read

50. Kuwafanyia Hisani na Wema Ndugu Zetu Katika Imani

Ni sunnah kuwatendea mema waumini na kuwatimizia mahitaji yao kwa uwezo alionao mtu na kuwa na uhusiano mwema pamoja na mashi’a wenzake.

1. Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. amesema:
“Yeyote yule ambaye hakubahatika kutufanyia sisi wema basi ni wajibu wake kuwafanyia mema na kuwatimizia mahitaji ya marafiki zetu. Na yeyote yule ambaye hakubahatika kudhuru makaburi yetu basi adhuru makaburi ya wafuasi na marafiki zetu.”

2. Muhammad bin Ali bin Hussein Jamil amenakili riwaya moja kutoka kwa Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa:

“Miongoni mwenu mtu aliye bora kabisa ni yule mwenye moyo mkarimu yaani mwenye moyo wa kutoa na mtu mwovu kabisa ni yule ambaye ni bahili. Na usafi wa imani, dalili yake ni kwamba huwawia kwa wema mu’min wenzake na kuwatimizia dharura na mahitajio yao. Bila shaka yeyote yule anayewafanyia hisani ndugu zake katika imani basi ndiye mpenzi wa Allah swt kwa sababu katika kufanya wema huko kuna mambo mengi yanayomzuia mtu asiingie katika mitego ya Sheitani na vile vile asiingie Jahannam, na kwa matokeo yake ndiye mtu anayeingia Jannat.”

Baada ya hapo Imam a.s. alimwambia Jamil, “Ewe Jamil! Habari hizi uwafikishie wenzako.

Kwa hayo mimi nikasema, “Ewe mwana wa Mtume wa Allah swt! Niwe fidia juu yako. Je! ni watu gani hao?”

Imam a.s. akasema: “Hao ni wale ambao wanawafanyia wema ndugu zao katika imani wakati wa shida huwa pamoja nao na vile vile wakati wa furaha pia huwa nao.”

3. Sheikh Saduq a.r. amenakili riwaya kutoka kwa Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ambaye amesema kuwa:
“Yeyote yule ambaye hakupata fursa kufanya wema nasi, basi awafanyie wema wapenzi na wafuasi wetu basi atapata thawabu za kutufanyia wema sisi. Na vile vile ambaye hakubahatika kutuzuru sisi katika uhai wetu na uhai wake basi awazuru wapenzi na wafuasi wetu, basi atapata thawabu kama za kutuzuru sisi.”

4. Safwan Al-Jammal anasema kuwa siku moja Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. alimwambia Mu’alla bin Khunais:
“Ewe Mu’alla! Uwe wa Allah swt, ili Allah swt aweze kukutunza na kukuhifadhi.

Kwa hayo Mu’alla alianza kusema: “Je! hivyo inawezekanaje?”

Basi Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akamjibu, uwe na hofu ya Allah swt, uwe daima ukimwona yeye katika mawazo yako, kwa hiyo yeye atakifanya kila kitu kiwe kinakuogopa wewe, na vile vile kitakuwa kinakuwazia wewe na kukujali wewe. Ewe Mu’alla ili kujipatia mapenzi ya Allah swt lazima uwatendee watu matendo mema, na utambue wazi wazi kuwa Allah swt anapendezewa sana na moyo wa ukarimu na huchukizwa sana na ubahili na huwa na uadui nao.

Angalia! Wewe kama utaniomba chochote na mwisho wake wewe ukaanza kufanya mapenzi nami, na badala yake mimi nitafurahishwa sana iwapo wewe hautaniomba chochote na hautapata chochote kutoka kwangu na baada ya hayo wewe bado ukawa na mapenzi nami.

Na kwa hakika ukiniuliza mema yote naweza kuyafanya kwa ajili yako basi ukweli ni kwamba sifa zote ni za Allah swt kwa sababu yeye amekupitishia neema yake kwa mikono yangu; mimi nimekuwa ni kipitishio tu kwa ajili yako kwa hiyo yeye ndiye anayestahiki sifa zote.”

5. Ali ibn Ibrahim anaandika katika tafsiri yake kuwa mtu mmoja alitokezea katika kikao cha Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. na humo akaanza kuwazungumzia matajiri na mara akaanza kuwasema vibaya na kuwatukana.

Kwa kusikia hayo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. alimwambia, “Nyamaza!”
Wale mafukara ambao wanawajali ndugu na jamaa zao na kuwawia wema wenzao, Allah swt huwapa ujira mzuri sana, kwa sababu Allah swt amesema katika Qur'an Tukufu: Surah Sabaa, 34, ayah 37:
‘Na si mali yenu wala watoto wenu watakao kukaribisheni kwetu muwe karibu, isipo kuwa aliye amini na akatenda mema. Hao basi watapata malipo maradufu kwa walio yafanya. Nao watakuwa salama katika maghorofa.’