Aya 101-102: Msiulizeulize Mambo
Maana
Enyi Mlioamini! Msiulize mambo ambayo mkidhihirishiwa yatawachukiza.
Kauli yake Mwenyezi Mungu 'Msiulize' inaishiria kuwa baadhi ya Masahaba walikuwa waking’ang’ania kuuliza mambo yasiyokuwa na dharura yoyote kuyajua na huenda jibu lake likawaudhi waulizaji. Kuna riwaya isemayo kuwa mtu mmoja alimuuliza Mtume (saw): “Ni nani baba yangu?” Mtume akamwambia, “baba yako ni Fulani.” Mwingine akauliza “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ! Baba yangu yuko wapi? Mtume akajibu: “Yuko motoni,” ndipo ikashuka Aya hiyo.
Riwaya nyingine inasema kuwa Mtume alisema: "Mwenyezi Mungu ame- wafaradhishia kuhiji, basi hijini." Wakauliza: “Kila mwaka ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?" Mtume akanyamaza. Wakarudia kuuliza, akasema La; lau ningelisema naam, ingelikuwa wajib.” Ndipo ikashuku Aya hii. Riwaya hii ndiyo yenye nguvu kuliko ile ya kwanza.
Na mnapoyauliza inapoteremshwa Qur'an mtabainishiwa.
Yaani msijikalifishe kuuliza mambo ila baada ya kuteremshwa Qur'an. Mtakapoanza kuuliza Mtume (saw) atawadhirishia mliyokuwa mkiyauliza.
Kwa hali hii, inatubainikia kuwa riwaya ya Hija ndiyo yenye nguvu katika sababu ya kushuka Aya, kuliko riwaya ya kuuliza mababa na wahenga wa Masahaba. Kwa sababu Qur'an inaanza kuleta itikadi na sharia na wala sio kuanzia kwa mababa na mababu wa Masahaba.
Katika Hadith imeelezwa: "Hakika Mwenyezi Mungu ameweka mipaka msiikiuke; amewafaradhishia faradhi msizipoteze; ameharamishia vitu msivifanye; na ameacha vitu vingine si kwa kusahau, lakini ni kwa kuwahurumia, basi vikubalini wala msivifanyie utafiti".
Mwenyezi Mungu amesamehe hayo
Yaani maswali yenu yaliyotangulia, kwa hiyo msiyarudie. Imesemekana kuwa maana yake ni amezuia kutaja vitu mlivyoviulizia, basi nanyi jizuieni wala msijikalifu kuviulizia. Tafsir zote mbili zina uwezekano hazikataliwi na dhahiri ya tamko.
Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira, Mpole.
Humsamehe mkosaji akikosea tena.
Waliyauliza watu waliokuwa kabla yenu kisha wakawa makafiri kwayo.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwakataza kuuliza mambo wasiyokuwa na haja nayo, anawapigia mfano wa watu waliokuwa kabla yao, waliuliza wakang'ang'ania kuuliza. Walipobainishiwa na Mwenyezi Mungu walichukia wakaasi na wakastahiki adhabu. Lau wangeliacha kuuliza ingelikuwa bora kwao.
Wafasiri wamerefusha maneno katika kubainisha makusudio ya watu waliouliza, kisha wakawa makafiri kwa sababu ya kuuliza, lakini Aya haikubainisha. Pamoja na hivyo, tunaweza kusema kuwa watu waliouliza wakawa makafiri kwa sababu ya kuuliza ni wana wa Israil, kwa sababu ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu akiwasimulia:
فَقَدْ سَأَلُوا مُوسَىٰ أَكْبَرَ مِنْ ذَٰلِكَ فَقَالُوا أَرِنَا اللَّهَ جَهْرَةً {153}
مَا جَعَلَ اللَّهُ مِنْ بَحِيرَةٍ وَلَا سَائِبَةٍ وَلَا وَصِيلَةٍ وَلَا حَامٍ ۙ وَلَٰكِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّهِ الْكَذِبَ ۖ وَأَكْثَرُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ {103}
وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا إِلَىٰ مَا أَنْزَلَ اللَّهُ وَإِلَى الرَّسُولِ قَالُوا حَسْبُنَا مَا وَجَدْنَا عَلَيْهِ آبَاءَنَا ۚ أَوَلَوْ كَانَ آبَاؤُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ شَيْئًا وَلَا يَهْتَدُونَ {104}
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا عَلَيْكُمْ أَنْفُسَكُمْ ۖ لَا يَضُرُّكُمْ مَنْ ضَلَّ إِذَا اهْتَدَيْتُمْ ۚ إِلَى اللَّهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًا فَيُنَبِّئُكُمْ بِمَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ {105}