Aya 190-195: Mwenyezi Mungu Na Wenye Akili
Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kutofautiana usiku na mchana, ziko ishara kwa wenye akili.
Tulionyesha dalili za kutosha za kiakili juu ya kuweko Mwenyezi Mungu (s.w.t.) wakati wa kutafsiri Aya ya 22 na 164 ya Sura Baqara. Nayo iko katika maana ya Aya hii tuliyo nayo. Kwa vile hapa ni mahali pake, tutarudia kuyaeleza maudhui hayo kwa ufupi na kwa namna nyingine.
Njia nzuri ya kumjua Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni njia ambayo anaitolea dalili Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu kuweko kwake. Kwa ufupi ni kuangalia mwenye akili kwenye ulimwengu na kufikiria kwa undani maajabu Yake na siri iliyomo ya mipangilio na maajabu kadhaa.
Utaona kuwa kila kilichopo kinafahamisha makusudio na malengo, kwa kuwekwa mahali panaponasibiana na kuwa katika mpangilio wa ulimwengu na mwendo wa maisha.
Kutokana na misingi hii miwili (hisia na akili), inapelekea kabisa kujua sababu ya kwanza inayosifika na uhai, elimu, uweza na hekima ya hali ya juu. Nimewasikia watu wengi wakisema kuwa watu wote, hata walahidi, wanakubali kuwa iko sababu ya kwanza, isipokuwa waumini huiita Mwenyezi Mungu na wengine huiita maada au nguvu asili, kwa hiyo tofauti iko katika majina tu.
Lakini hilo ni kosa kubwa na ni kuleta shubha. Kwa sababu waumini wanaamini kuweko sababu hiyo, inayothibitishwa na akili sio kwa hisia, na kwamba sababu hiyo inasifika kwa sifa ya ujuzi, uweza, hekima na uadilifu. Ama wengine wanasema kuwa inaonekana kwa macho na kuguswa kwa mkono na kwamba hiyo ni kipofu na kiziwi. Kwa hiyo tofauti ya kauli mbili hizo ni mbali zaidi ya mbingu na ardhi.
Ambao humtaja Mwenyezi Mungu katika hali ya kusimama na kukaa na kulala na wanafikiria umbo la mbingu na ardhi. Mola wetu hukuviumba hivi bure, utukufu ni wako; basi utuepushe na adhabu ya moto.
Makusudio ya kusimama, kukaa na kulala kwa ubavu ni kwamba wao wako katika twa'a ya Mwenyezi Mungu wakati wowote. Makusudio ya kufikiria umbo la mbingu na ardhi ni kuwa wanamkubali Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Ama kumyenyekea Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutaka kinga na adhabu ya moto, ni dalili ya uchaji Mungu na imani.
Arrazi anasema: "Aina za kuabudu ni tatu: Kusadikisha kwa moyo, kuthibitisha kwa ulimi na kutenda kwa viungo."
Kwa hiyo kauli yake Mwenyezi Mungu 'wanamtaja Mwenyezi Mungu' inaonyesha ibada ya ulimi, 'katika hali ya kusimama kukaa na kulala kwa ubavu' inaonyesha ibada ya viungo, na kauli yake, na 'hufikiria umbo la mbingu na ardhi;' inaonyesha ibada ya moyo na fikra na roho.
Na mtu ni mkusanyiko wa hivi vitu vitatu. Kama ulimi utazama kabisa katika dhikri (utajo), viungo vikawa vinatenda na akili ikazama katika kufikiria, basi hapo ndipo atakuwa ameingia katika ibada kwa mwili wake wote."
Hakuna mwenye shaka kwamba kumtaja Mwenyezi Mungu, kumwamini na kumwabudu ni vizuri, lakini vizuri zaidi ya kumtaja kwa ulimi, kusimama usiku, kuswali na kufunga mchana, ni kufanya kazi kwa ajili ya watu na kujitolea katika maslahi ya umma.
Na kila atakayetaka matukufu kutoka kwa Mwenyezi Mungu bila ya kujitoa mhanga huku, pamoja na kuwa na uwezo, basi atakuwa anatafuta kuthaminiwa bila ya thamani.
