Aya 121: Vita Vya Uhud.
Aya hii na nyingine kadhaa zinazofuatia zilishuka kuhusu tukio la vita vya Uhud ambalo kwa ufupi ni kama ifuatavyo: Uhud ni jina la mlima ulioko Madina. Vita vya Uhud vilikuwa mnamo mwezi wa
Shawwal (Mfungo mosi) mwaka wa tatu wa Hijra.
Baada ya kuuawa magwiji wa Kikuraish katika vita vya Badr, Abu Sufian alipata nafasi na akawa ndiye Rais wa Makuraish. Akawa anampangia njama Mtume (s.a.w.) pamoja na washirikina, akaweza kukusanya jeshi la wapiganaji elfu tatu. Akaenda nalo hadi karibu na mlima Uhud. Na alikuwa yuko pamoja na mkewe Hind bint Utba (mamie Muawiya).
Mtume (s.a.w) naye akatoka na wapiganaji elfu moja, lakini Abdallah bin Ubayya, kiongozi wa wanafiki alitaka kuwavunja nguvu watu kwa kujitoa, wakamwitikia watu mia tatu; Mtume akabaki na mia saba. Abdallah bin Amr (baba wa Jabir Al-ansari) alijaribu kumzuia bin ubayya na azma yake hiyo, lakini hakufaulu.
Na koo mbili za Ansari zikajaribu kumfuata bin Ubayya, lakini Mwenyezi Mungu akawahifadhi na wakathibiti pamoja na Mtume (s.a.w). Wao walikuwa Bani Salama katika Khazraj na Bani Haritha katika Aus.
“Mtume (s.a.w) akapanga mbinu ya mapigano. Akaweka wapiga mishale hamsini kwenye mlima nyuma ya jeshi la waislamu waliokuwa wakiongozwa na Abdallah bin Jubair, akawaambia, "nyinyi mtatuhami kwa upande wa nyuma, wala msion- doke hapo mlipo tukishinda au tukishindwa."
Vita vilipochacha, Hind akawaongoza wanawake kupiga ngoma nyuma ya wanaume ili kuwachochea huku akiimba: Mkikabili tutawakumbatia na mazulia kuwatandikia, Na mkigeuka tutawakimbia mapenzi hatutawapati Mtume (s.a.w.w) alipomsikia akasema:
Ewe Mwenyezi Mungu kwako nategemea na kwa ajili yako ninapigana. Tosha yangu ni Mwenyezi Mungu na bora ya mwenye kutegemewa ni Yeye Bendera ya Makuraish ilibebwa na Twalha bin Abu Twalha Al-Abdi kutoka ukoo wa Abdu Ddar, Imam Ali akamuua, bendera ikachukuliwa na Said bin Abu Twalha, akauawa na bendera ikaanguka, akaichukua Musafi bin Abu Twalha naye akauawa na Imam, mpaka wakauawa watu tisa katika ukoo wa Abdu Ddar. Wakavunjiliwa mbali washirikina na kushindwa. Waislamu wakawa wanaokota ngawira.
Wapiga mishale walipoona kushindwa kwa washirikina na ndugu zao waislamu wanakusanya ngawira, waliondoka pale walipowekwa na Mtume (s.a.w). Kiongozi wao Abdallah bin Jubair akawaambia: "Bakini sehemu zenu, mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake." Lakini walikataa na wakaenda kunyakua ngawira. Jubair akabaki na watu kumi tu.
Khalid bin Al-Walid kuona hivyo aliwafuatia na kikosi cha washirikina. Wakawamaliza baada ya kupigana nao kiume.
Makuraish walipoona alivyofanya Khalid waliwazingira Waislamu na kuwashambulia mpaka wakamfikia Mtume (s.a.w). Akapigwa jiwe na washirikina likamjeruhi jicho, uso wake ukarowa damu, akajeruhiwa mdomoni na vishikio viwili vya kofia ya chuma vikamwingia usoni.
Hapo waislamu wakaanza kukimbia baada ya mtu mmoja kupiga kelele kuwa Muhammad ameuawa. Hakuna aliyebakia isipokuwa watu wachache wakion- gozwa na Ali bin Abu Talib, Abu Dujana na Suheli bin Hanif wakipigana kiume kumkinga Mtume.
Hind akumuhadaa Wahshi amuue Muhammad au Ali au Hamza. Akamuua Hamza kwa mkuki wake. Hind akalipasua tumbo la Hamza akamtoa ini lake akalila. Tangu siku hiyo alibandikwa jina la 'Mla maini.' Katika vita hivyo waliuawa washirikina 22 na Waislamu 70 walikufa shahid.
Maana
Na uliporauka kutoka kwa ahli zako kwenda kuwaandalia waumini mahali pa kupigana.
Yaani, kumbuka ewe Mtume uliporauka kutoka nyumbani kwako kwenda kupanga sehemu watakayokaa wapiga mishale, wapanda farasi na waumini wengine uliokuwa nao.
إِذْ هَمَّتْ طَائِفَتَانِ مِنْكُمْ أَنْ تَفْشَلَا وَاللَّهُ وَلِيُّهُمَا ۗ وَعَلَى اللَّهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ {122}