read

Sadaka Na Misaada

Wananyumba Wanaostahiki Malipo

Wanaostahiki malipo ni mke (wa ndoa ya kudumu) mtiifu na watoto wake na watoto wa watoto wake na vile inavyoendelea kuteremka chini na ambao wanahitaji msaada, basi ni faradhi. Vile vile baba na mama na babu mzaa baba na mama mzaa mama na vile itakavyoendelea juu na iwapo wanahitaji msaada wake pamoja na watu wengineo, basi kwa kiasi cha uwezo wake kama anao na iwapo hatawapa basi atatazamwa miongoni mwa watu kama qat’a-ur-rahm [kukata mahusiano na familia na majamaa]. Na jambo hili limezungumziwa katika makala mengine.

1. Sadaka zilizo Sunnah

Zipo aina nyingi za malipo yaliyo Sunnah. Katika Ayah na riwayah nyingi mno kumesisitizwa mno kuwa Sadaka itolewe hususan katika siku ya Ijumaa, siku ya ‘Arafah, katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani itolewe kwa makhsusi ya majirani, majamaa n.k. Vile vile Sadaka ni dawa ya ugonjwa, huondoa balaa, huleta riziki, huzidisha mali na huepusha vifo vya kutisha kama kuungua moto, kuzama maji na kuwazuia Majini na kwamba huondoa balaa sabini. Kila utakavyotoa Sadaka zaidi basi matokeo yake pia yatakuwa ni mazuri zaidi. Wala haina kiwango kidogo, kiasi chochote mtu atakachokitoa kitatosha walau hata kama atatoa kokwa moja ya tende basi nayo itatosha.

2. Zawadi

Ni kitu ambacho mtu mmoja anampa mtu mwingine kwa ajili ya kuongezea urafiki ama awe masikini au tajiri. Na iwapo hivyo itakuwa kwa nia ya kutaka furaha ya Allah swt, basi itakuwa ni ‘ibada bora kabisa.

Imeripotiwa kutoka Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. katika Al-Kafi J.5, Uk. 144 kuwa :
“Iwapo mimi nitapenda kumpatia kitu rafiki yangu basi mimi nitampa zawadi kwani ninaipenda zaidi kuliko Sadaka.”

3. Ugeni na Ukarimu

Zipo riwayah nyingi mno kuhusu kuwakirimu wageni na kamba hiyo ndiyo tabia njema ya Mitume a.s. Ipo riwayah moja kuwa Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. kwa muda wa siku saba hakupata mgeni nyumbani kwake basi alisema huku akilia :
“Nasikitika mno na ninakhofu kuwa isije Allah swt akaniondolea rehema na baraka zake.”

4. Haki iliyo Maalumu na isiyo Maalum

Inatubidi sisi tuwe tumepanga viwango maalumu vya kila siku au kila wiki au kila mwezi katika mali zetu kwa ajili ya wale wenye shida na kwa ajili ya majamaa zetu ili kukidhi mahitaji yao.

Amesema Allah swt katika Qur’an: Surah al-Ma’arij, 70, Ayah 24-25 :
‘Na ambao katika mali yao iko haki maalumu. Na mwenye kuomba na anaye jizuilia kuomba…’

Al Imam Musa bin Ja’afer a.s. amepokelewa riwayah kuwa :
“Katika ukoo wa Bani Israil kulikuwa na mtu mwema ambaye alikuwa na mke aliye mwema pia. Siku moja aliota ndoto ambamo aliambiwa kuwa Allah swt amempangia kiasi fulani cha umri wake ambapo nusu ya umri huo utapita katika raha na mustarehe wakati nusu ya umri uliobakia utapita katika shida na dhiki na umasikini.

Hivyo Allah swt amekupa fursa wewe kuchagua iwapo utapenda kupitisha umri wako wa nusu ya awali ya raha na mustarehe na baadaye dhiki na umasikini ? Hivyo chagua mojawapo. Kwa hayo mtu huyo alijibu kuwa: ‘Mimi ninaye mke wangu aliye mwema na hushirikiana naye katika maswala yote, hivyo nitapenda kupewa muda wa kuweza kuongea naye kabla sijatoa uamuzi wa chaguo langu.’

