read

Aya 104: Kuamrisha Mema

Makusuido ya heri hapa ni uislamu, na mema ni kumtii Mwenyezi Mungu, na maovu ni kumwasi. Maana yanayopatikana ni kwamba hapana budi kupatikane kundi la watu litakalowalingania wasiokuwa waislamu kwenye uislamu; kwenye lile linalomridhisha Mwenyezi Mungu, analolilipa thawabu na kuacha lile linalomkasirisha analoliletea adhabu.

Tamko kutokana na nyinyi katika Aya hii inafahamisha wajibu wa kuamrisha mema kwa njia ya kutosheana (kifaya). Yaani, wakilisimamia hilo baadhi, utakuwa wajibu umewaondokea wengine. Wala si lazima kuwa mwenye kutekeleza umuhimu huu, awe mwadilifu. Hapana, si hivyo, kwa sababu mbili:

1. Kwamba sharti ya hukumu ni sawa na hukumu yenyewe, haithibiti ila kwa dalili wala hakuna dalili ya sharti ya uadilifu hapa; si kutoka katika Qur'an, Hadith au kutoka katika akili.

2. Hukumu ya kuamrisha mema haitegemei maasi au utiifu wa mwengine katika hukumu.

Mafakihi wengi wameshartisha wajibu wa kuamrisha mema kuwa mwenye kuamrisha awe atakuwa salama, kiasi ambacho hatapata madhara yoyote kwa kuamrisha mema na kukataza maovu.

Lakini sharti hili haliingi sehemu zote, kwani, kupigana na anayetupiga kwa ajili ya dini yetu na nchi yetu ni wajibu, ingawaje tunafahamu kwamba, kwa kawaida kupigana huleta madhara.

Inafaa kwa kila mtu kuyatoa mhanga maisha yake, akiwa na yakini kwamba kujitoa mhanga huku kuna maslahi ya umma. Faida ya watu na nchi ni muhimu na adhimu zaidi kuliko maisha yake, bali hilo linashukuriwa mbele ya Mwenyezi Mungu na kwa watu. Kuna Hadith isemayo: "Jihadi bora zaidi ni tamko la haki mbele za Sultan dhalimu."

Kwa ufupi ni wajibu kukinga madhara yakiwa hayatakuwa na faida yoyote. Vyenginevyo, itajuzu kuyavumilia; kama inavyojuzu kwa mtu kukata kiungo kibovu katika viungo vyake kwa kupigania uhai wake na kuhofia kumalizika.

Zaidi ya hayo, mifumo ina athari zake. Baadhi ya mifumo inaifukuza haki na kumsababishia mtu matatizo. Na mingine inalazimisha fikra kwa msikilizaji bila ya kujitambua. Mwenye akili na hekima anafanya kulingana na hali ilivyo ya taratibu au ya nguvu.

Firaun alikuwa na ukomo wa Usultani na kupetuka mipaka; Musa na Harun hawakuwa hata na msaidizi, lakini pamoja na hayo waliamrishwa kumlingania kwenye haki. Lakini kwa njia ya upole. Hata Muumba wa ulimwengu, (ambaye limetukuka neno lake) mara nyingine amewaambia waja wake kwa vitisho na kusema: "Hakika nyinyi hamtanusuriwa nasi." (23:65) Mara nyingine hutumia upole na kusema: "Je, hampendi Mwenyezi Mungu awasamehe na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe Mwenye kurehemu." (24:22)

Kwa ujumla kutangaza mwito wa uislamu kwa watu, na waislamu kuamrishana mema na kukatazana mabaya, ni katika nguzo za uislamu. Kwa hiyo kunawajibisha kuwapo kwa kikundi kitakachosimamia umuhimu huu, sawa na kulazimika kuwapo uongozi utakaosimamia amani na nidhamu, wafanya kazi wa viwandani, wakulima na wengineo ambao wanachangia maisha.

Huu ni msingi wa kila dini, kila dhehebu na kila fikra. Kwa sababu, hiyo ndiyo njia nzuri ya kueneza mwito, kupata ushindi na kuwazuia maadui. Angalia jinsi watu wa siasa na uchumi wanavyotilia umuhimu vyombo vya habari, kuvikuza na kuvitolea mamilioni ya mapesa na kufanya mizinga na habari kuwa bega kwa bega.
Hawakufanya hivyo ila ni kwamba wametambua, kutokana na uzowefu wao, kwamba habari ni silaha yenye nguvu kuliko mizinga na mabomu. Mmoja wa wakuu wa mapatano alisema baada ya kufaulu kwao katika vita vya ulimwengu: "Tumeshinda katika vita kwa mabomu ya karatasi."

Yaani magazeti Unaweza kuuliza, kwamba unawezaje kuziunganisha Aya hizi mbili: "Na wawepo katika nyinyi watu wanaolingania kwenye heri na wanaoamrisha mema na kukataza maovu." Na Aya isemayo: "Enyi mlioamini! Jiangalieni nafsi zenu hatawadhuru aliyepotea ikiwa mmeongoka." (5:105) Ambapo ya kwanza imefahamisha wajibu wa kuamrisha mema na ya pili imefahamisha kutokuwepo wajibu huo kutokana na neno "Jiangalieni nafsi zenu."

Jibu: Makusudio ya Aya ya pili, ni kwamba mwenye kutekeleza wajibu wa kuamrisha mema na kukataza mabaya, hatadhuriwa na upotevu wa aliyepotea wala upinzani wa mpinzani, maadamu yeye anaetekeleza wajibu wake tu, "Hakika ni juu yako kufikisha tu, na juu yetu ni kuhisabu." (13:40)

Swali la pili: kuna Hadith mashuhuri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) isemayo: "Mwenye kuona katika nyinyi uovu, na auondoe kwa mkono wake, akishindwa, basi (auondoa) kwa ulimi wake, akishindwa basi ni kwa moyo wake na hilo ni katika udhaifu zaidi wa imani."

Mpangilio huu unapingana na ilivyo desturi ya sharia, kiakili na kimazoweya; kwamba kuondoa uovu kunaanzia kwa ulimi halafu ndio vita. Sasa kuna wajihi gani wa kauli hii ya Mtume?

Jibu: Kuna tofauti kubwa sana baina ya kuondoa uovu na kukataza uovu, kwani kukataza uovu aghlabu ni kabla ya kutokea uovu wenyewe; ni kama vile kukinga, kama kuona kuwa mtu fulani anafikiria kuiba, ukamkataza kufanya wizi huo.

Ama kuondoa uovu, kunakuwa baada ya kutokea uovu wenyewe. Kwa mfano umejua kuwa mtu fulani ameiba mfuko wa mtu mwengine, hapo ukiwa unaweza kumnyang'anya na kumrudushia mwenyewe, basi ni wajibu kwako kulifanya hilo wewe mwenyewe, ikiwa kuna uwezekano wa kumyang'anya mwizi; na wewe usiweze kupata madhara.

Kama hukuweza ni wajibu kwako kumwamrisha mwizi aurudishe kwa mwenyewe na kumkataza kuuzuwia. Kama utashindwa na vishindo vya mwizi, basi usikiridhie kitendo chake - baina yako na Mola wako. Kwa hivyo maudhui ya Hadith ni kugeuza uovu, si kukataza uovu.1

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ ۚ وَأُولَٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ {105}

Wala msiwe kama wale waliofarakana wakahitalifiana baada ya kuwajia wao dalili zilizo wazi; na hao ndio wenye adhabu kubwa.

يَوْمَ تَبْيَضُّ وُجُوهٌ وَتَسْوَدُّ وُجُوهٌ ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ اسْوَدَّتْ وُجُوهُهُمْ أَكَفَرْتُمْ بَعْدَ إِيمَانِكُمْ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنْتُمْ تَكْفُرُونَ {106}

Siku ambayo nyuso zitang'aa na nyuso (nyingine) zitasawijika. Na ama ambao nyuso zao zitasawijika, (wataambiwa): Je mlikufuru baada ya kuamini kwenu? Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyakanusha.

وَأَمَّا الَّذِينَ ابْيَضَّتْ وُجُوهُهُمْ فَفِي رَحْمَةِ اللَّهِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {107}

Na ama ambao nyuso zao zitang'aa, watakuwa katika rehema ya Mwenyezi Mungu. Wao humo watadumu.

تِلْكَ آيَاتُ اللَّهِ نَتْلُوهَا عَلَيْكَ بِالْحَقِّ ۗ وَمَا اللَّهُ يُرِيدُ ظُلْمًا لِلْعَالَمِينَ {108}

Hizo ni Aya za Mwenyezi Mungu, tunakusomea wewe kwa haki; na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu viumbe.

وَلِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۚ وَإِلَى اللَّهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ {109}

Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo ardhini na vilivyomo mbinguni; na kwa Mwenyezi Mungu hurejezwa mambo yote.
  • 1. Imeelezwa katika Tafsir Al-Manar kwamba Sheikh Muhammad Abduh alipokuwa akifasiri Aya hii katika darsa, miongoni mwa aliyoyasema ni: "Ni juu ya kila mtu kuamrisha mema kiasi cha uwezo wake."Akatoa mfano wa shia kuwa wao wanashikamana na msingi huu, wala hawaiachi fursa yoyote inapopatikana. Akatoa ushahidi wa hilo kuwa alipokuwa Beirut alihitajia mnyonyeshaji kwa ajili ya mtoto wake wa kike. Akaletewa mwanamke wa Kishia. Huyu mwanamke akawa anawalingania wake wa Sheikh kwenye madhehebu yake.