Aya 156-158: Msiwe Kama Wale Waliokufuru
Maana
Enyi mlioamini msiwe kama wale waliokufuru.
Tamko la ambao wamekufuru, ni la kiujumla, linamkusanya kila kafiri; awe mnafiki au kafiri wa wazi wazi, bali wafasiri wengi wamesema; makusudio hasa ni wanafiki.
Na wakawasema ndugu zao.
Yaani: walisema waliyoyasema kwa ajili ya ndugu zao waliokufa.
Waliposafiri katika nchi au walipokuwa vitani; lau wangelikuwa kwetu wasingelikufa na wasingeliuawa.
Wanafiki walikuwa wakiyategemeza mauti ya msafiri kwenye safari na yule mwenye kuuawa vitani kwenye vita hivyo, sio kwa kuwa yameandikwa na Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu amewakataza waumini kusema mfano wa maneno haya. Kwa sababu ndani yake mna kuitikia mwito wa hadaa za wanafiki na matamanio yao. Ikiwa hawatayasema hayo na kuyategemeza mauti ya anayekufa safarini au vitani kwa Mwenyezi Mungu, basi watakuwa wamevipinga vitimbi vya wanafiki kwao wenyewe na kuwapatisha hasara. Makusudio ya udugu hapa ni kiujumla, yaani ndugu wa nasaba au kushabihiana katika itikadi na tabia.
Ili Mwenyezi Mungu ayafanye hayo kuwa majuto katika nyoyo zao.
Yaani, Mwenyezi Mungu amewakataza waumini kujifananisha na wanafiki kwa kauli na vitendo. Kwa sababu kujifananisha huku kunawafurahisha na kunathibitisha makusudio yao. Na kukosa kufanya hivyo kunawasumbua na kuwakasirisha.
Na Mwenyezi Mungu anahuisha na kufisha.
Ajali zote ziko kwenye uwezo wake, wala si kwa sababu ya vita au safari. Kwani anaweza kusalimika na yule aliyekaa mjini akafa. Hili ndilo jibu la kauli ya wanafi- ki, kuwa safari na vita vinasababisha mauti.
Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.
Hili ni himizo la kumtii Mwenyezi Mungu na ni tishio la anayewaiga makafiri na wanafiki kwa kauli na vitendo.
Na kama mkiuliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu au mkifa basi maghufira na rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko yale wanayoyakusanya.
Kila mwenye kuipigania haki au nafsi yake kwa upanga wake au kalamu yake au ulimi wake na akauawa, basi ameuawa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Vilevile kupigania maisha na elimu au chochote kinachowafaa watu na akafa, basi amekufa katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Na kila mwenye kufa au kuuawa, katika njia ya Mwenyezi Mungu amewajibikiwa kusamehewa dhambi na kupanda daraja katika dunia na akhera.
Kauli yake Mwenyezi Mungu ni bora kuliko yale wanayoyakusanya ni kwamba lililo bora kwa mumini ni kuathirika na linalodumu kuliko linaloisha ambalo ni starehe na anasa.
Na kama mkifa au mkiuawa, nyote mtakusanywa kwa Mwenyezi Mungu.
Huu ndio mwisho wa binadamu awe amefariki dunia kwa kuuawa au kwa sababu yoyote ile. Hapo ndipo penye malipo ya (matendo) yaliyopita, ikiwa kheri basi ni kheri na ikiwa ni shari basi ni shari. Mwenye akili anajiandaa na siku hii wala hawezi kufanya mchezo.
بِمَا رَحْمَةٍ مِنَ اللَّهِ لِنْتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنْتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانْفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ ۖ فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمْ وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ ۖ فَإِذَا عَزَمْتَ فَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُتَوَكِّلِينَ {159}
إِنْ يَنْصُرْكُمُ اللَّهُ فَلَا غَالِبَ لَكُمْ ۖ وَإِنْ يَخْذُلْكُمْ فَمَنْ ذَا الَّذِي يَنْصُرُكُمْ مِنْ بَعْدِهِ ۗ وَعَلَى اللَّهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ {160}