Mke wake alimshauri mumewe kuukubalia umri ule wenye neema uwe ndio wa kuanzia kwani: ‘Inawezekana Allah swt anataka kututeremshia neema na baraka zake hivyo tukaongoka.’

Hivyo usiku uliofuatia, bwana huyo aliulizwa jibu alilolifikia katika uamuzi wake. Naye akajibu : ‘Mimi ninataka kuupitisha nusu ya umri wangu katika neema, raha na mustarehe.’ Kwa hayo akajibiwa kuwa hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa mujibu wa chaguo lake.

Kuanzia hapo yeye alijaaliwa kila aina ya raha na akawa tajiri mkubwa mwenye mali na milki nyingi.

Katika kutajirika huku, mke wake akamwambia, ‘Ewe Bwanangu! Usiwasahau kuwasaidia na kukidhi haja za majamaa zetu na mafukara na masikini na uwe na uhusiano mwema pamoja nao. Na uwazawadie watu fulani fulani wakiwemo majirani na marafiki, zawadi mbalimbali.’

Mtu huyo alizingatia na kutekeleza ushauri uliokuwa umetolewa na mke wake. Na hivyo alifungua milango ya kugawa mali yake katika masuala hayo hadi ulipofika wakati wa kuisha kwa nusu ya umri wake wa awali.

Kuisha huku kwa nusu ya kwanza ya umri wake, aliota ndoto tena ambamo aliambiwa kuwa : ‘Kwa kutokana na uwema wako wa kuwasaidia wenye shida na dhiki imekuwa kipaumbele kwako, basi Allah swt amekubadilishia sehemu hii ya pili kuwa katika raha na mustarehe kama ilivyo sasa.’”

5. Haki ya Uvunaji

Wakati wa mavuno kwa kiwango kile ambacho bado Zaka haijapigiwa hisabu, inagawiwa kwa kuchota mkono moja kwa wapita njia kama vile alivyosema Allah swt katika Quran: Surah al-An-‘Aam 6, Ayah 141 :

‘Na Yeye ndiye aliyeziumba bustani zenye kutambaa juu ya chanja, na zisiyo tambaa, na mitende, na mimea yenye matunda mbali mbali, na mizaituni na mikomamanga inayo fanana. Kuleni matunda yake inapo zaa, na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake. Wala msitumie kwa fujo. Hakika Yeye hawapendi watumiayo kwa fujo.’

Katika aina za Sadaka, aina hizi mbili za Sadaka ni Sunnah kwani Ayah ya Qur'an Tukufu pamoja na riwayah nyingi zimezungumzia na kusisitiza na ndio maana zimezungumziwa mbalimbali.

6. Kukopa Madeni

Yaani kuwakopesha Waislamu ambao wanashida (ya kukopa deni) ili kukidhi masuala yao.
Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema, katika Al-Kafi :“Katika mlango wa Jannat kumeandikwa ‘Yapo mema kumi kwa mtoa Sadaka na mema kumi na nane kwa mkopeshaji madeni.’”

Vile vile Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema, katika Al-Wafi :
“Wakati Mu’min mmoja anapomkopesha Mu’min mwenzake deni kwa ajili ya kutaka ridhaa ya Allah swt , basi Allah swt anamhisabia deni hilo katika Sadaka hadi kuja kulipwa kwake.”

Kila mara mtu atakapokuwa akimpa muhula mdaiwa wake kulipa deni lake, basi Allah swt atakuwa akimwandikia kuwa ametoa Sadaka kiasi hicho kwani yeye alikuwa na haki kamili ya kufanya na kulazimisha malipo lakini hakutumia nguvu kudai na badala yake amemwongezea muda mdaiwa wake, hivyo inamaanisha kuwa amemkopa mara mbili katika mali hiyo. Hivyo mtu huyo anakuwa mustahiki wa kupata thawabu za kutoa Sadaka kwa mara ya pili.

Vile vile Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ameripotiwa akisema kuwa :
“Kwa kupuuzia ‘Ma’un’ (mambo ya nyumbani) ambayo Allah swt ameahidi katika Qur'an Tukufu adhabu, basi si Zaka inayozungumziwa, bali ni kuwasaidia kwa kuwakopesha wale wenye shida na wenye shida wanapokuja kuazima vitu vya nyumbani, basi inabidi kuwaazima vitu vya nyumbani.”

