Aya 11 – 12: Fungu La Mwanamume Ni Sawa Na Mara Mbili Ya Mwanamke.
Maana
Wakati wa ujahiliya, sababu za kurithi zilikuwa ni tatu;
1. Nasaba, lakini kwa wanaume tu, wanaoweza kushika silaha na kupigana. Ama wanawake na wanaume dhaifu hawakuwa na urithi. Lakini uislam ukaeneza urithi kwa wote.
2. Mtoto wa kupanga; yaani mtu kumfanya mtoto wa mwengine kuwa mwanawe hasa katika urithi na mengineyo. Uislam umelikataa hilo kwa kauli yake Mwenyezi Mungu: "Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa wana wenu hasa …" (33:4)
3. Kuliana yaamini; yaani mtu kumwambia mwenzake: "Damu yangu ni yako, utanirithi na nitakurithi."
Huu ulikubaliwa na uislam kwa ufafanuzi huu ufuatao: Mwanzo ilikuwa aliyehama (Muhajiri) pamoja na Mtume (s.a.w.) kutoka Makka kwenda Madina akimrithi mwenzake aliyehama (Muhajir) ikiwa wana urafiki wa pamoja; na ilikuwa Muhajir anarithiwa na Muhajir tu, na si mwengine hata kama yuko karibu. Vile vile baada ya Mtume kuwafungisha undugu Sahaba zake walikuwa kama ndugu wawili wanaorithiana.
Lakini baadaye uislam uliyafuta haya mawili (kuhama na kufungishwa undugu) Kwa Aya isemayo; "… Na ndugu wa tumbo wana haki zaidi wao kwa wao katika kitabu cha Mwenyezi Mungu…" (8:75) Vile vile katika (33:6)
Kwa hiyo wajibu wa kurithi katika uislam, umethibiti juu ya mambo mawili: Nasaba na sababu . Na sababu ni mambo mawili Ndoa na usimamizi Utakuja ubainifu kulingana na mpango wa Aya.
Ufuatao ni ufafanuzi wa matamko ya Aya mbili tulizonazo ambazo hizo pamoja na zinazofuatia zinazofungamana na urithi ni ufafanuzi wa aliyoyajumlisha Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kauli yake iliiyotangulia: "Wanaume wana fungu…"
1. Mwenyezi Mungu anawausia kwa watoto wenu; fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili.
Akiwa marehemu ameacha watoto wa kiume na wa kike, wa kiume watapata sawa na sehemu ya wanawake wawili. Ikiwa wako wengine katika mirathi; kama vile mume au mke, baba au mama, au baba na mama.
Kila mmoja atachukua fungu lake - kama tutakavyofafanua - na sehemu itakayobaki watapewa watoto wa kike na wa kiume; ambapo wa kike watachukua nusu ya watakayopata wa kiume. Hiyo ni kwa kuafikiana madhehebu zote za kiislam.
Vilevile yameafikiana madhehebu yote kwamba, marehemu akiacha mtoto wa kiume na wajukuu, basi mtoto wa kiume atawazuia wajukuu kurithi; ni sawa wajukuu wawe wa kike au wa kiume.
Yametofautia madhehebu ikiwa ataacha mtoto wa kike mmoja, wawili au zaidi bila ya kuacha mtoto wa kiume. Madhehebu mane yamesema kuwa mtoto wa kike mmoja atachukua nusu tu; wawili au zaidi watachukua theluthi mbili tu; kitaka- chobaki watapewa wengine.
Shia Imamia wamesema kuwa mali yote ni ya mtoto wa kike akiwa mmoja au zaidi, wengineo hawana chao. Kwa Ufafanuzi zaidi rejea kitabu chetu Ahwalush- shakhsiya Alal-madhahibil Khamsa.
2. Na wakiwa ni wanawake zaidi ya wawili, basi watapata theluthi mbili za alichokiacha (marehemu). Na akiwa ni mmoja, basi atapata nusu.
