara wameifuata” Qur’an inasema:
قَالُوا أَنُؤْمِنُ لَكَ وَاتَّبَعَكَ الْأَرْذَلُونَ {111}
Ama wanafiki wao waliikataa haki kwa sababu moja au nyingine lakini wao walifanya upinzani wakadhihirisha Uislamu kwa woga na hadaa, wakawa ni wabaya zaidi kuliko makafiri. Kwani makafiri udhahiri wao na undani wao ulikuwa sawa tu, kama vile mlevi anavyokunywa pombe njiani. Lakini wanafiki walificha yale yaliyo katika dhamira zao kama mwovu anayevaa nguo za watakatifu.
Hadaa hiyo inafahamisha kuwa mnafiki hana kizuizi chochote cha dini au akili, wala cha haki au uadilifu; dhamiri yake haishtuki maadamu yuko mbali na macho ya watu. Basi mtu wa namna hii ni vigumu sana kurudia kwenye heri.
Kwa hivyo ndio Mwenyezi Mungu amewataja wanafiki katika Aya hizi kwa sifa ya hadaa, kughafilika, maradhi ya moyo na upumbavu. Vile vile kughurika, kufuata matamanio, uchafu na kuendelea na upotevu.
Watu wanawaita kwa jina la wapelelezi, vibaraka waharibifu na wenye kujionyesha.
Watu hao wapo hivi sasa; kama walivokuwa wakati wa Mtume na kabla yake, na wataendelea katika vizazi vijavyo. Lakini ni wenye kulaaniwa popote walipo, hata wakiwa makaburini mwao. Kama wakifaulu basi ni kwa muda. Ama kufaulu kwa wakweli kunaendelea.
Ibara nzuri niliyoisoma kuhusu wanafiki ni kauli ya Muhyiddini maarufu kwa jina la Ibnul Arabi katika Juzuu ya nne ya kitabu Futuhatil- Makkiyyah.
“Ni uzuri uliyoje wa aliyoyasema Mwenyezi Mungu: ‘Wanawastahi watu’, ambao wana maumbile ya kusahau. ‘Na wala hawamstahi Mwenyezi Mungu’ ambaye hapotei wala hasahau, afadhali wangelifanya kinyume.”
Maana ya ibara hiyo ni kwamba lau mnafiki angelikuwa anafikiria vizuri na akawa anafikiria kidogo na kuwa na akili, angelificha makosa yake kwa Mwenyezi Mungu - kama inawezekana - sio kwa watu. Kwa sababu watu hawawezi kumnufaisha wala kumdhuru. Ambaye ananufaisha na kudhuru ni Yeye (Mungu) peke yake.
Kwani watu wanasahau uovu wanaouona; watamzungumzia mwenye uovu huo wakati fulani tu baadaye wanasahau na kunyamaza, kama vile hakukutokea kitu chochote. Tumeona wengi waliofanya madhambi makubwa makubwa yakawafedhehesha mpaka mtu akajificha kutokana na ubaya wa vitendo vyake, halafu baadaye mtu akajitokeza kwa watu, wakakaa naye, wakaamiliana naye kama mtu mwema.
Tena pengine wakamtegemea na kumpa cheo kikubwa hata kuweza kusimamia mambo matakatifu ya kidini ambayo hakuyasimamia yeyote isipokuwa Mtume au wasii wake.
Mbali ya kuwa watu husahau pia wanasifu na kutusi kulingana na matakwa yao na matamanio. Kwa hiyo, mwenye akili atamwogopa Mwenyezi Mungu wala hataogopa watu, bali atajichunga yeye mwenyewe na kujiepusha na yale anayoyaonea haya. Na hakuna mtu mwoga kama yule anayefanya kwa siri yale anayoyaonea haya kuyafanya dhahiri.
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِنْ قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ {21}
الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنْزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّهِ أَنْدَادًا وَأَنْتُمْ تَعْلَمُونَ {22}
- 1. Maulama wa kifqh wana kawaida waliyoiita kuchukulia usahihi kitendo cha Mwislamu. Kwa mfano umemwona mtu anakunywa maji na hujui ni ya halali au haramu; au ulijua kuwa ni haramu, ukatia shaka je, anakunywa kwa ajili ya dawa au hajui kama ni haramu au anakunywa tu bila ya udhuru wowote? Basi ni lazima uchukulie usawa tu, mpaka idhihiri kinyume.
- 2. Ukimwona mtu anakula nyama ya nguruwe na yeye anajua kuwa ni nyama ya nguruwe, lakini hajui hukumu yake ya haramu, basi yakupasa umwongoze kwenye hukumu ya Mwenyezi Mungu. Hali hiyo ndiyo inayoitwa kutojua hukumu. Ama akiwa anajua hukumu, lakini anaitakidi kwamba nyama hii anayoila ni nyama ya kondoo lakini kumbe ni nguruwe, sio wajibu juu yako kumbainishia, kwa sababu yeye ana udhuru. W a kwanza huitwa asiyejua hukumu na wa pili huitwa asiyejuwa maudhui.