read

Waliomcha Mola Wao Watapelekwa Peponi Aya 73 – 75

Maana

Na waliomcha Mola wao watapelekwa Peponi kwa makundi, mpaka watakapoifikia, nayo milango yake imekwishafunguliwa, walinzi wake watawaambia: Salaamun Alaikum, (Amani iwe juu yenu!) Mmekua wema. Basi ingieni humu mkae milele.

Wakosefu watapelekwa kwenye Jahannam huku Malaika wa adhabu wakiwasukuma kwa nguvu na kwa udhalili. Wenye takua wanaingia Peponi wakiwa wamezungukwa na Malaika kwa taadhima na takrima na watasema:

Alhamdulillah, (Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu) aliyetutimizia ahadi yake, na akaturithisha ardhi, tunakaa katika Bustani popote tupendapo. Basi ni malipo mazuri yaliyoje ya watendao!

Wanaosema hayo ni waumini. Makusudio ya ardhi hapa ni ardhi ya Peponi. Wataitumia kama vile anavyotumia mrithi, mali aliyoachiwa. Kule duniani waliifanyia kazi Pepo wakitegemea na kuamini aliyoahidi Mwenyezi Mungu kwa wenye takua na subira. Watapoiona watafurahia na kumsifu Mwenyezi Mungu wakijua kuwa ahadi yake ni ya kweli na haki.

Imeelezwa kwenye Nahajul-balagha: “Malaika watawazunguka watu Peponi, watawashukia kwa upole, na watawafungulia milango ya mbingu. Watawaandalia sehemu za heshima alizowafahamisha Mwenyezi Mungu, akaridhia mahangaiko na kusifia makazi yao”1

Na utawaona Malaika wakizunguka pembeni mwa Arshi ya Mwenyezi Mungu, wakimsabihi na kumsifu Mola wao.

Katika Juz. 8 (7:53), tumebainisha, kwa ushahidi wa Qur’ani, kuwa Makusudio ya Arshi ni kuwa amri yote ni ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo maana yake hapa ni kuwa Malaika hawafanyi lolote ila kwa amri ya Mwenyezi Mungu; kama ulivyokuja wasifu wao katika kauli yake Mwenyezi Mungu:

بَلْ عِبَادٌ مُكْرَمُونَ{26}
لَا يَسْبِقُونَهُ بِالْقَوْلِ وَهُمْ بِأَمْرِهِ يَعْمَلُونَ {27}

“Bali hao ni waja waliotukuzwa. Hawamtangulii kwa neno nao wanafanya kwa amri yake.”
Juz. 17 (21:26-27)

Na patahukumiwa baina yao kwa haki na patasemwa Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote!

Yaani muasi hatazidishiwa adhabu, wala mtiifu hatapunguziwa thawabu. Kuna tafsiri nyingine zinazasema kuwa Mwenyezi Mungu alipoanza kuumba alisema: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote.

Baada ya kufa viumbe na kuwafufua na kutulia watu wa peponi atasema: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote, ili awafundishe waja wake adabu yake ya kuanza kila jambo kwa sifa njema na kumalizia kwa sifa njema.

  • 1. Khutba 222