read

32. Maovu ya Kuomba Hata Kama Itakuwa ni Kijiti au Maji

1. Muhammad bin Muslim ameripoti riwaya kutoka kwa Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. kuwa amesema:
“Ewe Muhammad! Kama mwombaji (laiti) angelijua kuwa katika kuomba maovu mangapi yamejificha ndani yake, basi kamwe asingenyoosha mikono yake katika kuomba.”

2. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema:
“Ole wenu! Kamwe msiwanyooshee watu mikono yenu kwa ajili ya kuwaomba kwani itawadhalilisheni duniani, na mtakuwa mkijitafutia dhiki na shida na siku ya Qiyama mtasimamishwa katika mazingara magumu kujibu mahesabu yake.”

3. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:
“Mikono iko aina tatu,
kwanza ni mkono ulio juu kabisa ambao ni wa Allah swt

Mkono wa pili ni ule ambao ni wa mtoaji na

wa tatu ni wa yule wa mpokeaji ambao ni wa chini kabisa

Kila ikiwezekana mjaribu kujiepusha na kuomba, kwa sababu hiyo itakuwa ni vizuizi katika riziki yenu hapo mbeleni.

Iwapo mtu atapenda kuinusuru na kuihifadhi na kuilinda heshima na aibu yake basi anaweza kujichumia na kujitafutia riziki yake mwenyewe kwani kunakuwapo na pazia mbele ya riziki..

Kwa kiapo cha Allah swt ambaye roho yangu iko mikononi mwake, iwapo mtu akienda msituni ambapo akakata kuni na siku hiyo hiyo akaziuza au kubadilishana kwa tende na sehemu moja ya tende hizo akajiwekea yeye kumalizia shida zake na sehemu mbili akizigawa katika kuwasaidia wengine katika njia ya Allah swt, basi kwa hakika matendo yake haya ni bora na afadhali kabisa kuliko kunyoosha mikono yake mbele ya watu kwa ajili ya kuomba, kwani pengine wao watampa kidogo au chochote na wengine watamdanganya na kumdharau au na hata kumdhalilisha.”

4. Abu Basir ameripoti riwaya kutoka Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa:
“Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliijiwa na baadhi ya watu kutoka makabila ya Ansaar ambao baada ya kutoa salamu waliketi, na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliwajibu salamu yao.

Wao wakasema ewe Mtume wa Allah swt sisi tuna ombi letu moja. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akawaambia wamwambie. Nao wakasema ni haja yetu moja kubwa kabisa. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kwa kusikia hayo akasema nawaombeni mniambie ili niweze kujua. Wao wakaanza kusema, ombi letu ni kwamba tunakuomba wewe uchukue dhamana yetu ya kuingia Jannat (Peponi).
Kwa kusika hayo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alikiinamisha kichwa chake na kutumia vidole vyake alianza kama kuchimba ardhini kwa vidole vyake. Muda si muda akainua kichwa chake juu na kusema:
“Ninaweza kuwapa dhamana hiyo kwa masharti kwamba kamwe katika mazingira yoyote yale nyie hamtamwomba mtu yeyote kitu chochote.”

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. anasema kuwa hao watu hali yao ilikuwa mbaya kabisa kiasi kwamba katika safari hata kama fimbo yao ilikuwa ikidondoka basi wao walikuwa hawamwombi mtu yeyote msaada na hivyo walikuwa wakiteremka chini kutoka wanyama wao na wakijiinulia fimbo zao na walipokuwa wakikaa juu ya meza kwa chakula, wao walikuwa hawawaombi wenzao maji. Bali walikuwa wakienda wenyewe pale penye maji na walikuwa wakiyanywa.”

5. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema:
“Allah swt anamrehemu yule mja wake ambaye amebakia katika heshima utoharifu na katika desturi zake njema, na ambaye amejiokoa na hakuomba; kwa hakika kuomba kunaleta udhalilisho duniani, na uelewe wazi kuwa watu humu duniani kamwe hawataweza kummalizia shida zake zote. Na hapo baadaye Imam a.s. akaelezea kisa kimoja kwa kifupi cha Hatim:
Wakati nafsi za watu zinapo kata tamaa kwa watu basi hapo kwa hakika yanaingia katika shida na taabu kubwa, na kwa uhakika tamaa ndio ufakiri mkubwa na tamaa ndiyo ufukara mkubwa.”

6. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kwa kupitia Maimamu a.s. ameripoti riwaya kuwa:
“Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwusia Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s.,
“Ewe Ali! Ni rahisi kabisa kuutia mkono wako katika mdomo wa nyoka mkubwa kuliko kumyooshea mkono yule ambaye alikuwa hayupo duniani na akaja akazaliwa baadaye.”
Na akamwambia Abu Dhar: “Ewe Aba Dhar! Ole wako kamwe usiombe kwa sababu ni udhalilisho na unakaribisha shida na taabu. Na vile vile siku ya Qiyama utatakiwa utoe mahesabu yake makubwa na marefu.
Na akaendelea kusema “Ewe Aba Dhar! Kamwe usifungue kiganja chako kwa ajili ya kuomba.

Naam, unyooshe mikono yako kwa Allah swt kwa kumshukuru kwa ile riziki aliyokupa.”

7. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema:
“Msiwe miongoni mwa watu wasio wajali watu, msiwe kama watu wenye kuwa na dhiki na shida kama maji mnayoyatema baada ya kupiga mswaki mnavyo sukutua.”

8. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. katika kitabu Thawabul A’amal imeandikwa riwaya ya kuwa amesema:
“Allah swt anamrehemu yule mtu ambaye ameweka desturi na tabia zake kitakatifu na amejizuia kwa njia zote asiombe kwa watu. Kwa hakika kuomba ni kudhalilika na kujidhalilisha duniani na hakuna duniani wale watu watakaoweza kumtimizia haja yake.”

9. Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. amesema:
“Allah swt amemfanya Mtume Ibrahim a.s. kuwa Khalil wake (Rafiki wake) kwa sababu yeye kamwe hakulitupilia mbali jambo ambalo alimwomba yeye na yeye mwenyewe kamwe hakumnyooshea mtu yeyote mikono yake isipokuwa kwa Allah swt.”

10. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema katika riwaya moja iliyo ripotiwa kuwa:
“Allah swt bila shaka anawachukia sana wale watu ambao hawana aibu, na ni wachafu (kimwili na kiroho), na vile vile mtu yule ambaye amegunduliwa kwa watu kwa tabia zake za kuomba omba.”

11. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema:
“Msiwaombe ndugu zenu mahitaji yenu, isitokee kwamba wao wakakataa kukutimizia maombi yako, na nyie mkachukia na mkaingia katika kukufuru.”

12. Bwana Salman Al-Farsi r.a. anasema kuwa :
“Mpenzi wangu Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amefanya usia na kusisitiza kabisa kuwa, mimi nisipuuzie mambo saba.
Ya kwanza yeyote yule aliye mkubwa kuliko mimi nisimtupie macho yangu, bali nimtupie macho yule ambaye yuko chini yangu;

niwe na mapenzi na maskini na

niwe karibu nao,

niseme ukweli daima hata kama utakuwa mchungu,

niwatendee mema na kuwahurumia ndugu na majamaa zangu, hata kama yule nimfanyiaye hayo atanigeuzia mgongo,

kamwe nisiunyooshe mkono wangu mbele ya watu kuwaomba na vile vile ameniusia kuwa

daima niwe nikisema La Haula Wala Quwwata Illa billahil ‘Aliyyil ‘Adhiim kwani hiyo ni hazina mojawapo katika hazina za Jannat.”

13. Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. (Nahjul Balagha) anasema:
“Muwe mkiziachia matamanio na mahitajio yenu kuliko kuwaomba waovu na wasio stahiki. Na akaendelea kusema na utakatifu na utukufu ni sifa moja ya kupendeza ya mafakiri, na hakika urembo wa shida na dhiki ni kushukuru.”

14. Al Imam 'Ali bin Abi Talib a.s. amesema:
“Ujue kuwa uso wako unaong’ara kwa heshima na adabu, na wewe wakati unapokwenda kuomba na ukarefusha mikono yako kwa ajili ya kuomba basi heshima na adabu hiyo inayeyuka na kuanza kudondoka kutoka usoni mwako. Sasa ni kuangalia uyeyukaji huo unamdondokea nani ndio wewe unatakiwa ujue uangalie na ujue.”

Ibn Fahad ameripoti riwaya kutoka Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa:

“Shi’a wetu hata kama watakuwa wakifa kwa njaa basi kamwe wakati wowote ule hawatainyoosha mikono yao kwa mbele ya watu kwa ajili ya kuomba.”

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Mtu yeyote anayenyoosha mkono wake na kufungua kiganja chake kwa ajili ya kuomba, basi ushahidi wake utupiliwe mbali.”

17. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema:
“Iwapo mwombaji angelikuwa akijua yale majukumu na wajibu walio nao katika kufanya hivyo, basi kamwe asingeomba chochote kwa mtu yeyote. Na vile vile na kutokumpa mwombaji pia kuna majukumu na wajibu mkubwa sana iwapo watu wangelijua basi kamwe wasingeli wakatalia kuwasaidia watu.”

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. siku moja aliwaambia Ma-Sahaba wake:

“Ni kwa nini hamfanyi bay’a yangu (utiifu wangu)?”

Basi Ma-Sahaba wakamjibu:
“Ewe Mtume wa Allah swt! Sisi tumeshakwisha kufanya bay’a yako tangu mwanzoni. Kwa hayo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akasema, mfanye bay’a katika swala ambalo mle kiapo kuwa nyinyi kamwe hamtanyoosha mikono yenu kwa wengine kwa ajili ya kuomba. Na baada ya kula viapo hivyo ikaonekana mandhari tofauti kabisa miongoni mwa Ma-Sahaba kiasi kwamba hata mtu alipokuwa akidondosha mkongojo wake basi alikuwa akiteremka kutoka usafiri wake wa mnyama kama ngamia n.k. kuteremka chini na kujiokotea mkongojo wake, na kamwe alikuwa hamwambii mtu mwingine amwokotee na kumpa hiyo bakora yake iliyoanguka.”

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema:

“Iwapo mtu atakwenda mbio mbio msituni akakata kuni na mzigo huo akauchukua kuja nao kwa hiyo atakuwa ametunza heshima na hadhi yake, basi jambo hilo ni afadhali kuliko udhalilisho wa kuomba.”

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Yeyote yule aliyetuomba sisi tunampa na yeyote yule aliyetoa na yeyote yule aliye shukuru basi Allah swt atamfanya awe tajiri.”

Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema:

“Kwa kuwaomba watu mahitajio yako ni sawa na kuteketeza na kuangamiza heshima yako, na vile vile ustahi wako pia unamalizika. Na kwa hakika kile walichonacho wao, ni utajiri wao, inambidi mtu akate tamaa asitegemee chochote yaani asiwe na tamaa ya aina yoyote na hakika hii ndio inayo hesabika kuwa ni heshima kubwa ya muumin. Kumbukeni kuwa tamaa ni ufakiri wa aina mojawapo.”

Ja’bir amenakili riwaya kutoka Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa amesema:

“Allah swt ameweka karaha kwa wale wanao omba kwa kunang'ania na kwa kufuatilia.”