read

Waliomsingizia Uwongo Mwenyezi Mungu Aya 60 – 67

Maana

Na Siku ya Kiyama utawaona wale ambao wamemsingizia uwongo Mwenyezi Mungu nyuso zao zimesawijika. Je! Si katika Jahannamu makazi ya wanaotakabari?

Kila anayemnasibishia Mwenyezi Mungu yale asiyokuwa na ujuzi nayo basi atakuwa amemsingizia Mwenyezi Mungu; iwe amemnasibishia kuwa na washirika, mke na mtoto, au kazi za Mwenyezi Mungu; kama kuingilia utume ukhalifa, hukumu au kutoa fatwa kwa jina la dini.

Aliulizwa Imam Ja’far As-sadiq (a.s.) kuhusiana na maana ya Aya hii, akasema: “Mwenye kudai uimamu usiotokana na Mwenyezi Mungu, atakuwa amemsingizia uongo Mwenyezi Mungu” Muulizaji akasema: Hata kama ni Alawi. Imam akasema: hata kama ni Alawi. Muulizaji akaendelea kuuliza: Hata kama ni Fatimi, Imam akasema: Hata kam ni Fatimi.”

Malipo ya mwenye kumzulia Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ni kufufuliwa akiwa na uso uliosawijika, katika kundi lililoandaliwa Jahannam na Mwenyezi Mungu, makazi mabaya kabisa.

Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘wanotakabari’ baada ya kauli yake ‘wale ambao wamemsingizia Mwenyezi Mungu,’ inaashiria kuwa kumsingizia Mwenyezi Mungu ni kiburi.

Na Mwenyezi Mungu atawaokoa waliona takua kwa ajili ya kufuzu kwao. Hapana uovu utaowagusa, wala hawatahuzunika.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwahadharisha wasingiziaji na moto wa Jahannam, sasa anawabashiria wakweli na wenye takua, kuokoka na moto na kila ubaya. Zaidi ya hayo hawatakuwa na huzuni wala majuto kwa yale waliyoyakosa duniani.

Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu.

Kila kilichoko akiwemo mtu, mnyama mimea na mawe, kinafahamisha kuweko kwa Mwenyezi Mungu kwa sura ya ufundi wa mjengaji kutokana na jengo lenyewe na aliyekitengeneza na kila jingo

Na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu.

Yaani ni mwenye kusimamia, kwa sababu kila kitu kimepatikana kwa uweza wa Mwenyezi Mungu na kitabaki chini ya uangalizi wake mpaka atakapotaka, vinginevyo itakua hakina maana.

Anazo funguo za mbingu na ardhi.

Funguo ni kinaya cha kuwa Mwenyezi Mungu ni mzingatiaji wa ulimwen- gu na ni mjuzi wa yote yanayopita humo kuanzia chembe ndogo hadi sayari kubwa: “Na ziko kwake funguo za ghaibu” Juz. 7 (6:59).

Na wale ambao wamezikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, hao ndio wenye hasara.

Makusudio ya ishara za Mwenyezi Mungu ni ulimwengu na nidhamu yake ya ajabu ambayo lau itakoseka kwa kiasi cha unywele tu, basi utaharabika.
Maana ya kuzikataa ishara za Mwenyezi Mungu ni kutozikubali dalili za nidhamu hii kuwa kuna aliyezipanga na uhandisi na mhandisi wake.

Wakadhibishaji wamezitia hasara akili zao na dalili hizi, kwa sababu zimepofuka na hisia. Vile vile wamezitia hasara nafasi zao na akhera, kwa vile wamezichagulia ukafiri na inadi; na Jahannam yatakuwa ndio makazi ya kila kafiri mwenye inadi.

Sema: Je! Mnaniamrisha nimwabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, enyi majahili?

Kuna mapokezi yanayosema kuwa washirikina walimjia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) na kusema: Tutakupa mali itakayokufanya uwe tajiri zaidi ya wote katika Makka na tutukuoza msichana unayemtaka, kwa sharti ya kuwa uache mwito wako. Ndio ikashuka Aya hii.

Iwe riwaya hii ni sahihi au la lakini inafafanua zaidi Aya hii. Ni vizuri tudokoe maneno yafuatayo kutoka katika makala ya marehemu Mustafa Sadiq Ar-rafii, yenye kichwa cha maneno ‘Dirhamu na dinari’: “Nimewaona baadhi ya mafakihi wakitoa mawaidha na kuwaambia watu halali na haramu, lakini hakika wanawafanyia maskhara vile anavyomfanyia maskhara mwizi anayempa mawaidha mwizi mwingine na kumwambia usiibe.”

Hali hii pia iko kwa waandishi wanasiasa na wengineo wanaobeba nembo za uzalendo na ubinadamu. Ar-rafii anaendelea kusema: “Mwenye kutukuza dirhamu na dinari (pesa) huwa anautukuza unafiki, tamaa na uwongo… Hakika haiba ya Uislamu ni kujitolea maisha sio kupupia maisha, na kuwasaidia waumini sio kuwafanyia uadui. Na utajiri unapimwa kwa inavyofanya kazi mali sio kukusanya mali.”

