Aya 64 – 68: Amewatia Sura Na Akazifanya Nzuri
Ni Mwenyezi Mungu aliyewafanyia ardhi kuwa ni pahala pa kukaa, na mbingu kuwa jengo.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.), hapa, ameisifu ardhi kuwa ni mahali pa kukaa, mahali pengine ameipa sifa ya tandiko na pengine kitanda. Maana yote hayo ni mamoja. Na ameisifu mbingu hapa kuwa ni jengo na mahali pengine kuwa ni sakafu na yenye buruji na yenye mpangilio.
Makusudio ya sakafu ni kufananisha, kwa sababu inaonekana kama hivyo kwenye macho. Kundi la wafasiri limesema kuwa makusudio ya buruji ni nyota na mpangilio. ni njia. Ama makusudio ya jengo ni kuwa aliiumba kwa mpangilio mzuri na akaipamba kwa pambo la nyota; kama ilivyo katika Juz. 23 (37:6).
Na akawatia sura, na akazifanya nzuri sura zenu, na akawaruzuku vizuri. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu. Basi amekuwa na baraka Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemuumba mtu, akalifanya vizuri umbile lake, kimo na viungo, kwa mpangilio wa hali ya juu; kuongezea ubainifu, utambuzi, na mengineyo, kama vile utambuzi n.k. Hali hii ya uwiano wa ajabu baina ya mtu na ulimwengu; kiasi ambacho muundo wake umekuja kwa namna ambayo mtu anaweza kutumia nishati na heri zote zilizo ulimwenguni kulingana na haja na masilahi yake, huenda ndiyo inayomfanya mtu awe kiumbe wa aina yake.
Lau kusingelikuwa na dalili yoyote inayofahamisha kuweko Mwenyezi Mungu, isipokuwa kiumbe huyu wa ajabu (mtu), basi ingelitosha. Hapa ndio tunapokuta tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na katika ardhi zimo Ishara na katika nafsi zenu, je hamuoni?” (51:20-21). Tumeyazungumzia hayo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 15 (17:70).
Yeye yuko hai - hapana mungu isipo kuwa Yeye. Basi muabuduni Yeye mkimsafia Dini Yeye. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.
Yeye yuko hai kwa sababu Ndiye anayetoa uhai na ni Mmoja wa peke Yake kwa sababu ni Mungu. Kwani uungu unapelekea kuwa wa pekee mmoja tu. Maana ya kumsafia dini ni kumwamini na kumwelekea Yeye tu peke Yake, katika kauli zote na vitendo vyote. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:29) na Aya ya 14 ya sura hii tuliyo nayo.
Baada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kusema kuwa Yeye ndiye aliyewatia sura, anaashiria kuwa inatakikana mtu amshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema yake ya kuumba na kuruzuku.
Sema: Hakika nimekatazwa kuwaabudu wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, ziliponijia hoja zilizo wazi kutokana kwa Mola wangu. Na nimeamrishwa nisilimu kwa Mola wa walimwengu wote.
Huu ni mfumo mzuri wa kujadili na kudadisi. Washirikina walipomwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.): abudu masanamu tunayoyaabudu, ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Mtume wake waambie kuwa vipi niabudu masanamu na hali Mwenyezi Mungu amenikataza kuyaabudu na akaniamuru kusalimu amri Kwake Yeye peke yake.
Pia amenifahamisha dalili za kutosha kwamba mnavyoviabudu hav- istahiki kuabudiwa kabisa, kwa sababu ni mawe tu, yasiyodhuru wala kunufaisha. Umetangulia mfano wake katika Aya 41 ya sura hii tuliyo nayo.
Yeye ndiye ambaye amewaumba kwa udongo, kisha kwa tone, kisha kwa pande la damu, kisha akawatoa katika hali ya mtoto mchanga, kisha mpate kufikilia utu uzima, kisha mpate kuwa wazee. Na kati yenu wapo wanaokufa kabla, na ili mfikie muda uliokwishawekwa, na ili mpate kutia akili
Umetangulia mfano wake katika Juz. 14 (16:70), Juz. 17 (22:70), Juz. 18 (23:14) na Juz. 22 (35:11).
Mwanafalsafa Russel Na Muda Uliowekwa
Yeye ndiye ambaye anahuisha na anafisha. Akihukumu jambo liwe, basi huliambia: Kuwa! Likawa.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndiye anayeleta mauti na uhai katika vitu vya asili ya maumbile na Ndiye aliyeleta maumbile yote, zikiwemo sayari zake, kwa neno ‘kuwa’ kutokana na kutokuweko chochote. Sio kutokana na ukungu; wala mengineyo. Kama muulizaji atauliza: Ni nani basi aliyemuumba Mwenyezi Mungu? Tutajibu: maana ya neno Allah (Mwenyezi Mungu) ni kuwa Yeye ni muumba asiyeumbwa na kwamba dhati yake inapelekea kupatikana wala haihitaji mwenye kuipatisha.