Abu Basir amemwambia Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa
“Majirani zetu wanapokuja kuazima vyombo au vitu vingine vya nyumbani, na tunapo waazima basi huvunja vunja na kuviharibu vitu vyetu na hivyo sisi tunalazimika kuwakatalia kwa misingi hiyo, sasa Je! kuwakatalia huku ni dhambi?”

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. alimjibu :
“Iwapo watu hao wanatabia kama hiyo, basi si dhambi kuwanyima.”

Kuwakopesha Waislamu ambao wanashida ya kukopa deni ili kukidhi masuala yao.
Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema, katika Al-Kafi :
“Katika mlango wa Jannat kumeandikwa ‘Yapo mema kumi kwa mtoa Sadaka na mema kumi na nane kwa mkopeshaji madeni.’”

7. Kuwapa Muda Wadaiwa au Kuwasamehe Madeni

Inabidi kuwapa muda au kuwasamehe madeni wale ambao hawana uwezo wa kuyalipa madeni hayo. Na kuhusiana na swala hili Al Imam Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema :
“Iwapo mtu anataka asidhalilishwe Siku ambayo hakuna mwingine wa kuwaokoa isipokuwa Allah swt , basi inambidi awape muda wa kulipa madeni wadaiwa wake au kuwasamehe madeni yao.”

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema :
“Yeyote yule atakayempa muda wa kulipa madeni ambaye hana uwezo wa kulipa (basi kwa ajili yake ) thawabu zake mbele ya Allah swt ni sawa na thawabu za kutoa Sadaka kila siku kwa kiasi hicho hadi atakapolipwa.”

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. aliambiwa kuwa :
“’Abdur Rahmaan bin Sababah anamdai deni marehemu mmoja, nasi twamwambia yeye kuwa amsamehe lakini yeye anakataa kata kata kumsamehe deni lake.”

Kwa hayo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akasema :
“Ole wake, Je! haelewi kuwa iwapo atamsamehe marehemu deni lake basi Allah swt atamlipa Dirham kumi kwa kila Dirham yake moja. Na iwapo hatamsamehe basi atalipwa Dirham moja kwa Dirham yake moja.”

8. Kusaidia Mavazi na Ukarimu

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema, Al-Kafi, J.2,Uk. 204 :
“Mtu yeyote atakayemsaidia Mu’min kwa mavazi wakati wa baridi au joto basi Allah swt atamjaalia mavazi ya Jannat (Peponi au Paradiso ) na atampunguzia shida kali wakati wa kutoa roho yake (wakati anapokufa) na atampanulia kaburi lake na Siku ya Qiyamah atakapotoka nje ya kaburi lake atakuwa akitoka katika hali ya furaha kwa kuonana na Malaika.”
Vile vile Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema, Al-kafi, J.2, Uk.205 :
“Iwapo Mwislamu yeyote atamsaidia mtu asiye na mavazi kwa nguo [nzuri] au aliye na dhiki ya mali, akasaidiwa ( nyumba,mali n.k ) basi Allah swt anamwekea Malaika elfu saba hadi Siku ya Qiyama kwa ajili ya kumombea maghfirah kwa kila dhambi yake.”

9. Hishima na Taadhima na Kujihifadhi

Ili kujihifadhi na shari, dhuluma na udhalilisho wa madhalimu, kutolewe mali kwa misaada [itolewe mali kuwasaidia wanao hitaji]. Imeripotiwa kuwa ubora ya kutoa mali kwa kusaidia ni kule ambamo kunalindwa hadhi na heshima ya mtu.

10. Mema ya Kudumu

Kutumia mali kwa ajili ya ‘mema ya kudumu’ na kwa faida ya watu, kwa mfano kujenga Misikiti au madrasah, daraja, barabara, kupanda miti, vyoo, kuchimba mito, visima vya maji au kuchapisha vitabu vya dini n.k. ambavyo daima huwafaidisha watu kwa muda mrefu na hivyo mwenye kujitolea kufanya vitu hivi pia huendelea kupata thawabu zake milele.