Mwenye Majmaul-bayan amesema: "Dhahiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kwamba watoto wa kike waw-ili hawastahiki theluthi mbili, isipokuwa zaidi ya wawili lakini Umma umesema kwa pamoja kuwa hukumu ya wawili ni sawa na ya zaidi ya wawili."
Na hivi ndivyo sahihi hasa, na kila sababu au taawili zozote zinazoelezwa kuhusu zaidi ya wawili ni za kukisia tu.
Hata hivyo hilo si muhimu, la muhimu zaidi ni kubainisha tofauti za madhehebu ya kiislam kuhusu mirathi ya watoto wa kike ikiwa marehemu hakuacha wa kiume. Kwa kauli moja mafakihi wameafikiana kuwa marehemu akiwa ameacha mtoto wa kike mmoja, atapata nusu kuwa ni fungu lake. Wakiwa ni wawili na zaidi watachukua theluthi mbili. Lakini wamehitalifiana kuhusu nusu itakayobaki baada ya kupewa binti mmoja na theluthi itakayobaki baada ya kupewa mabinti wawili, ipewe nani?
Sunni wamesema, itapewa kaka wa marehemu kwa kutegemea riwaya ya Taus kutoka kwa Ibn Abbas naye kutoka kwa Mtume (s.a.w.) kwamba yeye amesema: "Yaambatanisheni mafungu na watu wake na kinachobakia ni cha asaba waume." Shia wameikanusha Hadith ya Taus; kwa sababu yeye ni mwongo mno 1. Na wamesema kuwa nusu ya pili itarudishwa kwa binti kwa hiyo atachukua mali yote. Kwa maana ya kuwa atachukua nusu kama fungu lake na nusu ya pili kwa kurud- ishiwa. Vile vile wakiwa wawili na zaidi watachukua theluthi iliyobaki.
Dalili yao Shia ni kuwa Qur'an imefaradhisha theluthi mbili kwa wawili, na zaidi ya nusu kwa bint mmoja. Kwa hiyo hapana budi kuweko na mtu atakayechukua sehemu iliyobaki; na Qur'an haikumweleza mtu huyo. Ndio maana kukazuka kutofautiana. Kwa hivyo basi ikawa hakuna kilichosalia isipokuwa Aya hii: Na ndugu wa tumbo wanahaki zaidi wao kwa wao. (8:75) na (33:6) Ambapo inafahamisha kuwa aliye karibu zaidi ndiye anayestahiki kuliko mwengine. Hakuna mwenye shaka kwamba binti yuko karibu zaidi ya kaka.
Zaidi ya hayo sio Shia peke yao waliosema kuwa mali yote ni ya binti mmoja au zaidi, bali Hanafi na Hambal pia wamesema kuwa marehemu akiacha binti mmoja au zaidi na asipatikane yeyote mwenye fungu au asaba basi mali yote ni ya binti, inagawaje Aya inasema: "… basi watapata theluthi mbili za (mali) aliyoiacha, laki- ni akiwa ni mmoja basi atapata nusu…"
Ikiwa Aya hii haimzuwii mtoto wa kike kuchukua mali yote katika namna waliy- oielezea Hanafi na Hambal, basi vile vile haiwezi kumzuia kwa namna nyingine. Kwa sababu dalili ya Aya ni moja haiwezi kugawanyika kwa namna yoyote ile.
Vile vile Hanafi na Hambal wamesema: Ikiwa marehemu ataacha mama bila ya mwengine yeyote mwenye fungu na asaba, basi mama atachukua mali yote. Thelutuhi ikiwa ni fungu lake na theluthi mbili kurudishiwa yeye, ingawaje Aya inasema: "… basi mama yake atachukua theluthi …" Ikiwa inawezekana kwa mama kuchukua mali yote ingawaje fungu lake ni theluthi, basi hata mtoto wa kike pia atachukua yote inagawaje fungu lake ni nusu au theluthi mbili.
Haya tumeyaeleza kwa ufafanuzi zaidi katika kitabu Ahwalush-shakhsiyya Ala madhahibil-khamsa, Na pia katika Juzuu ya sita ya Fiqh Imam Jafar As-Sadiq (as).
