read

Aya 13 – 18: Nawahadharisha Ukelele

Maana

Basi wakipuuza, sema: Nawahadharisha ukelele mfano ukelele wa A’di na Thamudi. Walipowafikia Mitume mbele yao na nyuma yao wakawaambia: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu!

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kuhusiana na washirikina wa kiarabu. Mbele yao na nyuma yao ni kinaya cha msisitizo wa mitume na jitihadi zao katika kubashiria na kuonya, na kwamba wao walifuata kila njia kwa ajili ya kuwaongoza wao, lakini shetani akawapambia na akawaingizia dhana yake, pale aliposema:

ثُمَّ لَآتِيَنَّهُمْ مِنْ بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَنْ شَمَائِلِهِمْ ۖ وَلَا تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ {17}

“Kisha hakika nitawaendea kwa mbele yao na nyuma yao na kuumeni kwao na kushotoni kwao; wengi katika wao hutawakuta wenye kushukuru.” Juz. 8 (7:17).

Maana ni kuwa, sema ewe Muhammad kumwambia yule anayekukanusha wewe na risala yako kuwa A’d na Thamud waliwakadhibisha waliowalingania kama haya ninayoyalingania – Tawhid, na wakatoa juhudi zao kwa ajili ya uongofu wao.

Lakini walipong’ang’nia kwenye upotevu, Mwenyezi Mungu aliwakamata kwa adhabu ya dunia na Akhera na kwam- ba mimi nawaonya yasije yakawasibu yale yaliyowasibu wao.

Wakasema: Angelitaka Mola wetu bila ya shaka angeliwateremsha Malaika. Basi sisi hakika tunayakataa hayo mliyotumwa.

A’d na Thamud waliwajibu mitume kwa kuwakadhibisha kwa sababu Mwenyezi Mungu, kwa madai yao, hatumi ispokuwa Malaika. Kauli yao hii tumeipinga katika kufasiri Juz. 7 (6:9).

Ama kina A’di walitakabari katika ardhi bila ya haki,

Kauli yake Mwenyezi Mungu: bila ya haki ni katika upande wa kufafanua na kusiitiza tu. Kwa sababu hakuna kiburi cha haki; hasa ikiwa ni kumfanyia kiburi Mwenyezi Mungu.

A’di walifanya kiburi wakawadharau wanyonge na wakasema hakuna yoyote anayetuweza.

Na wakasema: Nani aliye na nguvu zaidi kuliko sisi? Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu ambaye amewaumba ni Mwenye nguvu zaidi kuliko wao?

Hili ni wazi, halihitaji dalili. Imam Aliy (a.s.) anasema: “Kila mtukufu asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni dhalili, na kila mwenye nguvu asiyekua yeye Mungu ni dhaifu, na kila mfalme asiyekua Yeye ni mmilikiwa, na kila mjuzi asiyekua yeye ni mwanafunzi na kila muweza asiyekua Yeye ni dhaifu.

Na wao wakawa wanazikataa Ishara zetu!

Walizikana dalili za ulimwengu zinazofahamisha umoja wa Mwenyezi Mungu na ukuu wake. Wakasema kila kilichomo ulimwenguni pamoja na mpangilio wake na nidhamu ni kazi ya maumbile.

Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku za nuhusi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katika uhai wa duniani, na bila ya shaka adhabu ya Akhera ina hizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwadhibu duniani kwa upepo uliokuja na baridi katika siku za mkosi na hizaya, kisha watakamilisha adhabu kali zaidi na ya kufedhehesha huko Akhera kuliko adhabu ya duniani.

Na ama Thamudi tuliwaongoza, lakini walistahabu upofu kuliko uwongofu. Basi uliwachukua ukelele wa adhabu ya kuwafedhehi kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

Aya hii ni dalili wazi kwamba mtu ana hiyari wala halazimishwi, kwa sababu inasema Mwenyezi Mungu aliwaongoza Thamud kwenye njia ya uokovu, akawaamrisha kuifuata na akawakataza maasi, akawabainishia njia ya maangamizi akawakataza na kuwahadharisha na mwisho mbaya kama wataifuata, lakini wakaathirika nayo kuliko ya uokovu; ikawa malipo yao ni balaa na hasara.

Na tukawaokoa wale ambao wameamini na wakawa na takua.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwaokoa kwa sababu walifuata njia ya uokovu. Yametangulia mazungumzo kuhusu A’di katika Juz.12 (11:50) na kuhusu Thamud katika Juzuu hiyo hiyo na sura hiyo Aya 50.

وَيَوْمَ يُحْشَرُ أَعْدَاءُ اللَّهِ إِلَى النَّارِ فَهُمْ يُوزَعُونَ {19}

Na siku watakapokusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu kwenye Moto, nao watazuiliwa.

حَتَّىٰ إِذَا مَا جَاءُوهَا شَهِدَ عَلَيْهِمْ سَمْعُهُمْ وَأَبْصَارُهُمْ وَجُلُودُهُمْ بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {20}

Hata watakapoufikia Moto yatawashuhudia masikio yao, na macho yao na ngozi zao kwa waliyokuwa wakiyatenda.

وَقَالُوا لِجُلُودِهِمْ لِمَ شَهِدْتُمْ عَلَيْنَا ۖ قَالُوا أَنْطَقَنَا اللَّهُ الَّذِي أَنْطَقَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُوَ خَلَقَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ {21}

Na wataziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia? Zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu ambaye ametamkisha kila kitu! Na Yeye ndiye aliyewaumba mara ya kwanza, na kwake Yeye mtarejeshwa.

وَمَا كُنْتُمْ تَسْتَتِرُونَ أَنْ يَشْهَدَ عَلَيْكُمْ سَمْعُكُمْ وَلَا أَبْصَارُكُمْ وَلَا جُلُودُكُمْ وَلَٰكِنْ ظَنَنْتُمْ أَنَّ اللَّهَ لَا يَعْلَمُ كَثِيرًا مِمَّا تَعْمَلُونَ {22}

Na hamkuwa wenye kujificha hata masikio yenu, na macho yenu, na ngozi zenu, zisiwashuhudie. Lakini mlidhani kwamba Mwenyezi Mungu hayajui mengi katika mliyokuwa mkiyatenda.

وَذَٰلِكُمْ ظَنُّكُمُ الَّذِي ظَنَنْتُمْ بِرَبِّكُمْ أَرْدَاكُمْ فَأَصْبَحْتُمْ مِنَ الْخَاسِرِينَ {23}

Na hiyo dhana yenu mliyokuwa mkimdhania Mola wenu, imewaangamiza; na mmekuwa miongoni mwa waliopata hasara.

فَإِنْ يَصْبِرُوا فَالنَّارُ مَثْوًى لَهُمْ ۖ وَإِنْ يَسْتَعْتِبُوا فَمَا هُمْ مِنَ الْمُعْتَبِينَ {24}

Basi wakisubiri Moto ndio makazi yao. Na wakitoa udhuru hawakubaliwi.