Na kwa hakika umepewa wahyi na waliokuwa kabla yako: Bila ya shaka ukishirikisha amali zako zitapomoka, na lazima utakuwa miongoni mwa wenye kuhasirika.

Makusudio ya kupomoka (kuanguka) amali ni kukosa thawabu. Kushirikisha ni muhali kwa mitume, lakini kukadiria muhali sio muhali. Zaidi ya hayo ni kuwa kutahadharishwa kitu hakufahamishi kuwa aliyehadharishwa anadhaniwa kuwa atafanya alilohadharishwa.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu hakubali ibada ya yeyote ila ikiwa imetakata na kuwa safi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu. Mwenye kumwabudu Mwenyezi Mungu pamoja na mwingine, basi hastahiki thawabu; hata akiwa ni kama mtume. Tumefafanua kuanguka amali katika Juz. 2 (2:216 – 218), kifungu cha ‘Kupomoka.’

Bali muabudu Mwenyezi Mungu tu, na uwe miongoni mwa wenye kushukuru.

Kwa dhahiri hii ni amri, lakini kwa hakika ni kuelezea kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) haabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu tu wala hamshukuru yeyote asiyekuwa yeye. Imekuja kwa tamko la amri kutanabahisha waja kuwa ibada na shukrani ni lazima iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mmoja tu.

Zaidi ya hayo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) mara nyinyi huwaambia wote kwa kumtuma Mtume wake mtukufu: “Na kwamba elekeza uso wako kwenye dini safi, wala usiwe miongoni mwa washirikina.” Juz. 11 (10:105), “Basi simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa wewe...” Juz. 12 (11:112) na “Na simamisha Swala katika ncha mbili za mchana...” Juz. 12 (11:114).

Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu haki ya kadiri yake kwa sababu wao wamemkataa na kuamini masanamu na pesa.

Na Siku ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kuume.

Hiki ni kinaya cha ukuu wa Mwenyezi Mungu na uweza wake; na kwamba mbingu na ardhi na vyote viliomo baina yake vinanyenyekea amri yake.
Ametakasika na Ametukuka na wanayomshirikisha nayo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametakasika na kila shirki na wanayoyasema kuwa ana mkono wa kuume. Na pia ametakasika na ufananisho wanaomsifu nao majahili.

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَنْ فِي السَّمَاوَاتِ وَمَنْ فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَنْ شَاءَ اللَّهُ ۖ ثُمَّ نُفِخَ فِيهِ أُخْرَىٰ فَإِذَا هُمْ قِيَامٌ يَنْظُرُونَ {68}

Na itapulizwa parapanda, wazimie waliomo mbinguni na waliomo ardhini, ila ambaye Mwenyezi Mungu amemtaka. Kisha itapulizwa mara nyengine. Hapo watainuka wawe wanangojea.

وَأَشْرَقَتِ الْأَرْضُ بِنُورِ رَبِّهَا وَوُضِعَ الْكِتَابُ وَجِيءَ بِالنَّبِيِّينَ وَالشُّهَدَاءِ وَقُضِيَ بَيْنَهُمْ بِالْحَقِّ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ {69}

Na ardhi itang’ara kwa Nuru ya Mola wake, na Kitabu kitawekwa, Na wataletwa Manabii na mashahidi, na patahukumiwa baina yao kwa haki, wala hawatadhulumiwa.

وَوُفِّيَتْ كُلُّ نَفْسٍ مَا عَمِلَتْ وَهُوَ أَعْلَمُ بِمَا يَفْعَلُونَ {70}

Na kila nafsi italipwa kwa yale iliyoyafanya, na Yeye anayajua sana wanayoyatenda.

وَسِيقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا فُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا أَلَمْ يَأْتِكُمْ رُسُلٌ مِنْكُمْ يَتْلُونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِ رَبِّكُمْ وَيُنْذِرُونَكُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَٰذَا ۚ قَالُوا بَلَىٰ وَلَٰكِنْ حَقَّتْ كَلِمَةُ الْعَذَابِ عَلَى الْكَافِرِينَ {71}

Na wale ambao wamekufuru watasukumwa kwenye Jahannamu kwa makundi. Mpaka watakapoifikia itafunguliwa milango yake, na walinzi wake watawaambia: Kwani hawakuwajia Mitume miongoni mwenu wakiwasomea Aya za Mola wenu na kuwaonya kukutana na siku yenu hii? Watasema: Ndio! Lakini limekwisha thibiti neno la adhabu juu ya makafiri.

قِيلَ ادْخُلُوا أَبْوَابَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا ۖ فَبِئْسَ مَثْوَى الْمُتَكَبِّرِينَ {72}

Itasemwa: Ingieni milango ya Jahannamu mdumu humo. Basi ni ubaya ulioje wa makazi ya wanaotakabari.