read

Aya 18 – 22: Waonye Siku Inayokurubia

Maana

Na waonye siku inayokaribia, wakati nyoyo zitakapofika kooni, nao wamejaa huzuni. Madhalimu hawatakuwa na rafiki, wala mwombezi wa kuitikiwa.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume (s.a.w.) na wanaotakiwa kuonywa ni washirikina wa kiarabu. Maana ni kuwa kazi yako ewe Muhammad ni kuwaonya washirikina na adhabu ya siku ambayo nyoyo zitayeyuka kwa fazaa; ambapo hakutakuwa na rafiki wala mwombezi. Na siku hii iko karibu tu bila shaka itafika.

Mwenyezi Mungu anajua hiyana ya macho na yanayoficha vifua. Na Mwenyezi Mungu huhukumu kwa haki

Hakuna jambo alilolidhamiria mtu au kuliangalia kwa jicho la hiyana, ila Mwenyezi Mungu atakuwa analijua na atalitolea hukumu kesho kwa ilimu yake na uadilifu, kwa kila mhaini mwenye hatia. Hukumu yake itakuwa ya mwisho haina rufaa.

Na wale ambao wanaomba kinyume chake Mwenyezi Mungu hawahukumu chochote.

Makusudio ya kinyume chake ni kila kisichokuwa Mwenyezi Mungu wanchokiabudu watu; iwe ni sanamu, mali, cheo au mengineyo.

Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye Kusikia, Mwenye kuona.

Hii ni ibara nyingine baada ya ile isemayo:

وَأَنَّ اللَّهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا {12}

“Na kwamba Mwenyezi Mungu amekizunguka kila kitu kwa elimu.” (65:12).

Je, hawatembei katika ardhi wakaona vipi ulikuwa mwisho wa waliokuwa kabla yao? Nao walikuwa na nguvu zaidi kuliko wao na athari katika nchi. Na Mwenyezi Mungu aliwakamata kwa sababu ya madhambi yao. Na wala hapakuwa wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu.

Huku ni kutahadharishwa kunakotoka kwa Mwenyezi Mungu kwa wakosefu, kwamba mwisho wao utakuwa kama mwisho wa waliokuwa kabla yao. Walikuwa wengi na wenye mali nyingi, lakini ilipokuja adhabu hawakupata wa kuwasaidia wala wa kuwalinda. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (12:109), Juz. 17 (22:46), Juz. 21 (30:9) na Juz. 22 (35:44).

Hayo ni kwa sababu walikuwa wanawajia Mitume wao kwa hoja zilizo wazi, lakini wakawakataa, ndipo Mwenyezi Mungu akawakamata. Bila ya shaka Yeye ni Mwenye nguvu, Mkali wa kuadhibu.

Yametangulia maelezo mara nyingi, kwamba mwisho wa waliokadhibisha mitume ni kuvunjika na kubomoka. Kesho hakutakuwa na tofauti baina ya waliowakataa mitume na wale waliowamini lakini wakahalifu mafunzo yao na wakazima desturi zao; hata kama duniani watachukuliwa kuwa ni waislamu.

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مُوسَىٰ بِآيَاتِنَا وَسُلْطَانٍ مُبِينٍ {23}

Na kwa hakika tulimtuma Musa pamoja na Ishara zetu na hoja zilizo wazi.

إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَهَامَانَ وَقَارُونَ فَقَالُوا سَاحِرٌ كَذَّابٌ {24}

Kwa Firauni na Hamana na Qaruni. Wakasema: “Ni mchawi, mwongo mkubwa.

فَلَمَّا جَاءَهُمْ بِالْحَقِّ مِنْ عِنْدِنَا قَالُوا اقْتُلُوا أَبْنَاءَ الَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ وَاسْتَحْيُوا نِسَاءَهُمْ ۚ وَمَا كَيْدُ الْكَافِرِينَ إِلَّا فِي ضَلَالٍ {25}

Basi alipowaletea Haki inayotoka kwetu, walisema: ‘Waueni watoto wanaume wa wale waliomuamini na wawacheni hai wanawake wao.’ Na haviwi vitimbi vya makafiri ila katika upotovu.

وَقَالَ فِرْعَوْنُ ذَرُونِي أَقْتُلْ مُوسَىٰ وَلْيَدْعُ رَبَّهُ ۖ إِنِّي أَخَافُ أَنْ يُبَدِّلَ دِينَكُمْ أَوْ أَنْ يُظْهِرَ فِي الْأَرْضِ الْفَسَادَ {26}

Na Firauni akasema: “Niachieni nimuuwe Musa, naye amwite Mola wake! Hakika Mimi nachelea asije kubadilisha dini yenu, au akadhihirisha uharibifu katika nchi.”

وَقَالَ مُوسَىٰ إِنِّي عُذْتُ بِرَبِّي وَرَبِّكُمْ مِنْ كُلِّ مُتَكَبِّرٍ لَا يُؤْمِنُ بِيَوْمِ الْحِسَابِ {27}

Na Musa akasema: Hakika Mimi najikinga kwa Mola wangu na Mola wenu anilinde na kila mwenye kiburi asiyeiamini Siku ya Hisabu.

وَقَالَ رَجُلٌ مُؤْمِنٌ مِنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَكْتُمُ إِيمَانَهُ أَتَقْتُلُونَ رَجُلًا أَنْ يَقُولَ رَبِّيَ اللَّهُ وَقَدْ جَاءَكُمْ بِالْبَيِّنَاتِ مِنْ رَبِّكُمْ ۖ وَإِنْ يَكُ كَاذِبًا فَعَلَيْهِ كَذِبُهُ ۖ وَإِنْ يَكُ صَادِقًا يُصِبْكُمْ بَعْضُ الَّذِي يَعِدُكُمْ ۖ إِنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ مُسْرِفٌ كَذَّابٌ {28}

Na akasema mtu mmoja Muumini, katika watu wa Firauni, anayeficha Imani yake: Mtamuuwa mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Mwenyezi Mungu? Na hali amewajia na hoja zilizo wazi? Na akiwa ni mwongo basi uwongo wake ni juu yake mwenyewe, na akiwa ni mkweli yatawafika baadhi ya hayo anayowaahidi; Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi apindukiaye mipaka, mwongo mkubwa.

يَا قَوْمِ لَكُمُ الْمُلْكُ الْيَوْمَ ظَاهِرِينَ فِي الْأَرْضِ فَمَنْ يَنْصُرُنَا مِنْ بَأْسِ اللَّهِ إِنْ جَاءَنَا ۚ قَالَ فِرْعَوْنُ مَا أُرِيكُمْ إِلَّا مَا أَرَىٰ وَمَا أَهْدِيكُمْ إِلَّا سَبِيلَ الرَّشَادِ {29}

Enyi watu wangu! Leo mna ufalme, mmeshinda katika nchi; basi ni nani atakayetusaidia kutuokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu kama ikitufikia? Firauni akasema: Siwapi rai ila ile niliyoiona, wala siwaongozi ila kwenye njia ya uwongofu.