read

Waliokufuru Watasukumwa Aya 68 – 72

Maana

Na itapulizwa parapanda, wazimie waliomo mbinguni na waliomo ardhini, ila ambaye Mwenyezi Mungu amemtaka.

Kupuziwa parapanda ni kinaya cha ukelele. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

يَوْمَ يَسْمَعُونَ الصَّيْحَةَ بِالْحَقِّ ۚ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُرُوجِ {42}

“Siku watakaposikia ukelele kwa haki, hiyo ndiyo siku ya kutoka.” (50:42).

Katika baadhi ya tafsiri imeelezwa kuwa ukelele au mpulizo huu utakaririka mara tatu: Wa kwanza ni ule ilioelezwa katika Aya isemayo:

وَيَوْمَ يُنْفَخُ فِي الصُّورِ فَفَزِعَ مَنْ فِي السَّمَاوَاتِ وَمَنْ فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَنْ شَاءَ اللَّهُ ۚ وَكُلٌّ أَتَوْهُ دَاخِرِينَ {87}

“Na siku itakapopuziwa parapanda, watafazaika waliomo mbinguni na waliomo ardhini, ila amtakaye Mwenyezi Mungu.” Juz. 20 (27:87).

Ambaye Mwenyezi Mungu amemtaka ni yule mwenye takua ambaye umemtangulia wema.

Mpulizo wa pili ni wa mauti ulioashiriwa kwenye Aya hii tuliyo nayo. Na makusudio ya ila ambaye Mwenyezi Mungu amemtaka ni kuwa watu wa ardhini watakufa wote na wa mbinguni hawatabaki isipokuwa ambaye Mwenyezi Mungu atamtaka.

Wafasiri wametofautiana kuhusiana na huyo ambaye Mwenyezi Mungu atamtaka katika wa mbinguni. Ikasemekana kuwa ni Jibril na Israfil. Wengine wakasema ni mashahidi. Mwingine hata akathubutu kusema ni Mwenyezi Mungu – Tunamuomba msamaha Mwenyezi Mungu na tunatubu kwake.

Sio mbali kuwa kusema ila ambaye Mwenyezi Mungu amemtaka, sio hakika bali ni majazi ya kuwa amri siku hiyo ni ya Mwenyezi Mungu peke yake na kwamba:

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ {26}

وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ {27}

“Kila kilichoko juu yake kitatoweka na itabaki dhati ya Mola wako mwenye utukufu na heshima” (55:26-27).

Mpulizo wa tatu ni wa ufufuo amabao amaeuashiria Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kusema: Kisha itapulizwa mara nyengine. Hapo watainuka wawe wanangojea hukumu ya Mwenyezi Mungu kwao.

Kwenye Nahajul-balagha imeelezwa: “Na itapulizwa parapanda, kila chenye uhai kitakufa na kila sauti itakuwa bubu, milima na majabali yataporomoka na mawe yageuke mchanga na iwe tamabarare. Hakutakuwa na muombezi wa kuombea wala ndugu wa kutetea wala udhuru utakaonufaisha.”1

Na ardhi itang’ara kwa Nuru ya Mola wake

Makusudio ya ardhi hapa ni ardhi ya ufufuo na mkusanyiko. Nayo itang’arishwa na nuru ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa sababu yenyewe ni twahara isyokuwa na aina yoyote ya upotevu na ufisadi; haku- na isipokuwa haki na uadilifu.

Na Kitabu kitawekwa, yaani mandishi ya matendo yote:

وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنْشُورًا {13}

“Na Siku ya Kiyama tutamtolea kitabu atakachokikuta kimekunjuliwa.” Juz. 15 (17:13).

Mulla Sadra anasema katika Al-asfar: “Mwenye kutenda kitendo au kusema kauli, athari yake inajitokeza kwenye nafsi yake na moyo wake.

Athari hii inayopatikana kwenye moyo na roho iko kama nakshi na maandishi katika vitabu na mbao. Nyoyo na roho hizo, ambazo zina athari ya vitendo na kauli, kwa lugha ya sharia zinaitwa kurasa za matendo.”

Na wataletwa Manabii na mashahidi, na patahukumiwa baina yao kwa haki, wala hawatadhulumiwa. Na kila nafsi italipwa kwa yale iliyoyafanya, na Yeye anayajua sana wanayoyatenda.