Marehemu Haji Nouri (r.a.) katika Dar-us-Salaam anamnakili Sheikh mkongwe na ‘A’alam Rabbani Sheikh ‘Abdul Hussein Tehrani ( r.a. ) kuwa :
“Mirza Nabi Khan ambaye alikuwa ni mtu makhsusi katika zama za Muhammad Shah Qajar, hadi alipofariki alikuwa mashuhuri katika kutenda maovu.

Usiku mmoja mimi niliota kuwa nipo ninatembelea Bustani mojawapo na kuangalia majumba ya Jannat ( Peponi au Paradiso ) na ninaye mtu mmoja ambaye ananiongoza na kunionyesha na kunielezea habari mbalimbali. Basi tulifika mahala ambapo mtu huyo aliniambia kuwa hapa kuna maskani ya Mirza Nabi Khan na iwapo utapenda kumtembelea, basi yeye yupo ameketi hapo, mtu huyo alikuwa akinitolea ishara pa mahala hapo.

Mimi nilipoangalia kwa makini nikaona kuwa ameketi peke yake na aliponiona akanifanyia ishara kuwa nipande juu na nilipomfikia na kumkaribia, aliinuka na kunisalimia na kunikaribisha na kunikalisha sebuleni naye aliketi vile alivyokuwa akiketi humu duniani kwa tabia zake zile zile. Mimi kwa hakika nilikuwa nimeshikwa na bumbuwazi kwa hali aliyokuwa nayo.

Yeye aliweza kung’amua yale niliyokuwa nikiyawazia, na hivyo akaanza kuniambia kuwa, ‘Ewe Sheikh! Bila shaka umeshtushwa na kustaajabishwa kwa kuniona katika hali hii hapa Jannat (Peponi) kwani matendo yangu yalikuwa maovu na yaliyokuwa yakistahili adhabu wakati bado nikiwa duniani, kwa hakika hivyo ndivyo ilivyokuwa hapo awali huko katika mji wa Taliqan, nilikuwa na machimbo ya chumvi ambapo kodi yake nilikuwa nikiituma Najaf kila mwaka kwa ajili ya kuomboleza kifo cha Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. pamoja na wananyumba ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Na kwa hakika Allah swt alipendezewa na tendo langu hili na kwa malipo yake amenipatia maskani pamoja na bustani hizi.’

Sheikh Marehemu Haji Nouri anasema kuwa, ‘Mimi niliamka na kutoka katika ndoto hiyo ya kushangaza na kustaajabisha. Na ndoto yangu hiyo niliielezea kwa wanafunzi wangu darasani. Katika darasa hilo kulikuwapo na mwanafunzi mtoto wa Mullah Muti’i Taliqani, ambaye alithibitisha kuwa hayo yalikuwa maneno ya kweli kuwa huyo alikuwa na machimbo ya chumvi huko Taliqan na kodi yake ipatayo kiasi cha Tuman mia moja ( Sarafu ya jamhuri ya Kiislamu ya Iran ) na kiasi hicho alikuwa akikituma Najaf na mzazi wangu ndiye aliyekuwa akiichukua pesa hizo kwa ajili ya kuandaa maombolezo hayo ya kila mwaka ya Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s.

Marehemu Sheikh aliyekuwa mwalimu alikuwa hajui iwapo huyo alikuwa akihusiana na Taliqan na akifanyisha maombolezi kila mwaka huko Najaf.’

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema, katika Al-Wafi, al-Kafi na kunakiliwa pia katika Tahdhiib :
“Baada ya kufariki kwa mtu, huongoka kwa mambo matatu.
- Sadaka ambayo aliitoa humu duniani na ambayo inaendelea baada yake,
- Sunnah ambayo aliitekeleza kwa mfano Adhan ambayo baada ya kifo chake ingali ikiendelea,
- Jambo jema kwamba yeye ataanzisha na itaendelea
Kuacha mtoto mwenye tabia na mienendo mizuri ambaye atakuwa akimombea dua na usamehevu kwa ajili ya wazazi wake (na akifanya mema kwa niaba ya baba yake, kama inavyoelezwa katika vitabu vingine).