read

Aya 122: Makundi Mawili

Maana

Makundi mawili ni Bani Salama kutoka kabila la Khazraj na Bani Haritha kutoka Aus. Walikurubia kuathirika na harakati za Abdallah bin Ubayya, lau si kuwahiwa na nusura ya Mwenyezi Mungu. Na kauli yake Mwenyezi Mungu: Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuwanusuru. Ni dalili ya mkato kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) huwapa tawfiki yake baadhi ya watu kinyume cha watu wengine.

Kwa sababu Yeye hakuyaacha makundi hayo mawili yaogope na kukimbia. Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi wa anapopasaidia, kama ambavyo ni Mjuzi zaidi anapoweka utume Wake.

وَلَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّهُ بِبَدْرٍ وَأَنْتُمْ أَذِلَّةٌ ۖ فَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ {123}

Hakika Mwenyezi Mungu aliwanusuru katika vita vya Badr hali nyinyi ni madhalili. Basi mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kushukuru.

إِذْ تَقُولُ لِلْمُؤْمِنِينَ أَلَنْ يَكْفِيَكُمْ أَنْ يُمِدَّكُمْ رَبُّكُمْ بِثَلَاثَةِ آلَافٍ مِنَ الْمَلَائِكَةِ مُنْزَلِينَ {124}

Ulipowaambia waumini: Je, haiwatoshi Mola wenu kuwasaidia kwa malaika elfu tatu wenye kuteremshwa.

بَلَىٰ ۚ إِنْ تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا وَيَأْتُوكُمْ مِنْ فَوْرِهِمْ هَٰذَا يُمْدِدْكُمْ رَبُّكُمْ بِخَمْسَةِ آلَافٍ مِنَ الْمَلَائِكَةِ مُسَوِّمِينَ {125}

Ndio! Kama mkisubiri na mkamcha Mungu na wakawajilia katika wakati wao huu, atawasaidia Mola wenu na malaika elfu tano walio na alama.

وَمَا جَعَلَهُ اللَّهُ إِلَّا بُشْرَىٰ لَكُمْ وَلِتَطْمَئِنَّ قُلُوبُكُمْ بِهِ ۗ وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِنْدِ اللَّهِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ {126}

Na Mwenyezi Mungu hakuyajaalia ila ni bishara kwenu ili mioyo yenu ipate kutulia. Na hapana nusra ila itokayo kwa M/Mungu Mtukufu, Mwenye hekima

لِيَقْطَعَ طَرَفًا مِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَوْ يَكْبِتَهُمْ فَيَنْقَلِبُوا خَائِبِينَ {127}

Ili apate kuliangamiza kundi katika waliokufuru au awadhalilishe,warejee hali ya kuwa ni wenye kuambulia patupu.