Na Baraza kuu la waislam la Misr limetoa kitabu kikubwa kiitwacho Daw'atu-taqrib ambacho ndani yake mna utafiti kamili wa suala hili. Yale tuliyoyanakili ya Hanafi na Hambali yametoka katika kitabu Mughni cha Ibn Quddam na Mizani Shi'rani katika mlango wa Faraidh.
3. Na wazazi wake wawili kila mmoja wao atapata sudusi ya alichokiacha akiwa anaye mtoto.
Neno Walad (mtoto) linatumika kwa mtoto wa kike na kiume. Kwa sababu neno hilo linaotakana na Wilada (kuzaa), ambako kunaweza kuwa kwa wa kike na wa kiume. Na Qur'an imelitumia neno hilo kwa maana hayo pale iliposema: "Mwenyezi Mungu anausia kwa watoto wenu; mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili." Au pale iliposema: "Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwa na mtoto …" (19:35)
Makusudio ya wazazi wawili hapa ni baba na mama tu, haingii babu na bibi (nyanya). Ikiwa marehemu ameacha wazazi wawili na watoto, itaangaliwa: Ikiwa katika watoto yuko wa kiume wazazi watachukua sudusi2 kila mmoja, kinachobaki ni cha watoto hata ikiwa mtoto wa kiume ni mmoja tu. Ikiwa hakuna wa kiume, na wa kike wakawa zaidi ya mmoja, basi wazazi watachukua theluthi, na theluthi mbili zitakuwa ni za watoto wa kike. Hilo wameafikiana waislam wote.
Ikiwa mtoto wa kike ni mmoja tu pamoja na wazazi wawili, basi wazazi wawili kila mmoja atachukua sudusi na mtoto fungu lake ni nusu.
Hapo itabaki sudusi ambayo Sunni wanasema itarudishwa kwa baba tu. Ama Shia wanasema itarudishwa kwa baba, mama na mtoto ikiwa mama hana kizuizi (kwa kuwepo ndugu wa marehemu); waitagawa mali mafungu matano moja la baba, moja la mama na matatu ya binti.
Ikiwa mama atazuilika kwa kuwepo ndugu, basi ziada itarudishwa kwa baba na binti kwa mafungu manne, yaani ziada itagawanywa mafungu manne moja la baba na matatu ya binti.
4. Akiwa hana mtoto na akarithiwa na wazazi wake wawili; basi mama yake atapata theluthi. Akiwa anao ndugu, basi mama yake atapata sudusi.
Ikiwa marehemu hana mtoto wala mjukuu ikawa mirathi yake inakwenda kwa babake na mamake tu, basi mama atachukua theluthi ikiwa marehemu hana ndugu watakaomzuia mama kilichozidi sudusi. Ikiwa wapo hao ndugu, basi mama atachukua sudusi tu, kinachobaki katika hali zote mbili ni cha baba.
Madhehebu yametofautiana kuhusu idadi ya ndugu ambao watamzuia mama. Maliki wamesema, uchache wake ni kaka wawili na si kina dada. Hanafi Shafii na Hambali wamesema ni kaka wawili au dada wawili.
Shia wanasema ni kaka wawili au mmoja na dada wawili; au dada wanne kwa sharti ya kuwa wawe ni ndugu wa marehemu baba mmoja mama mmoja au baba mmoja, na wawe wamekwisha zaliwa wakati wa kufa mrithiwa, sio kwenye mimba na pia baba awe hai. Hawa ndio ndugu wanaomzuwiya mama kurithi theluthi, lakini wao wenyewe hawarithi kitu wakati huo.
5. Baada ya kutoa alivyousia au kulipa deni.
Marehemu akiacha mali, kwanza itatumiwa katika mazishi yake (sanda na mahali pa kuzikwa). Kisha yatalipwa madeni yake ikiwemo Hijja, Zaka, Khums na nadhiri, kisha utatekelezwa wasia wake usiozidi theluthi ya mali. Baada ya hapo ndipo utaangaliwa urathi ambao ni kama kutoa kilichozidi haja.
