read

Aya 47 – 55: Wanahojiana Motoni

Maana

Aya hizi zimekwishatangulia kimaneno na kimaana. Kwa hiyo tutazifasiri kwa kupitia tu na tutaashiria Aya zilizotangulia zilipo: Na watapohojiana huko Motoni, wanyonge – yaani wafuasi – watawaambia wale waliotakabari: - yaani waliofuatwa - Hakika sisi tulikuwa wafuasi wenu, basi je, mtatuondolea sehemu ya huu Moto?

Mtu huko Akhera atakuwa pamoja na aliyempenda duniani na akamtii. Mwenye kuwapenda waongofu hapa duniani, atakuwa pamoja nao katika neema ya Pepo na atawashukuru kwa kupata uwongofu kwenye njia ya amani na uwokofu.
Lakini yule atakayewafuata mataghuti, basi atawalaani kesho na atawaambia nyinyi ndio sababu ya uovu wangu, sasa je, mtanipunguzia adhabu ninayoipata.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (14:21).

Watasema waliotakabari: Hakika sote sisi tumo humo humo! Hakika Mwenyezi Mungu amekwishahukumu baina ya waja!

Waliofuatwa watawajibu wale waliowasikiza na kuwatii: Leo hapana mjadala wala maneno. Mwenyezi Mungu amekwishaihukumu kila nafsi kwa kila ilichokichuma, na amekwishatuhukumia sisi na wale waliotufuata kwenda motoni

Na walio Motoni watawaambia walinzi wa Jahannamu: Mwombeni Mola wenu atupunguzie siku moja ya adhabu.

Wanafikiria adhabu ya Jahannam ni kama jela ya duniani, wafungwa wanavyopata mapumziko nje ya jela. Hapo wataomba wafanyiwe motoni kama wanavyofanyiwa katika jela ya duniani.

Watasema: Je! Hawakuwa wakiwafikia Mitume wenu kwa hoja zilio wazi? Watasema: Kwani? Watasema: Basi ombeni! Na maombi ya makafiri hayawi ila ni kupotea bure.

Walinzi watawajibu kuwa Mwenyezi Mungu amekwishamaliza udhuru kwenu, kupitia mitume yake; kama mlivyokiri wenyewe. Kwa hiyo hakuna lawama ikiwa hatajibu maombi yenu ila mjilaumu wenyewe tu. Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii tuliyo nayo (39:71) na kwa upana zaidi kwenye Juz. 7 (7:50-53).

Hakika tunawanusuru Mitume wetu na wale ambao wameamini katika uhai wa duniani na siku wataposimama mashahidi.

Siku ya mashahidi ni Siku ya Kiyama ambapo wakasofu watatolewa ushahidi na malaika maulama wanaofikisha na hata viungo vya mkosaji:

حَتَّىٰ إِذَا مَا جَاءُوهَا شَهِدَ عَلَيْهِمْ سَمْعُهُمْ وَأَبْصَارُهُمْ وَجُلُودُهُمْ بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {20}

“Hata watakapoufikia Moto yatawashuhudia masikio yao, na macho yao na ngozi zao kwa waliyokuwa wakiyatenda.” (41:20).

Aya hii inafahamisha, kwa uwazi, kuwa Mwenyezi Mungu anawanusuru mitume na waumini wenye ikhlasi kuwa washindi duniani na Akhera. Ushindi wa Akhera uko wazi, lakini ushindi wa duniani una sura mbali mbali.

Unaweza ukawa ni nguvu ya kumshinda adui au kuenea itikadi na misingi au hata kuinuka jina na kuwa na shani daima. Kuna baadhi ya mashahidi, makaburi yao yamekuwa kama Al-Ka’aba, yanatembelewa na mamilioni. Historia ni shahidi wa hayo.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (22: 38-41) kifungu cha ‘MwenyeziMunguhuwakingawalioamini.

Siku ambayo hautawafaa madhalimu udhuru wao, nao watapata laana, na watapata makazi mabaya, pasipokuwa na wa kuwakinga wala udhuru utakaowafaa waasi. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekata nyudhuru zote. Na mwema ni yule asiyetaka udhuru kwa kufanya matendo mema.

Na kwa hakika tulimpa Musa uwongofu, na tukawarithisha Wana wa Israili Kitabu, ni Uwongofu na Ukumbusho kwa wenye akili.

Makusudio ya uwongofu hapa ni miujiza inayofahamisha utume wa Musa (a.s.) na yale aliyopewa wahyi, ya halali na haramu. Makusudio ya Kitabu ni Tawrat ya kweli.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja kuwa anawanusuru mitume na waumini, hapa anaashiria Musa na wale waliokuwa na ikhlasi katika wana wa Israil. Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwanusuru na Firauni na watu wake.

Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli.

Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.), akiamrishwa kuvumilia, kama walivyovumilia mitume ulul-azm na kuashiria ahadi Yake aliyoieleza katika kauli yake:

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ {33}

Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokwa washirikina wamechukia.” Juz. 10 (9:33).

