Aya 100: Wingi Wa Mwovu
Maana
Aya hii inarudufu Aya ile isemayo:
لَا يَسْتَوِي أَصْحَابُ النَّارِ وَأَصْحَابُ الْجَنَّةِ ۚ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ هُمُ الْفَائِزُونَ {20}
Wingi wa habithi ni anayoyamiliki miongoni mwa jaha na mali. Mwenye akili hawezi kumweka sawa habithi, na mwema hata kama ana mali nyingi na jaha kubwa. Kwa sababu jaha na mali hazimfanyi mwovu kuwa mwema; wala ufakiri na udhaifu haumfanyi mwema kuwa mwovu.
Mtu habith katika kipimo cha dini ni yule anayeasi hukumu za Mwenyezi Mungu katika kitabu chake na Sunna za Mtume wake. Na katika desturi ya watu ni yule wanayemhofia kwa shari yake na wasiyemwamini kwa jambo lolote na kutomsadiki katika kauli au vitendo vyake. Kimsingi ni kwamba mwenye sifa hizi, ni mbaya pia mbele ya Mwenyezi Mungu. Mtume wa Mwenyezi Mungu anasema: "Utukufu zaidi wa imani ni kuaminiwa na watu."
Ama mtu mwema ni yule aliye kinyume cha mtu habithi katika sifa zake zote.
Je Riziki Ni Bahati Au Majaaliwa?
Unaweza kuuliza: Ikiwa habithi anachukiwa na Mwenyezi Mungu na mwema anaridhiwa na Mwenyezi Mungu, kwa nini basi habithi anafaulu katika maisha haya na kuneemeshwa kwa jaha na utajiri, na mwema anaanguka na wala hapati matakwa yake.
Jibu: Maisha yana desturi na kanuni zinazokwenda nayo, na hazigeuki kwa hali yoyote ile. Kwa sababu hisia na uoni unakataa mkorogano katika ulimwengu. Desturi na kanuni hizi ni katika matengenezo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: Kwa sababu yeye ni muumbaji wa asili na vilivyomo katika asili.
Kimsingi ni kuwa desturi ya kawaida ya tabia inakataa kuwa mali, afya na ilimu, vishuke tu kutoka mbinguni. Isipokuwa vitu hivi na mfano wake vinakuja kwa njia zake na sababu zake za kimaumbile. Elimu inatokana na kujifundisha, afya inatokana na lishe na kinga, na mali inatokana na kazi. Kwa hiyo mwenye kujifunza hujua, mwenye kujiepusha na visababishi vya maradhi husalimika, mwenye kujinyonga atakufa tu; awe mwema au mwovu, mumin au kafiri.
Kwa hiyo wema au imani hauoteshi ngano wala hauponeshi ugonjwa wala haumfanyi asiyejua kuwa mjuzi. Yote haya na mfano wake yanakwenda kwa desturi ya tabia na desturi ya tabia inakwenda kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu, hilo halina shaka.
Kwa sababu yeye ndiye aliyejaalia kujifundisha ndio sababu ya elimu na kujikinga ndio sababu ya afya na kupanda kuwa ndio sababu ya kuvuna. Yeye ni Muumba wa kila kitu na kwake yeye ni mwishilio wa kila jambo.
Ndiyo! kuchuma mali kuna njia nyingi, na milango mingi, nyingine Mwenyezi Mungu amezihalalisha na nyingine akaziharamisha. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehalalisha biashara, kilimo na viwanda; na akaharamisha riba, utapeli, rushwa, kupora na ulanguzi.
Mwenye kuchuma mali kwa njia ya halali hunasibishwa chumo lake kwake, kwa sababu yeye amejitahidi na kufanya bidii kuitafuta, na vilevile hunasabishwa kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu yeye ndiye aliyepitisha sababu hizi na kuzihalalisha kwa kila azitakaye, awe mwema au mwovu.
Ama mwenye kuchuma mali kwa njia za haramu; kama vile riba na unyang'anyi; chumo lake litanasibishwa kwake na kwa hali aliyoitumia, wala halinasibishwi kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ameharamisha njia hizi kwa mwema na mwovu.
Utasema: Haya yote ni kweli, lakini hayajibu swali wala hayatatui mushkeli. Tumewahi kumuona mwema na mwovu wote wakifuata njia za sharia za riziki, na kuzitafuta riziki kwa njia zile alizozihalalisha Mwenyezi Mungu na kuziharamisha, lakini pamoja na hayo, riziki inakuwa zaidi kwa mwovu aliye habith na kuwa dhiki kwa mwema, pengine huyu mwema ametoa juhudi maradufu ya yule mwovu, bali mara nyingine riziki humjia mwovu bila ya kutazamia wala maandalizi au juhudi, na inazuilika kumwendea mwema anapoitazamia na kuifanyia maandalizi na juhudi.