Unaweza kuuliza: Ikiwa deni limetangulia wasia, mbona halikutangulia kutajwa katika Aya hii?
Jibu: Kutangalia huko kutajwa hakumaanishi kutangulia katika hukumu na utekelezaji. Kwa sababu kuunganisha kwa 'au' hakumaanishi kufuata mpango - kama ilivyo kinahau - isipokuwa kunamaanisha usawa katika hukmu. Ni kama vile kusema lianze lipi baada ya mazishi? Jibu litatokana na kupatikana dalili nyingine. Imethibiti kutoka kwa Mtume (s.a.w.) na Ijmai kwamba hakuna wasia wala mirathi isipokuwa baada ya kulipwa deni; na pia kuna Hadith nyingi zinazofahamisha kuwa marehemu ni rehani wa madeni yake.
6. Baba zenu na wa watoto wenu, hamjui ni yupi katika wao aliye karibu zaidi kwa manufaa. Ni faradhi itokayo kwa Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.
Hii ni jumla iliyoingia kati inayoonyesha kuwa siri ya makadirio ya mirathi haiwezi kufahamika kiakili isipokuwa anayeijua ni yule aliyemuumba mwanadamu; Yeye peke yake ndiye ajuaye linalomdhuru mtu na kumnufaisha.
Aya hii inafaa kuwa ni dalili kwamba hukumu za Mwenyezi Mungu zimewekwa kwa masilahi ya mtu na utengeneo wake. Kwa hivyo basi tunapata dalili ya imani ya mtu kwa matendo yake mema na tunapata dalili ya uovu wake kwa matendo yake maovu.
Ni faradhi itokayo kwa Mwenyezi Mungu sio kutoka kwa mtu ambaye anatawaliwa na matamanio. Tumeona tume nyingi za kutunga sheria na mabunge yakiweka sheria na kanuni kwa ajili ya masilahi ya wenye nguvu na kuwaonea wanyonge.
7. Nanyi mtapata nusu ya walichokiacha wake zenu, ikiwa hawana watoto. Ikiwa wana watoto basi mtapata robo ya walichokiacha baada ya kutoa walivyousia au kulipa deni.
Waislam wote wameafikiana kuwa mke na mume wanashiriki katika mirathi na warithi wote. Mume atapata nusu ikiwa mke hana mtoto aliyezaa naye au aliyezaa na mume mwengine. Na mke atapata robo ikiwa ana mtoto aliyezaa naye au aliyezaa na mke mwengine.
8. Na wao watapata robo ya mlichokiacha ikiwa hamna mtoto. Ikiwa mna mtoto, basi watapata thumni3 ya mlichokiacha baada ya kutoa mliyou- sia au kulipa deni.
Mke atapata robo ya mali ya mumewe ikiwa hana mtoto aliyezaa naye au aliyezaa na mke mwengine, na atapata thumuni ikiwa ana mtoto aliyezaa naye au aliyezaa na mwengine.
Madhehebu mane yameafikiana kuwa makusudio ya mtoto (Walad) hapa ni mtoto wa marehemu na mjukuu aliyezaliwa na mtoto wa kiume tu, awe mume au mke. Ama mjukuu aliyezaliwa na mtoto wa kike hawezi kumzuia mke au mume kupata fungu lake kubwa. Bali Shafi na Maliki wamesema kuwa mjukuu wa mtoto wa kike harithi wala hamzuwii mwengine, kwa sababu yeye ni upande wa kukeni (fungu la rihami).
Shia Imamia wamesema kuwa makusudio ya mtoto ni mtoto yeyote na mjukuu yeyote wa mtoto wa kike au wa mtoto wa kiume. Kwa hiyo mjukuu wa kike wa mtoto wa kike atawazuilia mke na mume kupata fungu kubwa na pia atarithi. Wake wakiwa wengi watashirikiana katika robo au thumni kwa kugawana sawa sawa.
