read

Aya 108-110: Msiwatukane

Maana

Wala msiwatukane wale wanaoomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu wasije wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua.

Wamesema kuwa Waislamu walikuwa wakiwatusi makafiri na wao huwajibu kwa kumtukana Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kauli hii haiko mbali sana na maana. Mara nyingi hutokea hivyo kwa wanaotofautiana kidini.

Tamko la Aya pia halilikatai hilo, bali imepokewa kutoka kwa Imam Jafar Aswadiq (as) kwamba aliulizwa kuhusu kauli ya Mtume: “Hakika shirki inajificha zaidi kuliko mtambao wa chungu kwenye jiwe jeusi katika usiku wa giza”

Akajibu: “Waumini walikuwa wakiwatukana wanaoabudiwa na washirikina na wakawa wanamtukana anayebudiwa na waumini. Waumini wakakatazwa kuwatukana waungu wao ili makafiri wasimtukane Mungu wa waumini. Kama kwamba waumni wamemshirikisha Mwenyezi Mungu bila ya kujua.

Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘bila ya kujua’. Ni ishara ya ujinga wa washirikina. Katika Aya kuna ufahamisho wazi kuwa; ambalo lina madhara zaidi ya manufaa ni haramu na kwamba Mwenyezi Mungu hatiiwi anapoasiwa.

Kama hivyo tumewapambia kila umma vitendo vyao.
Maana ya dhahiri ya jumla hii ni kuwa Mwenyezi Mungu kama alivyowapambia vitendo vyao, vilevile amewapambia wengine vitendo vyao hata washirikina. Lakini hakuna mwenye shaka kwamba maana haya sio makusudio, kwa sababu Shetani ndiye anayewapambia washirikina uasi kwa nukuu ya Aya 43 ya Sura hii.

Zaidi ya hayo ni kuwa Mwenyezi Mungu hamwamrishi mja wake ukafiri na ampambie kisha amwadhibu, bali ni kinyume na hayo. Mwenyezi Mungu anasema:

وَلَٰكِنَّ اللَّهَ حَبَّبَ إِلَيْكُمُ الْإِيمَانَ وَزَيَّنَهُ فِي قُلُوبِكُمْ وَكَرَّهَ إِلَيْكُمُ الْكُفْرَ وَالْفُسُوقَ وَالْعِصْيَانَ{7}

“…lakini Mwenyezi Mungu ameipendezesha kwenu imani na akaipamba nyoyoni mwenu na amewaafanya muuchukie ukafiri na ufasiki na uasi” (49:7)

Kwa ajili hii tunatilia nguvu kuichukulia Aya kuwa Mwenyezi Mungu amewaumba watu katika hali inayoona vizuri vitendo anavyovifanya mtu na inayokwenda na desturi na akampa akili ya kupambanua baya na zuri. Lau angeliwaumba katika hali ambayo inaona ubaya wa vitendo vyake vyote, asingelifanya chochote.

Haya ndiyo maana ya kauli yake hiyo Mwenyezi Mungu: ‘Tumewapambia kila umma vitendo vyao’ sawa na kauli yake:

كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ {53}

“Kila kundi linafurahia kwa waliyo nayo” (23:53).

Nasi tunasema: “Kila mtu huridhia amali yake”.

Kisha marejeo yao yatakuwa kwa Mola wao, naye atawaambia yale waliyokuwa wakiyatenda.

Kwa hiyo waumini waache kutukana waungu wa washirikina, maadamu Mwenyezi Mungu atawaadhibu.

Unaweza kuuliza kuwa anayemtukana Mwenyezi Mungu au Mtume wake ni wajibu kumuua, lakini mbona Aya hii inafahamisha kuwa ataachiwa his- abu yake na adhabu yake siku ya Kiyama?

Jibu: Aya hii ilishuka Makka, siku waislamu walipokuwa dhaifu, wakiwa bado hawajapewa ruhusa ya kupigana. Kwa sababu kupigana wakati huo kulikuwa ni kama kujiua. Ama ulipokuwa na nguvu Uislamu, ikawa ni wajibu kutekeleza hukumu ya kuuawa kwa mwenye kutukana; wala hai- juzu kuchelewesha.

Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwa ukomo wa viapo vyao, kuwa ikiwafikia ishara bila shaka wataiamini.

Mwenyezi Mungu (swt) alimpa nguvu Mtume wake Muhammad (s.a.w.) kwa dalili za kutosha juu ya Utume wake, lakini washirikina wa Kikuraishi wakamtaka Muhammad (s.a.w.) muujiza maalum na kufanya ndio sharti la kuamini kwao. Wakaapa kwa kiapo cha nguvu kuwa kama Muhammad atawakubalia maoni yao watamwamini. Ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha Mtume wake kuwaambia:

Hakika ishara ziko kwa Mwenyezi Mungu huziteremsha kwa hoja inayowasimamia wote. Zaidi ya hapo huteremsha au huacha kuteremsha kwa hekima yake na kupitisha kwake.

Waumini wakatamani Mwenyezi Mungu aitikie maombi ya makafiri kwa kuwataka wasilimu na waamini. Mwenyezi Mungu akawaambia kwa kauli yake:

Na ni kitu gani kitakachowatambulisha ya kuwa zitakapowafikia hawataamini?

Yaani kutoka wapi mmejua kuwa Mwenyezi Mungu (swt) akiteremsha muujiza waliotaka makafiri wataacha kufuru yao na inadi yao? Yametangulia maelezo kwa ufafanuzi katika kufasiri Sura hii, Aya 34 – 37 na katika kufasiri Juz.1 (2:118)

Na tutazigeuza nyoyo zao na macho yao kama kama walivyokuwa hawakuamini mara ya kwanza.

Tutazigeuza nyoyo zao na macho yao ni fumbo la kujua Mwenyezi Mungu hakika yao. Dhamir ya kumwamini inamrudia Muhammad au Qur’an.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu anajua kuwa washirikina hawataamini baada ya kushuka muujiza waliotaka, bali wao wataendelea kung’ang’ania upotevu wao wa kwanza waliokuwa nao kabla ya kushuka muujiza wanaoutaka. Wao ni watafutaji wa batili na upotevu, na wala sio watafutaji wa haki na uongofu.

Na tutawaacha katika upotevu wao wakimangamanga.

Yaani baada ya kung’anga’ania upotevu, pamoja na kusimamishiwa hoja, tutawaacha na upotevu wao mpaka ifike siku watakayopata malipo ya amali yao. Yamekaririka maana haya katika Aya kadhaa.