read

10. Sadaka Huepusha Hatari Katika Mali

Mnapokuwa na hofu ya kupata hatari katika mali, basi mtoe sadaka na kama hampati yule aliyemustahiki, basi mfanye nia sehemu hiyo muitenge na mali yenu.

Al Imam Hasan al-'Askary a.s. anasema kuwa:
“Wakati mmoja Al-Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akiwa pamoja na wenzake walikuwa safari na wenzake hao walikuwa na mali nyingi sana. Na njiani wakapata habari kuwa wako majambazi wanaowapora matajiri mali zao. Kwa kusikia hayo, hao matajiri walianza kutetemeka na wakaingiwa na hofu na wakaanza kumwuuliza Al-Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. Je! tufanyeje sasa?

Na kwa hayo Al-Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akawajibu:
‘Mkabidhini mali yenu yule ambaye ataweza kuhifadhi mali yenu, na kwa kweli ataitunza sana na badala ya kupungua hata itazidi pia, sio hayo tu na pale mutakapokuingiwa na shida ya mali yenu basi yeye kila siku atawarudishia pamoja na nyongeza yake.’

Kwa kusikia hayo hao wenzake aliokuwa nao katika safari wakamwuliza: “Je! ni nani huyo?”

Al-Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akawajibu:
“Yeye ni mmiliki wa malimwengu zote Allah swt.”

Basi hao wenzake wakamwuliza, Je! tunaweza kumkabidhi vipi mali zetu hizi? Hapo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akawaambia: Toeni Sadaka muwape wale wanaostahiki. Kwa kusikia hayo wakauliza, “ewe mjukuu wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.! Hapa tulipo tutawatoa wapi hawa masikini na mafakiri tutawatafuta wapi?” Basi Al-Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. aliwajibu: munuie kuwa sehemu moja ya mali yenu mtatoa Sadaka kisha na msiwe na wasiwasi, Allah swt atailinda mali yenu yote.

“Wale waliokuwa naye pamoja safarini walinuia hivyo kama vile Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. alivyowaambi,a na Imam a.s. akawaambia sasa nyie mko katika amani ya Allah swt, na wakiwa wanaendelea na safari majambazi hao walikumbana nao na kwa kudura za Allah swt wao wakawapita salama usalimini bila ya kudhurika na kusumbuliwa, hadi wakafika mwisho wa safari yao.

Waliopofika tu mwisho wa safari yao, wao wakatoa sehemu moja walizokuwa wamenuia kama Sadaka na sehemu iliyo bakia walifanyia biashara yao, na Allah swt akawajaalia baraka kiasi kwamba wakapata faida hata zaidi ya mara kumi.”