Kwa mnasaba wa kauli yake Mwenyezi Mungu. 'Mola wetu hukuviumba hivi bure' tutaonyesha kauli za Sunni wanaosema kuwa haifai kuleta sababu ya vitendo vya Mwenyezi Mungu kwa kuwa na makusudio au lengo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu hapaswi na jambo lolote wala hakuna ubaya kwake wa kitu chochote. (Al- Mawafiq J. 8 uk. 202)
Sheikh Abu Zuhra katika kitab Madhahibul Islamiyya, anasema; "Wamesema Ashaira. Yaani sunni, kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameumba vitu si kwa sababu yoyote."
Shia wanasema kuwa vitendo vyote vya Mwenyezi Mungu Mtukufu vina sababu ya maslahi ya watu au ya utaratibu wa ulimwengu, kwa kuwa yeye ni mjuzi mwenye hekima. Wakatoa dalili ya Aya hii. "Mola wetu hukuviumba hivi bure."
Pia inawezekana kuwajibu Sunni kwa kauli yao na vitendo vyao wala sio kwa Aya au riwaya. Kwamba wao wanafanya makisio na kuchukulia uzuri na maslahi yanayosababisha upole wa Mwenyezi Mungu katika kuwaangalia viumbe na kutengeneza vizuri hali zao, katika maisha yao ya duniani na akhera. Pia wanachukua asili ya hukumu za kisharia ya Mwenyezi Mungu kwa kukisia na kuonelea kuwa ni vizuri.
Vilevile wametunga vitabu mahsusi katika kubainisha hekima ya Mwenyezi Mungu katika maamrisho yake na makatazo yake. Maana ya hayo yote ni kuwa Yeye Mwenyezi Mungu haamrishi wala hakatazi isipokuwa kwa lengo sahihi na sababu yenye hekima.
Mola wetu! Hakika Wewe ambaye utamwingiza motoni, basi utakuwa umemfedhehesha.
Na sisi tunakutii kwa kutaka radhi Zako na kuepuka fedheha hii. Hivi ndivyo anavyokuwa mumini, anaweka mbele thawabu za Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Kwa hiyo anatii kwa kuogopa adhabu na kutumaini thawabu. Imamu Ali (a.s) amesema: akiwasifu Waumini: "Wao na pepo ni kama walioiona wakiwa humo wanastarehe. Na wao na moto ni kama waliuona wakiwa ndani yake wanaadhibiwa.” Ama anayemwabudu Mwenyezi Mungu kwa dhati yake tu, sio kwa kutumaini pepo Yake au kuogopa moto wake, huyo ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mwanafun- zi wake Imam Ali."
Na hawatakuwepo wasaidizi kwa ajili ya madhalimu.
Kila msaidizi wa batili katika dunia hii na ambaye ana haki za watu, basi yeye ni dhalimu, na itakapofika Siku ya haki na uadilifu hatakuwa na msaidizi. Mawaidha fasaha kabisa katika maudhui haya ni khutba ya Mtume alipohisi kukaribia mauti alisema: "Enyi watu ambaye nimemchapa mgongoni mwake, huu hapa mgongo wangu, na ambaye nimemchukulia mali yake hii hapa mali yangu, na achukue wala asiogope kumwekea nongwa.
Kwani hiyo siyo hulka yangu. Isipokuwa nawataka mchukue haki zenu tu kama ziko kwangu, au kisasi ili nikutane na Mola wangu nikiwa na nafsi njema." Maelezo zaidi yako katika tafsir ya Aya 160 ya Sura hii kifungu cha 'Muhammad na hulka njema.'
Mola wetu hakika sisi tumesikia mwenye kulingania anayelingania kwenye imani kwamba muaminini Mola wenu, nasi tukaamini.
Hii ndio hali ya kila mwenye kuitafuta haki kwa njia ya haki anaufungua moyo wake kwa mwito wa haki na anaikubali mara tu anapoisikia kutoka kwa yoyote; sikwambii akiwa ni bwana na Mitume na mwisho wa Mitume.
Akawakubalia Mola wao kwamba mimi sitapoteza amali ya mfanya amali miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke.