Makusudio ya mashahidi hapa ni manaibu wa mitume katika kufikisha ujumbe wao na desturi zao kwa watu. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu kesho atawafufua watu kwa ajili ya hisabu. Atawaleta manabii wawe mashahidi kwa manaibu wao kuwa wao walichukua ujumbe kwa manabii ili waufikishe kwa watu.
Kisha manaibu nao watatoa ushahidi kuwa wao waliwafundisha watu na waliufikisha ujumbe kwa ukamilifu. Baada ya kupatikana ushahidi wa manabii kwa manaibu na wa manibu kwa watu, hapo Mwenyezi Mungu atawahukumu wote kwa uadilifu bila ya kumpunguzia thawabu mtiifu wala kumzidishia adhabu Muasi.

Yeye anawajua zaidi wote, wakiwemo manabii na mashahidi, kuliko nafsi zao. Amewaita hapa kwa ushahidi kukamilisha hoja na kuondoa visababu vyote.

Tazama Juz. 2 (2:143).

Na wale ambao wamekufuru watasukumwa kwenye Jahannamu kwa makundi. Mpaka watakapoifikia itafunguliwa milango yake.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja, katika Kitabu aina kwa aina ya dhabu ya wakosefu; kama vile: udhalili na utwevu, upofu na kusawijika uso, minyororo na nguo za moto, chakula cha Zaqqum na kinywaji cha usaha na kusukumwa na malaika kupelekwa kwenye Jahannam ili wawe kuni zake. Hao malaika wana miadi nao ya kuwangoja, ndio maana watakuta milango tayari iko wazi.

Na walinzi wake watawaambia: Kwani hawakuwajia Mitume miongoni mwenu wakiwasomea Aya za Mola wenu na kuwaonya kukutana na siku yenu hii?

Makusudio ya swali hili ni kutahayariza na kwamba wao ndio waliojichagulia mwisho huu mbaya.

Watasema: Ndio! Lakini limekwishathibiti neno la adhabu juu ya makafiri.

Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَقَالُوا لَوْ كُنَّا نَسْمَعُ أَوْ نَعْقِلُ مَا كُنَّا فِي أَصْحَابِ السَّعِيرِ {10}

فَاعْتَرَفُوا بِذَنْبِهِمْ فَسُحْقًا لِأَصْحَابِ السَّعِيرِ {11}

“Na watasema: lau tungelikuwa tunasikia au kutia akilini, tusingelikuwa katika watu wa Motoni! Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa motoni!” (67:10-11).

Itasemwa: Ingieni milango ya Jahannamu mdumu humo.

Basi ni ubaya ulioje wa makazi ya wanaotakabari kwenye haki na kutoka kwenye uadilifu.

Lau kusingelikuwa na dalili nyingine ya kuandaliwa Jahannam isipokuwa kwa wenye kiburi, mataghuti, wafisadi na wapotevu tu, ingelitosha. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ {145}

“Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka ya chini motoni. Juz. 5 (4:145)

Akasematena:

إِنَّ جَهَنَّمَ كَانَتْ مِرْصَادًا {21}

لِلطَّاغِينَ مَآبًا {22}

“Hakika Jahannam inangojea. Ni marejeo kwa wenye kupetuka mipaka” (78:21-22).

Huko nyuma tumewahi kusema kuwa lau kusingeliku na mahakama, huko akhera, ya kisasi cha aliyedhulimiwa kwa dhalimu, basi ingelikuwa aliyeuliwa kidhulma ana hali mbaya zaidi ya aliyemuua.

Tazama Juz. 11 (10:3-4) kifungu cha: ‘malipo ni lazima.’

وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا سَلَامٌ عَلَيْكُمْ طِبْتُمْ فَادْخُلُوهَا خَالِدِينَ {73}

Na waliomcha Mola wao watapelekwa Peponi kwa makundi, mpaka watakapoifikia, nayo milango yake imekwishafunguliwa, walinzi wake watawaambia: Salaamun Alaikum, (Amani iwe juu yenu!) Mmekua wema. Basi ingieni humu mkae milele.

وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي صَدَقَنَا وَعْدَهُ وَأَوْرَثَنَا الْأَرْضَ نَتَبَوَّأُ مِنَ الْجَنَّةِ حَيْثُ نَشَاءُ ۖ فَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ {74}

Na watasema: Alhamdulillah, (Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu) aliyetutimizia ahadi yake, na akaturithisha ardhi, tunakaa katika Bustani popote tupendapo. Basi ni malipo mazuri yaliyoje ya watendao!

وَتَرَى الْمَلَائِكَةَ حَافِّينَ مِنْ حَوْلِ الْعَرْشِ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ ۖ وَقُضِيَ بَيْنَهُمْ بِالْحَقِّ وَقِيلَ الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ {75}

Na utawaona Malaika wak- izunguka pembeni mwa Arshi ya Mwenyezi Mungu, wakimsabihi na kumsifu Mola wao. Na patahukumiwa baina yao kwa haki na patasemwa: Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote!
  • 1. Khutba: 195