read

Waliokufuru Na Wenye Taqwa Aya 196-198

Maana

Maana ya matamshi ya Aya zote tatu yako wazi. La muhimu ni kubainisha makusudio kwa ujumla. Wafasiri wengi wamesema kuwa kafiri anaishi maisha ya hapa duniani kwa raha, lakini mwisho wake huko akhera ni balaa na mashaka. Na mu'min anaishi kwa mashaka na dhiki, na mwisho wake ni mzuri. Na kwamba "Dunia ni jela ya mu'min na ni pepo ya kafiri."

Tulivyofahamu sisi kutokana na Aya hizi ni kwamba zimeeleza tofauti baina ya wale walioathirika na dunia yao kuliko dini yao, na wala wasifanye kazi yoyote isipokuwa kwa maslahi yao ya kibinafsi, kama vile mayahudi na wanaofanana nao, na wale ambao wameitanguliza dini yao kuliko dunia yao kwa hali yoyote itakayokuwa.

Kundi la kwanza Mwenyezi Mungu ameliita makafiri kwa sababu wao wanaikufuru haki wala hawaipi uzito wowote. La pili ameliita wanaomcha Mwenyezi Mungu, kwa sababu linajiepusha na machukivu yake na maasia yake. Hakuna mwenye shaka kwamba mtu anayefanya tendo lolote kwa ajili ya dunia, akaipa kipaumbile na akahalalisha ya haramu kwa ajili ya dunia, basi takataka zote zitamwangukia, kama tunavyoshuhudia. Kinyume na mwenye kufanya zuhudi katika haramu na akathirika na njaa na kujinyima.
Makusudio ya kuzunguka zunguka katika miji ni kupata kwao neema za dunia. Huenda wakadhani kwamba dhahiri ya neema na starehe za wabatilifu ni kheri kwao, na kwamba dhahiri ya kujinyima kwa watu wa haki ni shari. Ndipo Mwenyezi Mungu akaiondoa dhana hii, kwamba ni kinyume cha hivyo. Kwa sababu neema ya wabatilifu ni starehe chache, kisha waingie katika Jahannam ambayo ni marejeo mabaya. Na kwamba shida ya wenye haki itaondoka, kisha itakuja neema ya milele na raha ya daima.

وَإِنَّ مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ لَمَنْ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَمَا أُنْزِلَ إِلَيْكُمْ وَمَا أُنْزِلَ إِلَيْهِمْ خَاشِعِينَ لِلَّهِ لَا يَشْتَرُونَ بِآيَاتِ اللَّهِ ثَمَنًا قَلِيلًا ۗ أُولَٰئِكَ لَهُمْ أَجْرُهُمْ عِنْدَ رَبِّهِمْ ۗ إِنَّ اللَّهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ {199}

Na hakika miongoni mwa watu wa Kitabu wako wanaomwamini Mwenyezi Mungu na yaliyoteremshwa kwenu na yaliyoteremshwa kwao, kwa kumnyenyekea Mwenyezi Mungu. Hawaziuzi Aya za Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo. Hao wana ujira wao kwa Mola wao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ {200}

Enyi ambao mmeamini! Fanyeni subira na mvumilie na muwe imara na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu.