read

Aya 1 – 6: Mwenye Kusamehe Dhambi Na Kukubali Toba

Maana

Hamim.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 1(2:1).

Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa sababu ni mizani ya haki na ya uadilifu na ni nuru inayoongoza kutokana na giza la upotevu na ujinga.

Mwenye nguvu, Mwenye kujua, Mwenye kughufiria dhambi na anayekubali toba, Mkali wa kuadhibu, Mwenye fadhila.

Kila sifa katika wasifu huu ina mfungamano na athari katika ulimwengu na binadamu na mwenendo wake: Mwenye kuumba ulimwengu ni lazima aujue na awe na uweza. Ndio ikaja sifa ya mwenye nguvu mwenye kujua. Kuwa na nguvu ni kuwa na uwezo.

Dhambi na toba ni vitendo vya mtu, lakini kukubali toba na kusamehewa ni kwa Mwenyezi Mungu. Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t.) husamehe kwa toba au kwa utiifu, kwa sababu mema yanafuta maovu. Vile vile Yeye ni mkali kwa anayeng’ang’ania uasi, wakati huohuo yeye ni mwenye fadhila kwa sababu anampa anayemuomba na asiyemuomba na anamuongezea mengi mtenda mema

Hakuna mungu ila Yeye.

Amepwekeka na sifa ya Tawhid, elimu ya ghaibu na uwezo juu ya kila kitu. Wenye madhambi wote wanahitajia msamaha wake na huruma yake.

Marejeo ni kwake.

Hakuna pa kukimbia kuepuka kukutana naye na hisabu yake na malipo yake. Heri zote ni za yule asiyeona yeyote mwenye kustahiki sifa hizi isipokuwa Mwenyezi Mungu, na wala asiogope yeyote asiyekuwa Yeye.

Hawabishani katika Ishara za Mwenyezi Mungu ila wale ambao wamekufuru, wasiotaka haki na uadilifu wala kuamini chochote isipokuwa hawaa na masilahi yao tu.

Pamoja na hayo wanajitafutia visababu, wakidai kuwa wao ndio walio na haki na kuijadili Qur’ani wakisema kuwa ni ngano za watu wa kale, tawhid ni upotevu na kufufuliwa ni uzushi. Dalili yao ya kwanza na ya mwisho ni kuwa wao wanawaiga mababa zao na kufuata masilahi.

Basi kusikughuri - ewe Muhammad - kutangatanga kwao katika nchi kwa ajili ya biashara na kwenda kwao Sham katika msafara wa kusi na Yemen katika msafara wa kaskazi. Yasikughuri haya, kwa sababu mwisho wake ni maangamizi:

إِنَّمَا نُمْلِي لَهُمْ لِيَزْدَادُوا إِثْمًا ۚ وَلَهُمْ عَذَابٌ مُهِينٌ {178}

“Hakika tunawapa muda na wanazidi tu katika dhambi na wana adhabu idhalilishayo.”
Juz.
4 (3:178).

Kabla yao walikadhibisha kaumu ya Nuh na makundi baada yao. Na kila uma ulikuwa na hamu juu ya Mtume wao wamkamate. Na walibishana kwa upotovu ili kuipindua haki.

Makusudio ya makundi hapa ni kila watu waliounda kikosi dhidi ya haki na watu wake.
Maana ni kuwa vita vyako ewe Muhammad, pamoja na washirikina, sio vita vyako wewe binafsi; isipokuwa ni vita baina ya haki na batili na kufuru na imani. Ni desturi ya waliopita na wanokuja.

Uma zilizopita ziliwakadhibisha mitume na viongozi wema. Wakawajadili kwa ujinga na inadi. Kila uma ulijaribu kumuua Nabii wao na muonyaji wao; sawa na walivyokupangia njama makuraishi ukiwa umelela kitandani mwako.

Tazama Juz. 9 (30 – 35).

Kwa hivyo niliwakamata. Basi ilikuwaje adhabu yangu!

Ilikuwa kali ya kuvunjavunja.

Namna hivi limewathibitikia makafiri neno la Mola wako kwamba wao ni watu wa Motoni.

Haya ni maonyo na hadhari kwa makuraishi kama waking’ang’ania ukafiri na upotevu, yasije yakawapata, yaliyowapata watu wa Nuh, A’d na Thamud.

Lakini kumhofisha asiyemuogopa Mwenyezi Mungu hakuna manufaa yoyote, isipokuwa kusimamisha hoja na kukata visababu vyote.

الَّذِينَ يَحْمِلُونَ الْعَرْشَ وَمَنْ حَوْلَهُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيُؤْمِنُونَ بِهِ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَحْمَةً وَعِلْمًا فَاغْفِرْ لِلَّذِينَ تَابُوا وَاتَّبَعُوا سَبِيلَكَ وَقِهِمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ {7}

Wale wanaobeba Arshi, na wanaoizunguka, wanamsabihi kwa kumuhimidi Mola wao, na wanamuamini na wanawaombea msamaha walio amini. Mola wetu! Umekienea kila kitu kwa rehema na ujuzi. Basi wasamehe ambao wametubu na wakaifuata Njia yako, na waepushe na adhabu ya Jahannamu.

رَبَّنَا وَأَدْخِلْهُمْ جَنَّاتِ عَدْنٍ الَّتِي وَعَدْتَهُمْ وَمَنْ صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ ۚ إِنَّكَ أَنْتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ {8}

Mola wetu! Na waingize katika Bustani za Milele ulizowaahidi. Na pia waliofanya mema miongoni mwa wazee wao na wake zao na dhuriya zao. Hakika Wewe ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

وَقِهِمُ السَّيِّئَاتِ ۚ وَمَنْ تَقِ السَّيِّئَاتِ يَوْمَئِذٍ فَقَدْ رَحِمْتَهُ ۚ وَذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ {9}

Na waepushe na maovu; kwani umwepushaye maovu siku hiyo, hakika umemrehemu; na huko ndiko kufuzu kukubwa.

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا يُنَادَوْنَ لَمَقْتُ اللَّهِ أَكْبَرُ مِنْ مَقْتِكُمْ أَنْفُسَكُمْ إِذْ تُدْعَوْنَ إِلَى الْإِيمَانِ فَتَكْفُرُونَ {10}

Kwa hakika wale waliokufuru watanadiwa: Bila ya shaka kuchukia Mwenyezi Mungu ni kukubwa kuliko kujichukia nyinyi nafsi zenu, mlipokuwa mnaitwa kwenye imani mkakataa.