Jibu: Baadhi ya watu wanakimbilia kulifasiri hilo kwa kusema ni sadfa au bahati. Hakuna kinachofahamika kutokana na maelezo hayo zaidi ya kushindwa kwao kutoa tafsiri sahihi. Vinginevyo wasingelikimbilia kwenye maelezo ya kubahatisha tu.
Kwa hiyo sisi tunapinga Sadfa na bahati na tunaamini kwa imani ya mkato kwamba kuna chaguo la juu linajiingiza kwa sababu tusizozijua. kwa vile elimu katika masuala hayo na mfano wake, bado ni changa. Na kushindwa kwa elimu hakumaanishi kuwa kitu hakiko. Imani yetu hii inatiliwa mkazo na kauli zake Mwenyezi Mungu zifuatazo:
وَاللَّهُ فَضَّلَ بَعْضَكُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ فِي الرِّزْقِ ۚ {71}
"Mwenyezi Mungu hukunjua riziki kwa amtakaye na huidhikisha (13:26) Aya hii imekuja kwa herufi zake katika 17:30, 28:82, 29:62, 30:37, 34: 36, 34:39, 39:52, 42:12.
Kwa hiyo basi aliyesema au anayesema: Mwenyezi Mungu amemtajirisha fulani kwa kuwa yeye ni mwema basi atakuwa anazungumza mantiki ya Firaun na kupima kwa kipimo cha Shetani. Hekima yake Mwenyezi Mungu Mtukufu imetaka kumlipa mwema malipo mazuri na kumwadhibu mwovu katika akhera inayobakia sio katika hii dunia inayokwisha. Hii ni Nyumba ya matendo na ile ni Nyumba ya Hisabu.
Zaidi ya haya ni kuwa wingi wa mali wa mwovu huenda ukawa ni balaa kwake na sababu ya kuadhibiwa kwake. Mwenyezi Mungu anasema:
ذَرْهُمْ يَأْكُلُوا وَيَتَمَتَّعُوا وَيُلْهِهِمُ الْأَمَلُ ۖ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ {3}
يَتَمَتَّعُونَ وَيَأْكُلُونَ كَمَا تَأْكُلُ الْأَنْعَامُ وَالنَّارُ مَثْوًى لَهُمْ {12}
Kwa ufupi ni kwamba riziki inategemea mambo mawili. Kuhangaika na matakwa ya Mwenyezi Mungu. Asiyehangaika ataishi omba omba; na mwenye kuhangaika Mwenyezi Mungu humruzuku kutokana na bidii yake, akitaka humpa nyingi na akitaka humpa chache.
Uhakika huu umo katika maumbile ya binadamu na anaufanya bila ya kujitambua. Mfanyi biashara humwomba Mwenyezi Mungu (s.w.t) amruzuku kupata soko zuri la bidhaa zake na watu wazikubali. Mkulima anamwomba Mungu aiteremshie mimea yake mvua; wala hamuombi kumwoteshea mimea bila ya mvua.
Mimi hapa namwomba Mwenyezi Mungu ampe tawfiq mwanangu katika masomo yake na kufaulu mtihani; wala si mwombi akipe mawazo chuo kikuu kimpatie shahada bila ya kusoma na kufanya mtihani. Iko methali isemayo: Mgaaga na upwa hali wali mkavu
Pengine inawezekana mahangaiko yasiambulie kitu, lakini pamoja na hayo inatakikana kupanga mipango na kuongeza juhudi. Kwa sababu kuongeza juhudi, kutumia mipango, na kuvumilia tabu ni sababu ya matakwa ya kufaulu kutoka kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَسْأَلُوا عَنْ أَشْيَاءَ إِنْ تُبْدَ لَكُمْ تَسُؤْكُمْ وَإِنْ تَسْأَلُوا عَنْهَا حِينَ يُنَزَّلُ الْقُرْآنُ تُبْدَ لَكُمْ عَفَا اللَّهُ عَنْهَا ۗ وَاللَّهُ غَفُورٌ حَلِيمٌ {101}
قَدْ سَأَلَهَا قَوْمٌ مِنْ قَبْلِكُمْ ثُمَّ أَصْبَحُوا بِهَا كَافِرِينَ {102}