Ahadi ya Mwenyezi Mungu haiwezi kuachwa.

Na omba maghufira kwa dhambi zako.

Amri ya kuomba msamaha wa dhambi haimaanishi kuwa kuna dhambi. Mtume alimuomba Mola wake ahukumu kwa haki, ingawaje anajua kuwa hahukumu isipokuwa haki:

قَالَ رَبِّ احْكُمْ بِالْحَقِّ ۗ {112}

“Akasema: Mola wangu! Hukumu kwa haki.” Juz. 17 (21:112).

Unaweza kuuliza: Kuna faida gani basi ya kufanya istighfari ya dhambi? Jibu: Hakuna isipokuwa ibada; kama amri ya tahalili, takbira na tasbih, kama alivyosema:

Na umsabihi Mola wako kwa kumhimidi jioni na asubuhi.

Neno jioni limefasiriwa kutokana na neno la kiarabu ibkar lenye maana ya kuanzia kupinduka jua hadi usiku. Na asubuhi kutoka Ashiyy lenye maana ya kuanzia Alfajiri hadi mchana.

Zaidi ya hayo ni kuwa kuamrishwa Mtume kuomba msamaha na hali hana dhambi, kunafahamisha kuwa kutubia wenye dhambi ni bora zaidi.

Aina hii ya maneno inaitwa kuuashiria mlengwa. Kwa sababu anayesikiliza atatambua kuwa hukumu inayothibiti kwa anayeatamkiwa inathibiti kwa aliyenyamaziwa vile vile, kwa kiasi cha kusikia tu.

Mwenyezi Mungu Na Waisrail

Katika Juz. 1 (2:40-46) tulisema kuwa maana ya neno Israil ni Abdallah (mtumishi wa Mwenyezi Mungu), kwa kutegemea wafasiri, akiwemo Tabariy, Razi na mwenye Majmaul-bayan.

Lakini tulipoanza Juzuu hii tuliyo nayo, tukaona kuwa kauli hii inahitaji uthibitisho na kwamba haikufaa kutegemea kauli za wafasiri, au angalau tungelitegemeza kauli kwa msemaji (kusema kuwa Fulani ndiye aliyesema hivi); kama inavyotakikana katika mantiki ya elimu. Lakini kuwategemea wajuzi hasa waliotangulia, lilikuwa na linaendelea kuwa ni tatizo la waaandishi na watunzi na hata wapokezi wa Hadith.

Basi nikawa natafuta kitabu Talmud, lakini sikupata, badala yake nikapata kitabu: Treasure provision in the rules of the Talmud na Kamusi ya Kitabu (Bible Dictionary), nikavinunua. Waliochangia kutengeneza kamusi hii ni wasomi wa kikiristo 28, wakiwemo makasisi 17, na wengine ni madokta, mashemasi na waalimu. Humo kuna nukuu hii: "Israil: Maana ya neno hili ni yule anayepigana jihadi na Mwenyezi Mungu au aliyepigana miereka na Mwenyezi Mungu. Hilo ni jina la Yakobo alilopewa na Mungu aliyepigana naye hadi alfajiri" (Biblia Mwanzo 32:28).
Kwa hiyo maana ya Israil ni yule anayepigana miereka na Mwenyezi Mungu, kwa nukuu ya Tawrat. Kuna tofauti kubwa baina ya mja au mtu- mishi na mpiganaji. Kwa sababu mpiganaji anapigana na yule aliyefanana naye, lakini mtumishi anakuwa mnyonge.

Hii inatubainikia kuwa Tawrat ya sasa sio ile aliyoiashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliposema: 'Na tukawarithisha wana wa Israil Kitabu ni uwongofu na ukumbusho' kwa sababu Tawrat ya sasa ni ya matamanio na upofu, kwa vile inasema kuwa Ya'qub alipigana na Mungu mpaka Alfajiri, Lut alilala na mabinti zake mpaka akazaa nao na Daud naye aliwapora wake za watu na kuwaua waume zao.

Watafiti wamekongamana kuwa Tawrat iliyoko sasa, iliandikwa baada ya Musa kwa muda mrefu. Tazama Qamusul-kitabul-muqaddasa (kamusi ya kitabu kitakatifu ya kiarabu), ukurasa 763 na 1120 chapa ya Al-injilya ya Beirut 1964. Vile vile Al-asfarul-muqaddasa,' (Vitabu vitakatifu) cha Abdul-wahid Wafi, ukurasa 16 chapa ya kwanza 1964.

Vile vile imetubainikia kuwa wana wa Israil wa mwanzo waliorithishwa Kitabu, wako mbali sana kinasabu na kushabihiana na dola ya Israil, kambi mpya ya ukoloni mashariki ya kati.

Jarida la A-Majalla la Misr la mwezi January 1970, limechapisha makala yenye kurasa 20, kwa anuani ya 'Tawrat ya Mayahudi' ya mwandishi Hussein Dhul-fiqar Sabri.