Akisema mara ya pili kuwa hayo ni madai tu yanyohitaji uthibitisho, na kwamba huo ukungu huuhitaji mwenye kuupatisha, tutamjibu hivi: Maisha haya na nidhamu hii haiwezi kufasiriwa na ukungu wala na kitu chochote kisichokuwa na uhai wala utambuzi. Kwa sababu asiyenacho haiwezi kuitoa.
Kwa hiyo basi haitabakia kwa mwenye akili kufasiri uhai na nidhamu katika maumbile isipokuwa kukubali kuweko Mwenye uwezo, Mpangiliaji aliyemuumba wa kila kitu na asiyehitajia chochote. Makadirio yoyote yasiyokuwa haya hayakubaliki kiakili.
Na mwenye kupinga basi na alete lililo bora kuliko hili na amwachie mtu kufuata atakalo nasi tutakuwa pamoja naye.
Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemumba mtu katika umbile zuri, akamgurisha kutoka hali moja hadi nyingine mpaka kufikia muda wake uliowekwa. Ikiwa hatujamuona muumba basi tumeona athari na dalili zinazofahamisha kuwa Yeye ni Mkuu katika uumbaji Wake.
Kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘na ili mfikie muda uliokwishawekwa, na ili mpate kufahamu.’ Tunakumbuka tukio lililomtokea mwanafalsafa mkubwa Bretrand Russel, alipokuwa na umri wa miaka 76.
Mnamo mwaka 1948, alisafiri kwa ndege kutoka Oslow hadi London. Ndege ilipokuwa inakurubia ufukwe wa Norway, mhudumu mmoja wa ndege alimuuliza kama ni lazima avute sigara? Alikuwa amekaa kwenye viti vya mbele, akamjibu: “Nisipovuta nitakufa.”
Basi akamuonyesha viti vya nyuma aende akakae huko, ataruhusiwa kuvuta sigara. Mara tu baada ya kukaa, ndege ikaanguka baharini, watu waliokuwa viti vya mbele wakafariki na waliokuwa vya nyuma wakapona.
Hatuwezi kupata tafsiri ya hili ispokuwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘na ili mfikie muda uliokwishawekwa, na ili mpate kufahamu.’ Mwenyezi Mungu ametanabisha kufika muda uliowekwa na kufahamu, ili awaeleze walahidi wanaofasiri tukio kama hili na mfano wake kuwa ni sadfa.
أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِ اللَّهِ أَنَّىٰ يُصْرَفُونَ {69}
الَّذِينَ كَذَّبُوا بِالْكِتَابِ وَبِمَا أَرْسَلْنَا بِهِ رُسُلَنَا ۖ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ {70}
إِذِ الْأَغْلَالُ فِي أَعْنَاقِهِمْ وَالسَّلَاسِلُ يُسْحَبُونَ {71}
فِي الْحَمِيمِ ثُمَّ فِي النَّارِ يُسْجَرُونَ {72}
ثُمَّ قِيلَ لَهُمْ أَيْنَ مَا كُنْتُمْ تُشْرِكُونَ {73}
مِنْ دُونِ اللَّهِ ۖ قَالُوا ضَلُّوا عَنَّا بَلْ لَمْ نَكُنْ نَدْعُو مِنْ قَبْلُ شَيْئًا ۚ كَذَٰلِكَ يُضِلُّ اللَّهُ الْكَافِرِينَ {74}
ذَٰلِكُمْ بِمَا كُنْتُمْ تَفْرَحُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَبِمَا كُنْتُمْ تَمْرَحُونَ {75}
ادْخُلُوا أَبْوَابَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا ۖ فَبِئْسَ مَثْوَى الْمُتَكَبِّرِينَ {76}
فَاصْبِرْ إِنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ ۚ فَإِمَّا نُرِيَنَّكَ بَعْضَ الَّذِي نَعِدُهُمْ أَوْ نَتَوَفَّيَنَّكَ فَإِلَيْنَا يُرْجَعُونَ {77}
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِنْ قَبْلِكَ مِنْهُمْ مَنْ قَصَصْنَا عَلَيْكَ وَمِنْهُمْ مَنْ لَمْ نَقْصُصْ عَلَيْكَ ۗ وَمَا كَانَ لِرَسُولٍ أَنْ يَأْتِيَ بِآيَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّهِ ۚ فَإِذَا جَاءَ أَمْرُ اللَّهِ قُضِيَ بِالْحَقِّ وَخَسِرَ هُنَالِكَ الْمُبْطِلُونَ {78}