8. Kila Siku Asubuhi Mtoe Sadaka na Mnuie
1. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amenakili riwayah kutoka kwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa:
“Toeni Sadaka asubuhi na mapema kwa sababu kunaondoa balaa kwa siku nzima.”
2. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema kuwa:
“Kwa kutoa Sadaka asubuhi na mapema basi mtoa Sadaka huepukana na kila aina ya matatizo na mabaya yote kwa siku nzima.”
3. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema kuwa:
“Toeni Sadaka asubuhi, na kwa mapenzi kabisa, mwenye kutoa Sadaka amebahatika. Basi humwomba Allah swt amani kutokana na balaa zote zilizoko ardhini na mbinguni, na kwa hakika Allah swt humjaalia hivyo kwa sababu ya kutoa Sadaka.”
4. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. anaelezea kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwusia Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. kuwa:
“Ewe 'Ali! Sadaka huondoa balaa ambazo lazima zitatokezea, na kwa kutenda mema pamoja na ndugu na majamaa kunarefusha umri.
Ya 'Ali! Iwapo jamaa na ndugu ni watu wenye shida, basi kuwapa Sadaka hao haitakuwa ni Sadaka.
Ya 'Ali! Kusema maneno bila vitendo ni ya bure hayana maana, na Sadaka bila kuwa na nia nayo haiwi Sadaka.”
5. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. anasema kuwa: Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwuliza mtu mmoja
“Je! leo umefunga Saumu?”
Mtu huyo alijibu, “La hapana! Ewe Mtume wa Allah.”
Tena Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwuliza:
“Je! leo umeshawahi kumtembelea aliye mgonjwa?”
Naye akajibu: “Hapana! Ewe Mtume wa Allah”
Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliendelea kumwuliza naye aliendelea kumjibu hapana hakufanya hivyo.
Mwishoni Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.aliendelea kumwuliza: “Je! umemlisha masikini yeyote?”
Naye akajibu: “Hapana Ewe Mtume wa Allah!”
Na hapo ndipo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alipomwambia huyo mtu:
“Nenda kwa wananyumba wako, nenda na ukawatendee wema na uwe nao kwa uzuri na uwawie wema, basi hayo ndiyo yatakuwa Sadaka yako kwao.”