Madhehebu mane yamesema: "Ikiwa marehemu hana mrithi zaidi ya mumewe au mkewe, basi kinachobaki hakirudishwi kwa mume huyo wala mke - Taz. Kitabu Mughni cha Ibn Quddama, Shia Imamia wametofautiana katika hilo kwa kauli tatu:
1. Kurudishwa kinachobaki kwa mume tu, sio kwa mke. Kauli hii ndiyo maarufu kwa mafaqihi wa siku hizi na ndivyo wanavyofanya.
2. Kurudishiwa mke au mume katika hali zote.
3. Kurudishiwa mke au mume wakati wa kughibu Imam mwadilifu. Na sisi tuko kwenye rai hii ambayo pia ni rai ya Sheikh Saduq, Najibuddin bin Said, Allama Hilly na Shahidi wa kwanza. Tumetaja dalili za kuchagua rai hii katika kitab Fiqhul-Imam Jafar As-Sadiq (A.S.) .
9. Ikiwa mwanamume au mwanamke anayerithiwa ni mkiwa naye ana ndugu wa kiume au wa kike, basi kila mmoja katika wao atapata sudusi. Wakiwa wengi zaidi ya hivyo, basi watashirikiana katika theluthi.
Neno Kalala (ukiwa, kutokuwa na baba wala mtoto) limekuja mara mbili katika Qur'an, moja ikiwa hapa na jengine mwisho wa Sura hii. Makusudio yake hapa ni ndugu wasiokuwa baba na mama au mtoto. Neno hilo anaitwa nalo marehemu anayerithiwa na ndugu wa kiume au wa kike walio hai kama ambavyo anaitwa nalo mrithi ndugu wa kiume au wa kike aliye hai. Maana zote mbili - kama uzionavyo - zinafuatana. Kwa hiyo yoyote utakayoichukua ni sawa.
Wafasiri wameafikiana kuwa makusudio ya ndugu wa kiume au wa kike katika Aya hii ni ndugu wa upande wa kwa mama tu; bali hata wengine wamesoma Qiraa cha minalummi (wa upande wa mama). Ama mirathi ya ndugu wa kiume au wa kike kwa baba na mama au kwa baba tu, hukumu yake itakuja katika Aya iliyoko mwisho wa sura hii.
Madhehebu yameafikiana kwamba mmoja katika ndugu (mtoto wa mama) atapata sudusi awe mwanamume au mwanamke. Wakiwa ni zaidi,wawe wa kike au wa kiume au mchanganyiko watapata theluthi kwa kugawana sawa sawa, mwanamke sawa na mwanamume.
10. Baada ya (kutoa) yaliyousiwa au kulipa deni pasi na kuleta dhara.
Yametangulia maelezo kuwa hakuna mirathi ila baada ya kulipwa deni na kutekelezwa wasia. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekataza kuleta dhara katika deni na wasia. Dhara katika deni ni kukiri au kuusia deni lisilokuwepo kwa kukusudia kuwadhuru warithi.
Na dhara katika wasia ni kuzidisha kiwango cha theluthi ya mali yake. Kama akifanya hivyo utekelezaji wake utategemea ruhusa ya warithi. Hadith inasema: "Kuwaacha warithi wako wakiwa wanaojitosheleza ni bora kuliko kuwaacha hali ya kuwa ni mafukara omba omba."
Ni wasia utokao kwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni mjuzi mpole.
Kila anachousia Mwenyezi Mungu ni wajibu kitekelezwe.
تِلْكَ حُدُودُ اللَّهِ ۚ وَمَنْ يُطِعِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ {13}
وَمَنْ يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُ يُدْخِلْهُ نَارًا خَالِدًا فِيهَا وَلَهُ عَذَابٌ مُهِينٌ {14}
- 1. Sayyid Mohsin Amin anasema katika kitabu Naqdhul washia mlango wa 'Taasib': "Hata Taus mwenyewe amekanusha kuwa amepokea Hadith hii na akasema - huyo Taus - kwamba shetani ndiye aliyeiweka kauli hii kwenye ulimi wa aliyeninasibishia mimi." Sayyid amelipokea hilo kwa wapokezi wa kisunni.
- 2. Sehemu ya sita (1\6)
- 3. Sehemu ya nane (1\8