Yanayozingatiwa ni matendo, sio nasaba ya mtendaji au kabila yake, wala si kwa jinsia yake, awe mwanamume au mwanamke. Wote ni sawa katika uislamu. Huu ni uthibitisho wa haki ya mwanamke na utukufu wake. Ni nyinyi kwa nyinyi mwanamume ni baba wa mwanamke na mwanamke ni mama wa mwanamume, na kila mmoja ni kaka wa mwengine na mume wa mwengine; wote wanatokana na asili moja; wote mnatokana na Adam na Adam anatokana na mchanga. Kuna Hadith isemayo: "Wanawake ni ndugu baba mmoja mama mmoja wa wanaume." Yamekwishatangulia maelezo zaidi katika tafsir ya (2:228).
Basi wale waliohama na wakafukuzwa katika majumba yao na wakaudhiwa katika njia yangu na wakapigana na wakauawa, bila shaka nitawafutia makosa yao na nitawaingiza katika mabustani ambayo hupita mito chini yake. Ndiyo malipo yanayotoka kwa Mwenyezi Mungu na kwake Mwenyezi Mungu kuna malipo mema.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuyafungamanisha malipo na matendo mema na wala sio kwa jinsia, amebainisha kuwa matendo ambayo yatapata nyongeza ya thawabu ni kama haya yafuatayo.
1. Kutoka mumini kwa hiyari yake katika mji wake ambao hawezi kusimamisha dini kwenda mji mwengine anaoweza kufanya hivyo. Kwa sababu ya Aya hii na Aya isemayo "Hakika Malaika watawaambia wale ambao wamewafisha hali ya kuwa wamezidhulumu nafsi zao: Mlikuwa katika hali gani? Watasema: “Tulikuwa wanyonge katika ardhi." Watawaambia: Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa pana mkaweza kugura humo. Hao makazi yao ni jahannam, nayo ni marejeo mabaya kabisa." (4:97)
Kwa sababu ya Aya mbili hizo, mafakihi wametoa fatwa ya kuharamisha kukaa mtu mnyonge katika mji wa kikafiri ambao hawezi kutekeleza faradhi na nembo za Kiislamu, wakawajibisha kwake kuhamia mji wa waislamu ili kuweza kutekeleza yale yaliyo wajibu kwake isipokuwa kama atashindwa kuhama.
Jambo la kusikitisha siku hizi ni kuhusu vijana wetu wa Kiislamu wenye uwezo, wanakazania kwenda Amerika na Ulaya, si kwa jengine ila kwa kufuata ufuska, zinaa na ulevi.
2. Kutolewa waumini kwa nguvu majumbani mwao, kama washirikina wa Kiquraish walivyowafanyia wale waliomwamini Muhammad (s.a.w.) na kama walivyofanya waisrail kwa wapalestina.
3. Kuudhiwa katika njia ya haki. Hakuna yeyote anayeifuata ila ataudhiwa. Imeelezwa katika Hadith kwamba mtu hujaribiwa kwa kiasi cha dini yake. Ikiwa katika dini yake ni nzito basi huzidi mitihani na ikiwa ni nyepesi basi pia atajaribiwa kwa kiasi chake. Wala hakuna kitu kikubwa zaidi kwa malipo mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko kuvumilia maudhi kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu na kuwa na subira. "Ewe Mwenyezi Mungu tujaalie katika wenye kuvumilia.
4. Kujitoa mhanga katika njia ya haki. Wote hawa Mwenyezi Mungu atawafutia maovu yao na zaidi ya hayo atawapa thawabu itakayofanana na utukufu wake na cheo chake.
Kukaririka neno malipo na utukufu ni kuonyesha kuwa malipo yake hayana mfano, kama ambavyo utukufu wake hauna mfano.
لَا يَغُرَّنَّكَ تَقَلُّبُ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي الْبِلَادِ {196}
مَتَاعٌ قَلِيلٌ ثُمَّ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۚ وَبِئْسَ الْمِهَادُ {197}
لَٰكِنِ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ لَهُمْ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا نُزُلًا مِنْ عِنْدِ اللَّهِ ۗ وَمَا عِنْدَ اللَّهِ خَيْرٌ لِلْأَبْرَارِ {198}