read

Mwenyezi Mungu Anasamehe Madhambi Yote Aya 53 – 59

Maana

Sema: Enyi waja wangu waliozifanyia israfu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Huu ni mwito wazi, kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa wale waliodhulumu nafsi zao kwa kufanya madhambi na maasi. Akaahidi msamaha kwa kila dhambi kadiri itakavyokuwa kubwa. Kwa hiyo amefungua mlango kwa yule mwenye kutaka kufuta maovu yake yeye mwenyewe na kutengeneza yaliyoharibika.

Kuna Hadith inayosema: “Hakika Mwenyezi Mungu hachoki mpaka mchoke. Mkiacha naye anaacha.” yaani mkiacha toba naye anaacha maghufira. Katika Hadith nyingine Mtume (s.a.w.) anasema: “Hakuna ninachopenda zaidi katika dunia na vilivyomo kuliko Aya hii.” Imekua mashuhuri kauli ya kuwa hii ni Aya yenye matarajio zaidi katika Qur’ani.

Miongoni mwa madhambi makubwa zaidi ni kukata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu:

قَالَ وَمَنْ يَقْنَطُ مِنْ رَحْمَةِ رَبِّهِ إِلَّا الضَّالُّونَ {56}

“Na ni nani anayekata tamaa na rehema ya Mola wake isipokuwa wale waliopotea.” Juz. 14 (15:56).

Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 5 (4:56). Pia tumeweka kifungu maalum cha toba ’Toba na umbile’ katika Juz. 4 (4:17-18)

Na rejeeni kwa Mola wenu, na silimuni kwake, kabla ya kuwajia adhabu. Kisha hapo hamtanusuriwa.

Chukueni fursa enyi wenye dhambi wala msiipoteze. Tubieni kwake na mumfanyie ikhlasi kwa kauli na vitendo.

Na fuateni yaliyo bora zaidi katika yale yaliyoteremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu, kabla haijawajia adhabu kwa ghafla, na hali hamtambui.

Hakuna kitu, katika alivyoviteremsha Mwenyezi Mungu kilicho bora zaidi ya kingine kwake. Kila alichokisema ni kizuri zaidi na adhimu. Ama kwa wenye dhambi basi kitu bora zaidi walichoteremshiwa ni mwito wa toba na kukubaliwa hata ikiwa dhambi ni kubwa kiasi gani. Na yasiyokuwa hayo ni kiaga na hadhari.

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akabainisha matokeo ya atakayepuuza toba; kama ifuatavyo:

Isije ikasema nafsi: Ee masikitiko yangu kwa yale niliyopoteza upande wa Mwenyezi Mungu katika kumtii. Masikitiko ni miongoni mwa adhabu kubwa ya nafsi. Hasa ikiwa hakuna kimbilio wala pa kutokea.

Na hakika nilikuwa miongoni mwa wanaofanya maskhara!

Kesho mwenye madhambi atasema kwa majuto na masikitiko: Sikutosheka na kumwasi Mwenyezi Mungu na kupuuza toba mpaka nikawafanyia masi- hara wanaomtii Mwenyezi Mungu na wenye kuogopa adhabu yake.

Au ikasema: Ingelikuwa Mwenyezi Mungu ameniongoa, bila ya shaka ningelikuwa miongoni mwa wenye takua.
Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Watasema walioshirikisha: Lau angelitaka Mwenyezi Mungu tusingelishirikisha” Juz. 8 (6:148).

Au ikasema inapoona adhabu: Lau kuwa ningelipata kurudi, ningeli kuwa miongoni mwa wafanya mema.

Mfano wake ni:

قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ{99}

لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ ۚ {100}

“Husema Mola wangu nirudishe ili nitende mema badala ya yale niliyoacha” Juz. 18 (23:99-100).

Wapi! Mambo hayako kama unavyotaka zilikwishakujia Ishara zangu, nawe ukazikadhibisha, na ukajivuna, na ukawa miongoni mwa makafiri!

Zilimjia ishara za Mwenyezi Mungu akazikanusha na akasema hazitoki kwa Mwenyezi Mungu. Akafanya kiburi na imani na akamkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha akakadhibisha na akasema: hakuna chochote kilichonijia kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume wake.

Kwa hiyo akachanganya maovu ya kufuru, uwongo na kiburi. Lau angelichukua fursa ya kutubia ingelikuwa hana haja na malalamiko yote haya; na angelikuwa kwenye raha bila ya kuwa na hizaya.

وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ تَرَى الَّذِينَ كَذَبُوا عَلَى اللَّهِ وُجُوهُهُمْ مُسْوَدَّةٌ ۚ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِلْمُتَكَبِّرِينَ {60}

Na Siku ya Kiyama utawaona wale ambao wamemsingizia uwongo Mwenyezi Mungu nyuso zao zimesawijika. Je! Si katika Jahannamu makazi ya wanaotakabari?

وَيُنَجِّي اللَّهُ الَّذِينَ اتَّقَوْا بِمَفَازَتِهِمْ لَا يَمَسُّهُمُ السُّوءُ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ {61}

Na Mwenyezi Mungu atawaokoa walio na takua kwa ajili ya kufuzu kwao. Hapana uovu utao wagusa, wala hawatahuzunika.

اللَّهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ {62}

Mwenyezi Mungu Mungu ndiye Muumba wa kila kitu; na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu.

لَهُ مَقَالِيدُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَالَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ اللَّهِ أُولَٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ {63}

Anazo funguo za mbingu na ardhi. Na wale ambao wamezikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, hao ndio wenye hasara.

قُلْ أَفَغَيْرَ اللَّهِ تَأْمُرُونِّي أَعْبُدُ أَيُّهَا الْجَاهِلُونَ {64}

Sema: Je! Mnaniamrisha nimwabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, enyi majahili?

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِنْ قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ {65}

Na kwa hakika umepewa wahyi na waliokuwa kabla yako: Bila ya shaka ukishirikisha amali zako zitapomoka, na lazima utakuwa miongoni mwa wenye kuhasirika.

بَلِ اللَّهَ فَاعْبُدْ وَكُنْ مِنَ الشَّاكِرِينَ {66}

Bali muabudu Mwenyezi Mungu tu, na uwe miongoni mwa wenye kushukuru.

وَمَا قَدَرُوا اللَّهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ {67}

Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu haki ya kadiri yake. Na Siku ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kuume. Ametakasika na Ametukuka na wanayomshirikisha nayo.