Aya 41 – 46: Ninawaita Kwenye Wokovu Nyinyi Mnaniita Kwenye Moto
Maana
Na Enyi watu wangu! Kwa nini mimi ninawaita kwenye wokovu, nanyi mnaniita kwenye Moto? Mnaniita nimkufuru Mwenyezi Mungu na nimshirikishe na yule ambaye simjui, nami ninawaita kwa Mwenye nguvu Mwingi wa maghufira?
Maneno haya na yanayofuatia mpaka Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaona waja, anayasimulia Mwenyezi Mungu kuhusu mumin anayetoa nasaha.
Maana ni, niambieni enyi washirikina kuhusu hali yangu na nyinyi. Mimi nawalingania kwenye kheri itakayowaokoa na adhabu na maangamizi; ambayo ni kumwamini Mwenyezi Mungu mwenye nguvu asiyekuwa na mfano na yoyote; na mwenye kumsamehe anayetubia na kurejea Kwake; na nyinyi mananiita kwenye adhabu ya kuungua na kwenye shirki asiyoisamehe Mwenyezi Mungu wala kuingia akilini. Haifuati isipokuwa mwenye kupotea njia.
Bila ya shaka mnayeniitia, hastahiki wito duniani wala Akhera.
Bila shaka yule mnayenitaka nimwabudu, kama Firauni na mwenginewe, hana faida yoyote duniani na Akhera:
إِنْ تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ۚ {14}
Na hakika marejeo yetu ni kwa Mwenyezi Mungu.
Kila kiumbe kitarudi kwa Mwenyezi Mungu kesho, sio kwa Firauni wala kwa mwenginewe. Watasimama wote mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya hisabu na malipo na wanaopita kiasi basi hao ndio watu wa Motoni!
Amenukuu Tabari na Razi kutoka kwa Mujahid, kwamba makusudio ya wanaopita kiasi hapa ni waliomwaga damu bila ya haki.
Basi mtayakumbuka ninayowaambia yale ya ukweli na nasaha pale mtakapoona adhabu na kuwashukia balaa Nami namkabidhi Mwenyezi Mungu mambo yangu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaona waja.
Muhyiddin Bin Arabi anasema katika Futuhatil-makkiyya kuwa neno ufawwidhu (tulilolifasiri kwa maana ya kutegemeza), limechukuliwa kutoka neno fadha lenye maana ya kumimina chombo kikiwa kimejaa na hakiwezi kuchukua ziada.
Kwa hiyo mumin akibebeshwa zaidi ya uwezo wake, huipeleka ile ziada kwa Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hupokea ziada hiyo na kumpunguzia mzigo mumin. Na yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi na mwenye kumuona mwenye kuamini na akamtegemea na yule anayeelekea kwingine.
Basi Mwenyezi Mungu akamlinda na ubaya wa hila walizozifanya. Na adhabu mbaya itawazunguka watu wa Firauni.
Firauni alimdhamiria ubaya Musa na mumin mwenye kutoa nasaha, Mwenyezi Mungu akawaokoa na vitimbi vyake, akaangamia Firauni na watu wake kwenye maji. Namna hii Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawaondolea ubaya wenye ikhlasi, na majanga yanawarudia viongozi wa uhaini. Hii ni kabla ya mauti.
Ama baada ya mauti, basi wanaonyeshwa Moto asubuhi na jioni.
Kuna riwaya iliyopokewa kutoka kwa Imam Ja’far Assadiq (a.s.) akisema: Hiyo itakuwa baada ya mauti na kabla ya Kiyama. Kwa sababu siku hiyo haitakuwa na asubuhi wala jioni. Lau angeliadhibiwa mwenye hatia asubihi na jioni tu, basi ingelikuwa afadhali kwake.
Na itapofika Saa ya Kiyama patasemwa: Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali kabisa!
Kila mkosefu ataambiwa Siku ya Kiyama: Ingia Jahannam na ni marejeo mabaya; ni sawa awe ni katika watu wa Firauni au wengineo. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amehusu kutaja Firauni kwa sababu mazungumzo yanamuhusu yeye hivi sasa.
وَإِذْ يَتَحَاجُّونَ فِي النَّارِ فَيَقُولُ الضُّعَفَاءُ لِلَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا إِنَّا كُنَّا لَكُمْ تَبَعًا فَهَلْ أَنْتُمْ مُغْنُونَ عَنَّا نَصِيبًا مِنَ النَّارِ {47}
قَالَ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا إِنَّا كُلٌّ فِيهَا إِنَّ اللَّهَ قَدْ حَكَمَ بَيْنَ الْعِبَادِ {48}
وَقَالَ الَّذِينَ فِي النَّارِ لِخَزَنَةِ جَهَنَّمَ ادْعُوا رَبَّكُمْ يُخَفِّفْ عَنَّا يَوْمًا مِنَ الْعَذَابِ {49}
قَالُوا أَوَلَمْ تَكُ تَأْتِيكُمْ رُسُلُكُمْ بِالْبَيِّنَاتِ ۖ قَالُوا بَلَىٰ ۚ قَالُوا فَادْعُوا ۗ وَمَا دُعَاءُ الْكَافِرِينَ إِلَّا فِي ضَلَالٍ {50}
إِنَّا لَنَنْصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ {51}
يَوْمَ لَا يَنْفَعُ الظَّالِمِينَ مَعْذِرَتُهُمْ ۖ وَلَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ {52}
وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْهُدَىٰ وَأَوْرَثْنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ الْكِتَابَ {53}
هُدًى وَذِكْرَىٰ لِأُولِي الْأَلْبَابِ {54}
فَاصْبِرْ إِنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنْبِكَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ بِالْعَشِيِّ وَالْإِبْكَارِ {55}