Aya 97-100: Anayemfanyia Uadui Jibril
Lugha
Imesemekana kuwa maana ya neno Jibril ni mja wa Mungu (Abdullah) na Mikail ni mja mdogo wa Mwenyezi Mungu (Ubaidullah)
Maana
Sema: Anayemfanyia uadui Jibril basi yeye ni kafiri, laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake.”
Wamekubaliana wafasiri kwamba ababu ya kushuka Aya hii ni Mayahudi walimuuliza Mtume (s.a.w.) kuhusu Malaika anayemteremshia wahyi. Akawajibu: “Ni Jibril.” Wakasema” “Ah! Huyo ni adui yetu, kwa sababu yeye huleta shida na vita na Mikail huleta amani na raha: lau angelikuwa Mikail ndiye anayekuletea wahyi tungelimwamini.”
Wameufanya ushindani kwa dhahiri, kwanza kwenye ukabila wa Muhammad (s.a.w.) kwamba wahyi ushuke kwa mmoja wa Waisrail. Mwenyezi Mungu na Mtume wake alipowashinda kwa hoja, wakabadilisha ushindani kwa Jibril sio Muhammad tena. Hakika ilivyo hasa - kama tulivyoelezea mwanzo - sio sababu ya Uarabu na Uyahudi au Jibril na Muhammad bali ni maslahi yao tu; ni uasherati, ulevi, riba na utapeli. Na wao wanafanya unafiki na kuficha uwongo wao.
Kwa hivyo kwa upande wa malumbano na kuwapa hoja, Mwenyezi Mungu alisema:
Hakika yeye ameiteremsha Qur’an moyoni mwako kwa idhini ya Mwenyezi Mungu inayosadikisha yale yaliyokuwa kabla yake:
Yaani uadui wenu kwa Jibril hauna msingi, kwa sababu yeye ni mpelekaji wahyi tu, kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kwa Muhammad. Na wahyi huo unasadikisha yaliyo katika Tawrat yenu, miongoni mwa sifa za Muhammad na bishara kwa wanaoamini. Kwa hivyo uadui wenu kwa Jibril ni uadui kwa Mwenyezi Mungu, wahyi, Tawrat, uongozi wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe vyake na bishara kwa waumini.
Hakika tumekuteremshia hoja zilizo wazi na hawazikatai ila mafasiki
Yaani yaliyomjia Muhammad (s.a.w.) hayana shaka baada ya kuwa na hoja na dalili, na wala hayakanushi isipokuwa mwenye kukufuru Mwenyezi Mungu; mwenye kuipinga haki. Makusudio ya ufasiki hapa ni ufasiki wa itikadi yaani ukafiri sio ufasiki wa vitendo ambao unatendwa na mtu anapokuwa na imani.
Je, Kila mara wanapofunga ahadi, kikundi katika wao huitupa?
Ahadi walizozitupa Mayahudi na kuzivunja ni nyingi; Kama ya kumwamini Muhammad, ya kuacha kuwasaidia makafiri, ya kuwaamini Mitume na kutowaua na kutomwabudu yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, n.k. kwa hiyo wakamkadhibisha Muhammad na wakawasaidia washirikina, walio maadui wao na wa Muhammad. Vile vile huko nyuma waliwakadhibisha Mitume wakawa tayari kumsulubu Masih, na waliabudu ndama na mengine mengi.
Bali wengi katika wao hawaamini.
Yaani kuna kundi lililoabudu ndama na lililowaua Mitume, n.k; na wengi wao ingawaje hawakufanya hivyo, lakini bado ni makafiri, waovu. Kwa ufupi ni kwamba asiyekuwa na haki anaweza kudai haki, na mwenye makosa anaweza kudai kuwa hana makosa.
Wanayaweza hayo kwa mbinu za kusema. Lakini mara moja wanafedheheka zinapowashinda hoja na dalili ambazo hawawezi kuzikimbia; kama walivyofedheheka Mayahudi katika uwongo wao na madai yao kuwa wanafanya kama vile alivyoteremsha wahyi Mwenyezi Mungu.
Kuishi kwa amani na kumwamini mwenyezi mungu
Wenye kulingania amani wanakusudia kuwa watamaliza tofauti za wanaozozana kwa mikutano. Lakini tumejifunza kuwa mazungumzo ya amani na haja ya kuwa na amani, hayawezi kufaa kitu kwa watu wenye kuangalia manufaa yao.
Wenye tamaa hawawezi kuacha tamaa zao isipokuwa kwa njia ya vikwazo na vitisho. Maisha ya amani yanahitaji akili iliyofunguka na tabia njema. Ni tabia gani tukufu itakayokuwa mbele za mtu asiyeamini isipokuwa maada, ulanguzi na kutaka utajiri wa haraka haraka? Na ni hoja gani zitakazomkinaisha mwenye tamaa?
Inasemekana kwamba mataifa mawili makubwa ya Mashariki na Magharibi yanadai amani kati yao, lakini wakati huo huo kila mmoja anajitengeneza silaha za hali ya juu na kujikinga kwa kumhofia mwenzake. Kwa hivyo amani wanayodai ni ya maneno na wala si ya vitendo.
Maumbile ya kiakili yanathibitisha kwamba kila taifa lina haki kamili katika kujiamulia mambo yake haliwezi kuingiliwa. Sasa je ni nani anayefuata misingi hii?
Amani na haki haiwezi kupatikana kwa ukamilifu mpaka pande zote zinazohusika ziamini haki kwa njia ya haki. Ni muhali kuongoka kwenye heri na kutarajia heri yule asiyamini chochote isip-okuwa dhati yake na yule asiyejishughulisha na lolote zaidi ya manufaa.
وَلَمَّا جَاءَهُمْ رَسُولٌ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ مُصَدِّقٌ لِمَا مَعَهُمْ نَبَذَ فَرِيقٌ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ كِتَابَ اللَّهِ وَرَاءَ ظُهُورِهِمْ كَأَنَّهُمْ لَا يَعْلَمُونَ {101}