Aya 188-189: Kusifiwa Kwa Wasiyoyafanya
Maana
Furaha si haramu. Ni nani asiyefurahi akipata jambo la kheri au kuokoka na shari? Bali kufurahi kwa ajili ya kheri ya watu inaonyesha ukweli wa nia na furaha njema.
Mtume (s.a.w.) alifurahi kwa sababu ya kuwasili binamu yake Jafer bin Abu Talib kutoka Uhabeshi, akambusu na akasema: "Sijui ni jambo gani kati ya mawili litakalomshinda mwenzake kwa furaha, ni kwa kuwasili Jafar au kwa kuiteka Khaibar?!"
Furaha isiyotakikana ni ile iliyo na msukumo wa mifundo, kufurahia matatizo ya wengine na majivuno, au kufurahi mtu kwa sababu amenyang'anya, akaua au kufanya ufisadi bila ya kuadhibiwa au kulaumiwa, au kufurahi kwa sababu ya kufanya hila na hadaa ili asifiwe na sifa asizokuwa nazo, na mengineyo ambayo tunayashuhudia huku na huko.
Baada ya utangulizi huu tunaelezea kwa ufupi kauli zinazohusu Aya hii:
Usiwadhanie kabisa wale ambao wanafurahia mambo waliyoyafanya na wakapenda kusifiwa kwa wasiyoyafanya, usiwadhanie kabisa kuwa wataokoka na adhabu, na wana wao adhabu iumizayo.
Yasemekana kuwa Aya hii ilishuka kwa wanavyuoni wa Kiyahudi ambao walificha jina la Muhammad na sifa zake zinazopatikana katika Tawrat, na wakati huo huo wanapenda wasifiwe kuwa ni wa kweli, na kwamba wao wako kwenye mila ya Ibrahim (a.s.)
Na ikasemekana kuwa ilishuka kwa ajili ya wanafiki, waliokuwa wakihepa kuungana na Mtume (s.a.w.) katika vita kwa kutoa sababu za uongo na Mtume alikuwa akionyesha kuwakubalia. Hilo liliwafurahisha sana na kupenda kusifiwa kwa wasiyoamini.
Kauli yenye nguvu ni kuwa baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwataja wale waliochukua ahadi kuwa wasifiche haki, na wakaitupa ahadi, ndipo akawataja katika Aya hii kwamba wao wamefurahi kwa tendo lao hilo wakapenda kusifiwa kuwa ni wa kweli na wenye haki, na hali wao wako mbali nayo kabisa.
Kadiri watakavyoendelea katika upotevu wao hawatatoka katika mamlaka ya Mwenyezi Mungu na uwezo wake, wala hawataokoka na adhabu yake. Vipi isiwe hivyo. "Na ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni mwenye uweza juu ya kila kitu."
Kwa tafsir hii wanaingia katika Aya hii Mayahudi na Manasara walioficha yanayomhusu Muhammad (s.a.w.) na wanafiki katika Waislamu walioficha ukafiri na kudhihirisha imani.
Unaweza kuuliza, kwa nini Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema, 'usiwadhanie' baada ya kwisha kusema usiwadhanie ambao…'
Jibu: imekaririka hapa kwa sababu ya kuondoa mikanganyo baada ya maneno marefu. Matumizi haya yameenea siku hizi katika maandishi na idhaa.
Swali la pili: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema: "Usiwadhanie kuwa wataokoka na adhabu." Na kisha akasema: "Na wana wao adhabu iumizayo." Pamoja na kuwa jumla ya kwanza inaitoshelezea ya pili.
Jibu: hapa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anatofautisha kati ya jumla mbili, kwa sababu ya kwanza imefahamisha kwamba wao si wenye kuokoka na adhabu bila ya kubainisha adhabu yenyewe kama ni hafifu au ni kali, ndipo akabainisha katika jumla ya pili kuwa ni katika aina ya adhabu iumizayo. Kama vile kusema: "Nakupenda tena nakupenda sana.'
إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِأُولِي الْأَلْبَابِ {190}
الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ {191}
رَبَّنَا إِنَّكَ مَنْ تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنْصَارٍ {192}
رَبَّنَا إِنَّنَا سَمِعْنَا مُنَادِيًا يُنَادِي لِلْإِيمَانِ أَنْ آمِنُوا بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا ۚ رَبَّنَا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَكَفِّرْ عَنَّا سَيِّئَاتِنَا وَتَوَفَّنَا مَعَ الْأَبْرَارِ {193}
رَبَّنَا وَآتِنَا مَا وَعَدْتَنَا عَلَىٰ رُسُلِكَ وَلَا تُخْزِنَا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ إِنَّكَ لَا تُخْلِفُ الْمِيعَادَ {194}
فَاسْتَجَابَ لَهُمْ رَبُّهُمْ أَنِّي لَا أُضِيعُ عَمَلَ عَامِلٍ مِنْكُمْ مِنْ ذَكَرٍ أَوْ أُنْثَىٰ ۖ بَعْضُكُمْ مِنْ بَعْضٍ ۖ فَالَّذِينَ هَاجَرُوا وَأُخْرِجُوا مِنْ دِيَارِهِمْ وَأُوذُوا فِي سَبِيلِي وَقَاتَلُوا وَقُتِلُوا لَأُكَفِّرَنَّ عَنْهُمْ سَيِّئَاتِهِمْ وَلَأُدْخِلَنَّهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ثَوَابًا مِنْ عِنْدِ اللَّهِ ۗ وَاللَّهُ عِنْدَهُ حُسْنُ الثَّوَابِ {195}