Aya 1 – 3: Kuumba Mbingu Na Ardhi
Maana
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi na akafanya giza na mwangaza.
Aya zote hizi tatu ni Aya za kilimwengu zinazofahamisha umoja wake na ukuu wake Mwenyezi Mungu. Aya ya kwanza inaashiria kuumbwa mbingu na ardhi na giza na mwangaza. Ya pili, inaashiria kuumbwa mtu na kufufuliwa kwake baada ya kufa.
Na ya tatu, kuenea ujuzi wake kwa kila kitu. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu," anakusudia kufundisha; yaani semeni sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu (Alhamdulillah).
Kumsifu Mwenyezi Mungu ni kuzuri katika hali zote; hata wakati wa madhara. Kwa sababu yeye ndiye afaaye kutukuzwa na kuadhimisha. Ukipatwa na msiba na ukasema Alhamdulillah basi hapo unazingatiwa kuwa mvumilivu (mwenye subira) juu ya shida, na imani yako ni yenye nguvu iliyokita ambayo haiyumbishwi na chochote. Uzuri wa Alhamdulillah unatiliwa mkazo wakati wa furaha na kuondolewa balaa.
Kwa sababu ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa aliyoneemesha.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amejitaja kuwa ndiye Muumbaji wa mbingu na ardhi na giza na mwangaza ili azizindue akili kwamba Yeye hana mshirika katika uumbaji na Uungu. Kwa hiyo anakuwa Yeye peke yake ndiye mwenye kustahiki kusifiwa na kufanyiwa ikhlasi katika kuabudiwa.
Tena wale waliokufuru wanamlinganisha Mola wao (na wengine).
Ajabu ya maajabu ni kwamba ulimwengu huu pamoja na ardhi yake na mbingu yake, na ubainifu huu ulio wazi na dalili mkato, bado hazikuliondoa giza zito kwenye akili ya mshirikina na kwenye moyo wake mpofu wa haki, na akaleta picha kuwa kuna mwingine mwenye kulingana sawa na Mwenyezi Mungu katika kustahiki kusifiwa na kuabudiwa.
Yeye ndiye aliyewaumba kwa udongo.
Yaani ameumba asili yenu, Adam kutokana na mchanga na maji. Au ameumba mada ya kila mtu kwa udongo, kwa sababu mtu anatokana na nyama na damu; na hivyo viwili vimetokana na mmea na nyama ya mnyama aliyetokana na mmea; na mmea nao umetokana na udongo.
Kisha akapitisha muda; na muda maalum uko kwake.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemwekea kila mtu muda (ajali) mara mbili: Wa kwanza, unaisha kwa kufa kwake, hapo hujulikana ameishi muda gani. Pili, ni kurudishwa na kufufuliwa kwake baada ya kufa. Ujuzi wa muda huu uko kwa Mwenyezi Mungu peke yake wala haujui yeyote katika viumbe vyake; kama lilivyofahamisha neno 'uko kwake.'
Tena nyinyi mnatia shaka.
Yaani, baada ya kuweko dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu katika kuumba kukubwa, ambako ni ulimwengu, na katika kuumba kudogo ambako ni kuumba mtu na kufa kwake na kufufuliwa kwake. Baada ya haya yote mnatia shaka katika kuweko Mwenyezi Mungu, umoja wake na utukufu wake!
Tafsir bora ya jumla hii ni kauli ya Amirul-muminin Ali (a.s.): "Namwonea ajabu anayemtilia shaka Mwenyezi Mungu naye anaona kuumba kwa Mwenyezi Mungu; ninamwonea ajabu anayesahau mauti naye anayaona mauti; na ninamstaajabia anayepinga kufufuliwa kwa mwisho naye anaona kufufuliwa kwa kwanza."
Na yeye ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini; anaijua siri yenu na dhahiri yenu na anayajua mnayoyachuma.
Katika Aya ya kwanza Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja kwamba yeye ni Muumbaji wa mbingu na ardhi. Natija ya hayo ni kuwa yeye yuko mbinguni na ardhini; na maana ya kuweko humo ni kuweko athari zake. Katika Aya ya pili ametaja kuwa yeye ndiye Muumba wa binadamu, na atakayemfisha na atakayemfufua. Linalolazimiana na hilo ni kwamba Yeye ni Mjuzi wa anayoyaficha binadamu na anayoyadhihirisha na anayoyachuma katika imani na ukafiri, ikhlasi na unafiki na vilevile vitendo vinavyomrudia yeye vya kheri au shari.
وَمَا تَأْتِيهِمْ مِنْ آيَةٍ مِنْ آيَاتِ رَبِّهِمْ إِلَّا كَانُوا عَنْهَا مُعْرِضِينَ {4}
فَقَدْ كَذَّبُوا بِالْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُمْ ۖ فَسَوْفَ يَأْتِيهِمْ أَنْبَاءُ مَا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ {5}
أَلَمْ يَرَوْا كَمْ أَهْلَكْنَا مِنْ قَبْلِهِمْ مِنْ قَرْنٍ مَكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ مَا لَمْ نُمَكِّنْ لَكُمْ وَأَرْسَلْنَا السَّمَاءَ عَلَيْهِمْ مِدْرَارًا وَجَعَلْنَا الْأَنْهَارَ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهِمْ فَأَهْلَكْنَاهُمْ بِذُنُوبِهِمْ وَأَنْشَأْنَا مِنْ بَعْدِهِمْ قَرْنًا آخَرِينَ {6}