Ndani ya makala hiyo kuna mahali anamnukuu Mzayuni Stehr, kwamba Mungu wa Israil, kama inavyoona fikra ya Kiyahudi, ana mfungano na historia ya wana wa israil. Ikiondoka Israil, basi dalili za kufahamisha kuweko Mungu nazo zitakuwa zimeondoka. Kwa hiyo inamlazimu kila myahudi apamabane na dhati hiyo isiyojulikana - yaani Mwenyezi Mungu - mpaka alfajiri, kama alivyofanya Ya'qub, iwe mapambano haya ni ya kushindwa au kushinda.

Vile vile mwandishi amemnukuu mzayuni, Popper, kwamba maana yaliyo katika akili za mayahudi wengi ni kuwa Ya'qub alikuwa na nguvu kuliko Mwenyezi Mungu.

Mwisho, baada ya utafiti wa kina wa mwandishi huyu, akatoka na natija aliyoipata kutoka Tawrat na vitabu vingine vya kiyahudi na pia kutoka katika kauli za wanafikra wa kizayuni, kwamba kiini cha itikadi ya kiza- yuni ni kuweko Israil na kupambana na tishio lolote, hata kama chimbuko la tishio hilo ni Mungu. Na kwamba Tawrat ya sasa ni uchambuzi tu wa uyahudi na kupingana na Mwenyezi Mungu. Yeye yuko pamoja nao na wakati huohuo yuko dhidi yao, katika Tawrat yao Mungu amechanganyika: hatakikani, lakini pia ni mwenye huruma.

Huu ndio Uzayuni. Itikadi yake ni kuwa kuna watu wana nguvu zaidi ya Mwenyezi Mungu, na kwamba kuweko Mungu kunategemea kuweko Israil. Ikiondoka Israil Mungu naye ameondoka.

Ndio maana Uzayuni ukajiunga na ukoloni wa kimataifa, dhidi ya mataifa mengine, dini na ubinadamu kwa ujumla. Matokeo ya muungano huu yakawa ni kupatikana Israil, ndani ya ardhi ya Palestina. Lakini Alhamdulillah, roho ya uadui dhidi ya ukoloni na uzayuni imeenea kwenye miji yote ya kiarabu. Dalili kubwa ya hilo ni mapambano ya Wapalestina na kukubaliana waarabu kuisaidia Palestina. Kwa uweza wa Mwenyezi Mungu, matunda yatapatikana, kama si leo ni kesho.

إِنَّ الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِ اللَّهِ بِغَيْرِ سُلْطَانٍ أَتَاهُمْ ۙ إِنْ فِي صُدُورِهِمْ إِلَّا كِبْرٌ مَا هُمْ بِبَالِغِيهِ ۚ فَاسْتَعِذْ بِاللَّهِ ۖ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ {56}

Hakika wale ambao wanabishana katika Ishara za Mwenyezi Mungu bila ya dalili yoyote iliyowafika, hawana vifuani mwao ila kutaka ukubwa tu, na wala hawaufikii. Basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu; hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.

لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ {57}

Hakika umbo la mbingu na ardhi ni kubwa zaidi kuliko umbo la watu. Lakini watu wengi hawajui.

وَمَا يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَلَا الْمُسِيءُ ۚ قَلِيلًا مَا تَتَذَكَّرُونَ {58}

Na kipofu na mwenye kuona hawawi sawa; na walioamini na watendao mema hawawi sawa na muovu. Ni machache mnayoyakumbuka.

إِنَّ السَّاعَةَ لَآتِيَةٌ لَا رَيْبَ فِيهَا وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يُؤْمِنُونَ {59}

Hakika Saa, itafika, haina shaka, lakini watu wengi hawaamini.

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ {60}

Na Mola wenu amesema: Niombeni nitawaitikia. Kwa hakika wale ambao wanajivuna kufanya ibada yangu wataingia Jahannamu wadhalilike.

اللَّهُ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ اللَّيْلَ لِتَسْكُنُوا فِيهِ وَالنَّهَارَ مُبْصِرًا ۚ إِنَّ اللَّهَ لَذُو فَضْلٍ عَلَى النَّاسِ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَشْكُرُونَ {61}

Mwenyezi Mungu ambaye amewafanyia usiku ili mpate kutulia humo, na mchana wa kuonea. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye fadhila juu ya watu, lakini watu wengi hawashukuru.

ذَٰلِكُمُ اللَّهُ رَبُّكُمْ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ {62}

Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu, Muumba wa kila kitu. Hapana mungu ila Yeye; basi mnageuzwa wapi?

كَذَٰلِكَ يُؤْفَكُ الَّذِينَ كَانُوا بِآيَاتِ اللَّهِ يَجْحَدُونَ {63}

Hivyo ndivyo walivyogeuzwa wale ambao walikuwa wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu.