read

Aya 1 – 8: Kitabu Kilichopambanuliwa

Maana

Haa Mim.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1). Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameianza sura hii kwa kuitaja Qur’ani na kuisifu kwa sifa zifuatazo:

1. Ni uteremsho kutoka kwa Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

Qur’ani imetoka kwa Mwingi wa kurehemu Mwenye kurehemu, nayo ni rehema kwa walimwengu. Pia aliyeshuka nayo kuileta kwa Muhammad (s.a.w.) ni rehema, kwa sababu yeye ni roho mwaminifu. Na Mwenyezi Mungu amemtolea ushahidi Mtume wake mtukufu kuwa yeye anawahangaikia sana; kwa waumini ni mpole mwenye huruma” Juz. 11 (9:128) .

Kwa hiyo basi Qur’ani ni rehema, aliyetumwa kuifikisha kwa Mtume ni rehema, Mtume ni rehema na Yule ambaye ameiteremsha ndiye msingi na chimbuko la rehema. Basi natija ya uhakika ya rehema (huruma) hizi nne ni kuwa mwenye kushikamana na Qur’ani na akaitumia, hushukiwa na mmiminiko wa rehema, na mwenye kuachana nayo, atakuwa ameidhulumu nafsi yake na ameichagulia maangamizi na balaa.

2. Ni Kitabu kilichopambanuliwa Aya zake.

Zinazobainisha halali ya Mwenyezi Mungu, haramu yake, nasaha zake na mawaidha yake, wala hazikumwachia udhuru mwenye kutafuta udhuru na visababu.

3. Qur’ani ya Kiarabu kwa watu wanaojua.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameiteremsha Qur’ani kwa Kiarabu, kwa vile hamtumi Mtume ispokuwa kwa lugha ya watu wake, ili waweze kumfahamu. Ilikuwa hivyo kwa Ibrahim, Tawrat ya Musa na Injil ya Isa (a.s.).

Nabii Muhammad (s.a.w.) alimwandikia Kisra, Kaizari, viongozi na wafalme wengineo wasiokuwa wa kiarabu, kwa lugha ya kiarabu, akiwaita kwenye Uislamu. Yametangulia maneno kuhusiana na hilo katika Juz. 12 (12:2) na Juz. 22 (36:1-12) kifungu ‘Mdundo wa ndani katika Qur’ani’.

Vyovyote iwavyo ni kuwa siri ya ukuu wa Qur’ani haiwi kwenye lugha na mfumo peke yake; bali inakuwa katika maana yake na malengo yake ya kudumu yasiyokuwa na mipaka ya kibaguzi, kizazi wala wakati.

4. Inayotoa bishara, na inayoonya.

Qur’ani inampa mtiifu habari njema ya rehema za Mwenyezi Mungu na pepo yake, na inamuonya muasi kwa adhabu ya Mwenyezi Mungu na hasira yake.

Lakini wengi wao wamepuuza; kwa hiyo hawasikii.

Wamepuuza haki kwa ujinga na kung’ang’ania kuiga mababa au tamaa ya manufaa ya haraka haraka; hata kama ni njozi na mawazo tu.

Na wakasema: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa hayo unayotuitia, na masikio yetu yana uziwi, na baina yetu na wewe kuna pazia. Basi wewe tenda, nasi tunatenda.”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) aliwapa, wapenda anasa wakishirikina mwito wa kumwamini Mwenyezi Mungu peke yake na kutumia Kitabu chake, lakini jawabu lao lilikuwa nyoyo zetu zina kizuizi na wewe, na masikio yetu hayakusikilizi na sisi na wewe tuko mbali mbali. Jitahidi utakavyo na utoe vitisho sisi hatutishiki.

Hivi ndivyo yafanyavyo matamanio – yanaua moyo na kupofusha macho na yanatoa uhuru wa ujinga na upotevu.

Sema: Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; ninapewa wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Basi nyookeni sawa kumwendea Yeye, na mumtake maghufira.

