Aya 179: Kupambanua Wema Na Uovu
Maana
Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwaacha waumini juu ya hali mliyonayo mpaka awapambanue wabaya na wazuri.
Maadui wa Mtume (s.a.w.) walikuwa aina mbili: Kwanza ni washirikina, nao ni wale walioukataa uislamu kwa ndani na nje, wakatangaza vita tangu mwanzo wakaishia kuunda vikundi,wakajiandaa kwa nguvu wanazoziweza. Wakawa ni maadui wanaojulikana wazi wakitofautika na waislamu.
Aina ya pili ni wanafiki, nao ni wale walioficha ukafiri na uadui kwa Mtume na sahaba zake, wakadhihirisha mapenzi. Kazi yao ilikuwa ni njama dhidi ya Mtume (s.a.w.) ndani ya safu za waislamu mara wanawababaisha watu kwa uongo, mara nyingine wanawavuta waislamu kwenye maasi, au kuwavunja nguvu za kupambana na adui na kuwatia hofu. Na katika baadhi ya vita walikuwa pamoja na jeshi la waislamu, kisha wakajitoa njiani.
Wanafiki walimsumbua sana Mtume kuliko alivyosumbuliwa na washirikina. Kwa sababu, washirikina walikuwa maadui wanaoonekana wazi, lakini wanafiki walikuwa wakifanya vitimbi kwa kujificha na kuleta madhara kichinichini. Na hivyo ndivyo walivyo kwa yeyote anayelingania kheri, wakati wowote na mahali popote. Wanajaribu kuchafua katika safu za watu wazuri. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ame- wataja katika Aya nyingi, kama vile Aya ya 173 ya Sura hii, na katika Aya hii tuliyonayo na pia katika Aya isemayo: "Na namna hii tumefanyia kila Nabii adui, mashetani katika watu wa majini. Baadhi yao wanawafunulia wengine maneno ya kuwapamba pamba kwa kuwahadaa." (6:112)
Mtume aliamrishwa kuwafanyia hao wanafiki na kila aliyetamka shahada muamala wa kiislamu. Kuhifadhia damu zao na mali zao, kushirikiana nao katika vita na hata katika ngawira. Kwa sababu uislamu ulikuwa bado ni mchanga, lau atawaua au kuwafukuza wangelisema wakuzaji mambo kwamba Muhammad hampendi anayemwamini na asiyemwamini. Na washirikina wangelifanya hilo ni njia ya kuu- tangazia vibaya uislamu na Mtume wake.
Kwa sababu hiyo Mtume akawa hana la kufanya. Akiwakubali wataharibu na kuwaweka mbali waislamu na jihad, na akiwakataa alihofia mlinganio wake usipungukiwe na wasaidizi na wafuasi. Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii: "Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwaacha waumini…" Yaani sio hekima ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwaacha katika hali hiyo, wanafiki wajifiche kwenye pazia la kudai Uislamu. La sivyo hivyo, bali anawafichua ili wajulikane na wafedheheshwe mbele ya watu na wasibakiwe na pa kutolea vitimbi na ufisadi. Na jambo la kuwafedhehesha sio kutamka shahada, kurukuu na kusujudu, na mambo mengine ambayo ni mepesi kuyafanya. La! Bali ni jambo zito ambalo litawafichua wanafiki na wasibakie na nafasi yoyote ya ria na hadaa au vitimbi na kutia sumu.
Kwa mtihani huu mzito na amri ya kuwa na subira na kuwa na uthabiti katika vita vya Uhud, mtajua enyi waumini neema ya Mwenyezi Mungu kwenu na kwamba Yeye hakuwaacha katika hali mliyokua nayo, ya kuchanganyikana na maadui ambao mlitosheka nao hapo mwanzo kwa jina la uislamu. Makusudio ya wazuri ni waumini na wabaya ni wanafiki.
Na hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwafunulia mambo ya ghaibu.
Yaani si katika hekima yake Mwenyezi Mungu Mtukufu wala si katika desturi Yake kuwafahamisha watu elimu Yake na awaambie hili ni zuri na hili ni baya; bali ni juu yenu kuyafahamu hayo kupitia majaribio ya shida na misukosuko, kama ilivyotokea Uhud wakati Mtume (s.a.w.) alipowaita maswahaba warudi kwa adui mara ya pili katika Hamraul Asad. Yaani Mwenyezi Mungu hamfahamishi yeyote yaliyo katika nyoyo za watu kuwa ni imani au unafiki, isipokuwa kuwaamrisha kujitoa mhanga kwa hali na mali, na kwenye utekelezaji ndipo anajulikana mwenye kujitiatia na mwenyewe hasa.
Ndio, Mwenyezi Mungu anawafichulia baadhi ya Mitume yake juu ya unafiki wa huyu na imani ya yule, kwa hekima ambayo yeye mwenyewe Mungu anaijua zaidi. Haya ndiyo maana ya kauli yake.
Lakini Mwenyezi Mungu huchagua katika Mitume yake amtakaye.
Kauli hiyo inafanana na kauli yake Mwenyezi Mungu isemayo: "Mjuzi wa ghaibu, wala hamdhihirishi ghaibu Yake yeyote isipokuwa Mtume aliyemridhia." (72:26-27)
وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّهُ مِنْ فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَهُمْ ۖ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَهُمْ ۖ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُوا بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ وَلِلَّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ {180}
لَقَدْ سَمِعَ اللَّهُ قَوْلَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّهَ فَقِيرٌ وَنَحْنُ أَغْنِيَاءُ ۘ سَنَكْتُبُ مَا قَالُوا وَقَتْلَهُمُ الْأَنْبِيَاءَ بِغَيْرِ حَقٍّ وَنَقُولُ ذُوقُوا عَذَابَ الْحَرِيقِ {181}
ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيكُمْ وَأَنَّ اللَّهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِلْعَبِيدِ {182}