Mataghuti walimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kuwa baina yetu na wewe kuna kizuizi, Mwenyezi Mungu akamwamuru Nabii wake mtukufu awaambia, kizuizi hiki na nyinyi kimetokea wapi?
Kwani mimi si ni mtu tu kama nyinyi, kiroho na kimwili, nikifanya manayoyafanya? Je, wahyi ulionijia kuwa mimi na nyinyi tumwamini Mungu mmoja na tusimshirikishe na yeyote, tutubie kwake na twende sawa kwenye njia ya haki na uadilifu, ndio unaniweka mbali na nyinyi? Au hiyo ndio ingekuwa njia bora ya kutuunganisha kwenye heri na takua? Lakini nyinyi mmekataaa ispokuwa upofu tu na upotevu.

Na ole wao wanaomshirikisha ambao hawatoi Zaka nao ndio wanaoikataa Akhera.

Katika tafsir Albahrul-muhit imeelezwa kuwa sura hii imeshuka Makka na sharia ya zaka ya mali ilishuka Madina, kwa hiyo hapa hapana budi kuifasiri zaka kwa maana ya kutoa tu kwa aina yoyote ya heri au kuifasiri kwa maana ya kuitwaharisha nafsi na ushirikina.

Sisi tunaitilia nguvu tafsiri ya kwanza, kwa sababu kama tukifasiri kwa maana ya kutwaharika nafsi na washirikiana tayari wanajulikana kuwa haawakutwaharika na shirk, itakuwa ni kama kufasiri maji kwa maana ya maji. Kwa hiyo maana yanakuwa washirikina wamekusanya mambo mabaya matatu: Ushirikina, kupinga Akhera na ubakhili.

Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema watakuwa na ujira usiosimbuliwa.

Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawalipa na kuwapa thawabu bila ya kuwasimbulia kwa sababu wao wanastahiki kila ukarimu. Neno kusimbulia tumelifasiri kutokana na neno mann ambalo pia hufasiriwa kwa maana ya kukatika. Kuifasiri Aya kwa maana yoyote kati ya hayo mawili inafaa, lakini tunaona ya kwanza iko karibu zaidi.

قُلْ أَئِنَّكُمْ لَتَكْفُرُونَ بِالَّذِي خَلَقَ الْأَرْضَ فِي يَوْمَيْنِ وَتَجْعَلُونَ لَهُ أَنْدَادًا ۚ ذَٰلِكَ رَبُّ الْعَالَمِينَ {9}

Sema: Hivyo nyinyi mnamkataa aliyeumba ardhi katika siku mbili, na mnamfanyia washirika? Huyo ndiye Mola wa walimwengu wote.

وَجَعَلَ فِيهَا رَوَاسِيَ مِنْ فَوْقِهَا وَبَارَكَ فِيهَا وَقَدَّرَ فِيهَا أَقْوَاتَهَا فِي أَرْبَعَةِ أَيَّامٍ سَوَاءً لِلسَّائِلِينَ {10}

Na akaweka humo milima juu yake na akabarikia humo na akakadiria humo chakula chake katika siku nne. Ni sawa kwa wanaouliza.

ثُمَّ اسْتَوَىٰ إِلَى السَّمَاءِ وَهِيَ دُخَانٌ فَقَالَ لَهَا وَلِلْأَرْضِ ائْتِيَا طَوْعًا أَوْ كَرْهًا قَالَتَا أَتَيْنَا طَائِعِينَ {11}

Kisha akaielekea mbingu, na ilikuwa moshi, akaiambia hiyo na ardhi: Njooni, kwa hiari au kwa nguvu! Vyote viwili vikasema: Tumekuja nasi ni watiifu.

فَقَضَاهُنَّ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ فِي يَوْمَيْنِ وَأَوْحَىٰ فِي كُلِّ سَمَاءٍ أَمْرَهَا ۚ وَزَيَّنَّا السَّمَاءَ الدُّنْيَا بِمَصَابِيحَ وَحِفْظًا ۚ ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ {12}

Basi akazifanya mbingu saba kwa siku mbili, na akaipangia kila mbingu mambo yake. Na tukaipamba mbingu ya dunia kwa mataa na kwa ulinzi. Hayo ndio makadirio ya Mwenyezi nguvu Mwenye Kujua.